Mwigulu ataja sababu Tanzania kuendelea kukopa

Muktasari:

  • Serikali imesema inakopa kwa sababu kuna miradi mikubwa inayohitaji fedha nyingi kwa wakati mmoja kutekelezwa

Dar es Salaam. Serikali imesema nchi inaendelea kukopa fedha kwa ajili ya utekelezaji miradi ya kimkakati kwa sababu ina uwezo wa kulipa.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Februari 23, 2024 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, akisema kadri nchi inavyokuwa tajiri ndivyo viwango vyake vya madeni huwa vikubwa.

Kauli hiyo ameitoa wakati ambao Serikali imeongeza matumizi ya fedha kwa ajili ya kulipa madeni kutoka Sh9.1 trilioni mwaka 2022/23 hadi Sh10.4 trilioni kwa mwaka 2023/24.

Dk Mwigulu amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akisaini mikataba miwili ya mikopo yenye thamani ya Sh398.7 bilioni.

Mikataba hiyo ni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Tabora – Kigoma – Uvinza – Malagarasi, na mkataba wa kuiwezesha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dk Mwigulu amesema ukiona nchi inakopa maana yake anayekopesha anajua kuwa atarejeshewa fedha zake.

"Mtu mwenye uwezo ndiye mwenye deni kubwa hata mataifa yale tajiri duniani ndiyo yenye madeni makubwa zaidi, zile nchi zilizoendelea kabisa zina madeni makubwa kuliko Tanzania," amesema.

Amesema watu wanapaswa kuelewa nchi itakapokuwa tajiri zaidi na deni litakuwa kubwa kuliko sasa, na inakopa kwa sababu ina uwezo wa kulipa.

"Tunazichukua tufanyie kazi, fedha zilezile ambazo tungechukua kidogo-kidogo kufanyia kazi kwa miaka 40, tunachukua mikopo kwa sababu tuna fedha ya kurejesha, badala ya kujenga reli kwa kila mwezi kukusanya hela tunachukua fedha tunajenga halafu reli ikiwa inafanya kazi tunalipa deni," amesema.

"Tunakopa kwa sababu tuna miradi mikubwa inayohitaji fedha nyingi kwa wakati mmoja kutekelezwa.”

Amesema hadi sasa madeni ambayo ni mzigo mkubwa kwa nchi ni yaliyokopwa kwa masharti ya kibiashara.

Dk Mwigulu amesema Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani alitaka mikopo yenye riba nafuu, akieleza hiyo ndiyo sababu ya AfDB kushiriki ujenzi wa SGR na Benki ya Dunia (WB).

"AfDB na WB ina mikopo ya chini ya asilimia mbili lakini benki ya biashara unapata asilimia 10 hadi 11 mara tano zaidi," amesema Dk Mwigulu.

Amesema hilo pia linafanyika kwa sababu makandarasi si mali ya Serikali, bali ni watu wenye kazi ndani ya nchi na nje ya nchi, hivyo ni ngumu kumuweka kwa miaka 60 akijenga mradi wako.

Taarifa ya wizara hiyo ya Juni 7, mwaka jana, inaeleza ilifanya tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa kwa miaka 20 ijayo, kuanzia 2022/23 hadi 2041/42.

Matokeo ya tathmini yanaonyesha deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Dk Mwigulu, thamani ya sasa ya deni la Serikali dhidi ya pato la Taifa ni asilimia 31.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55.

Kuhusu mikataba

Dk Mwigulu amesema katika kiasi cha fedha kilichotolewa, Sh231.3 bilioni ni kwa ajili ya kuanzia ujenzi wa reli ya kisasa awamu ya sita na saba yenye urefu wa kiliomita 567.

Mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka saba kuanzia mwaka 2024 hadi mwaka 2031.

"Uwekezaji huu wa reli, utawezesha kuunganishwa na Bandari ya Dar es Salaam kupitia mradi unaondelea wa ujenzi wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam – Morogoro – Makutupora – Isaka – Tabora.

Amesema lengo ni kuiunganisha Tanzania na Burundi kupitia reli ya kisasa kutoka Malagarasi hadi Musongati - Burundi yenye urefu wa kilomita 84.

Kuhusu mkopo wa kilimo, Dk Mwigulu amesema Sh166.4 bilioni zinalenga kuwezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya shughuli za kilimo zinazolenga kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kukuza biashara ya bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi.

"Pia, itaongeza ajira zitakazoinua uchumi katika ngazi ya mtu mmoja, familia na Taifa kwa ujumla," amesema.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kukamilika kwa ujenzi wa reli ya Uvinza hadi Musongati kutawezesha kufikia mgodi wa madini ya nikeli uliopo Musongati nchini Burundi unaokadiriwa kuwa na hifadhi ya tani milioni 150 za madini hayo pamoja na kobati na shaba.

“Reli hii inatarajiwa kusafirisha madini tani milioni tatu kwa mwaka," amesema Profesa Mbarawa.

Dk Patricia Laverley, Meneja Mkazi wa AfDB Tanzania amesema benki hiyo iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuendelea kujenga maendeleo ya watu.

Amesema mradi wa SGR utachangia kuimarisha uhusiano wa kikanda na kuunga mkono dira ya Umoja wa Afrika ya 2063 ya Afrika jumuishi.

"SGR itasaidia Serikali ya Tanzania kufikia azma yake ya maendeleo ya kubadilisha ukanda wa kati wa usafiri kuwa ukanda wa kiuchumi ili kusaidia biashara huria ya Bara la Afrika," amesema.