Mataifa 20 Afrika kujadili fursa za mafuta na gesi Zanzibar
Katibu Mkuu Wizara Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Hamad Bakari Hamad akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa mafuta na gesi Afrika unaotarajiwa kufanyika Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Hatua hiyo inazidi kuitangaza Zanzibar na kuipa fursa ya kueleza hatua za uchimbaji wa mafuta na gesi katika kisiwa hicho.
Unguja. Zaidi ya wadau 250 wa sekta ya mafuta na gesi kutoka mataifa 20 ya Afrika wanatarajiwa kukutana Zanzibar kujadili mustakabali wa sekta hiyo, fursa za uwekezaji na namna ya kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya nishati barani humo.
Wadau hao, wakiwamo wawakilishi wa taasisi za kitaalamu za mafuta na gesi, wafanyabiashara, wawekezaji, watafiti na wasomi kutoka vyuo vikuu, watashiriki Kongamano la Pili la New African Dimension of Oil and Gas Conference and Exhibition (NADOGCE), litakalofanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 25 hadi 27, 2026, mjini Unguja.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili, Julai 12, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Hamad Bakari Hamad, amesema kongamano hilo litakuwa jukwaa la kujadili mustakabali wa sekta ya mafuta na gesi Afrika, pamoja na fursa zinazoweza kuchochea maendeleo ya uchumi wa bara hilo.
Amesema kongamano hilo limeandaliwa na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, kwa kushirikiana na Jumuiya ya Vijana wa Kiafrika katika Sekta ya Mafuta na Gesi (Young Africans Petroleum Association–Yapa).
Kwa mujibu wa Hamad, kuwa mwenyeji wa kongamano hilo ni fursa muhimu kwa Zanzibar kujitangaza kimataifa kama moja ya maeneo yanayoendelea katika sekta ya mafuta na gesi, sambamba na kuonesha hatua zilizofikiwa katika shughuli za utafutaji na maendeleo ya rasilimali hizo.
“Ni hatua kubwa kwa Zanzibar kuwa mwenyeji wa kongamano hili. Linatupa nafasi ya kujieleza katika jukwaa la kimataifa na kuonyesha tulipofikia katika shughuli za utafutaji na maendeleo ya mafuta na gesi,” amesema.
Amesema kongamano hilo lenye kaulimbiu “Kuunganisha sekta za mafuta, gesi na nishati safi kwa mustakabali wa Afrika,” litajadili namna Afrika inaweza kutumia rasilimali zake za mafuta, gesi na nishati safi kujenga uchumi imara na kuongeza uwezo wa kujitegemea katika sekta ya nishati.
Hamad amesema Zanzibar imeendelea kupiga hatua katika sekta ya mafuta na gesi, ikiwamo kuendelea na shughuli za uchunguzi wa kina wa kijiolojia (3D seismic surveys), hatua aliyosema inaongeza matarajio ya maendeleo ya sekta hiyo na kuvutia wawekezaji.
Amesema kongamano hilo pia litatoa fursa kwa Zanzibar kueleza maendeleo yaliyofikiwa katika sekta hiyo na kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, ameipongeza Yapa kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuandaa kongamano hilo, akisema ushirikiano huo unachangia kukuza sekta ya mafuta na gesi, pamoja na kuwajengea uwezo vijana wa Afrika wanaoshiriki katika shughuli za sekta hiyo.
Mratibu wa Yapa na NADOGCE, Mudrik Kassim Suleiman, amesema pamoja na mijadala ya kitaalamu, kongamano hilo litakuwa na maonyesho ya siku mbili yatakayowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya mafuta, gesi na nishati.
Amesema maandalizi ya kongamano hilo yamejengwa katika mafanikio ya toleo la kwanza lililofanyika mwaka jana, ambalo lilivutia ushiriki mkubwa wa wadau kutoka mataifa mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Yapa, Jaffar Mohamed Hamza, amesema ni heshima kwa Zanzibar kuwa mwenyeji wa kongamano hilo, akibainisha kuwa taasisi hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa vijana wa Afrika katika sekta ya mafuta na gesi na kuleta fursa za maendeleo ndani ya bara hilo.
Miongoni mwa mataifa yaliyothibitisha kushiriki kongamano hilo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Benin, Algeria, Libya, Cameroon, Tunisia na Uturuki, pamoja na nchi nyingine za Afrika.