Mwigulu aishauri kampuni ya madini kuiuzia Serikali dhahabu

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba (katikati), akimshuhudia ofisa mkuu wa masuala ya fedha wa Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Anglo Gold Ashanti, inayomiliki Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Gillian Doran (kushoto) akisaini kitabu cha wageni, wakati uongozi wa kampuni hiyo ulipomtembelea jijini Dodoma, na kujadili masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya kampuni hiyo na Serikali

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema hatua ya Serikali kununua dhahabu itaifanya kuwa na chanzo cha uhakika cha kupata dhahabu.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ameushauri uongozi wa Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Anglo Gold Ashanti, inayomiliki Mgodi wa dhahabu wa Geita (Geita Gold Mine-GGM), kuanza kuiuzia Serikali dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania,  ili kuiwezesha kuhifadhi dhahabu kama akiba ya fedha za kigeni.


Dk Nchemba ametoa ushauri huo jijini Dodoma hivi karibuni alipokutana na kufanya mazungumzo na Ofisa Mkuu wa masuala ya fedha wa kampuni hiyo, Gillian Doran, ambapo walijadili masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya kampuni hiyo na Serikali.


Amesema hatua hiyo itaifanya Serikali kuwa na chanzo cha uhakika cha kupata dhahabu pamoja na kuwatumia wachimbaji wadogo, ambao hivi sasa ndio wanaofanya biashara ya kuiuzia dhahabu Benki Kuu ya Tanzania.


“Lengo la hatua ya Serikali ya kuanza kuhifadhi dhahabu kama fedha za kigeni ni kuifanya nchi kuwa na chanzo cha uhakika cha fedha hizo,  kitakachotumika kama dhamana wakati inapohitaji fedha hizo kwa ajili ya matumizi mbalimbali badala ya kutegemea mikopo” amesema Dk Nchemba.


Aidha, Dk Nchemba amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ameilekeza Wizara ya Fedha kuanza kununua dhahabu na kuitunza kama fedha za kigeni, maelekezo ambayo wameyatekeleza, na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza kununua dhahabu.


“Akiba ya dhahabu itatusaidia kununua bidhaa muhimu zitakazokuwa zinahitajika nchini ikiwemo mafuta, wakati wa changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni na hatua hii ina faida kubwa kiuchumi,” amesisitiza Dk Nchemba


Vilevile Dk Nchemba amesema mitambo ya kuchenjua dhahabu iliyojengwa Geita na Mwanza, itakuwa na manufaa endapo dhahabu inayozalishwa nchini itachakatwa na kuongezwa thamani hapahapa na kuchangia pato la Taifa.


Katika mwaka wa fedha 2023/2024, BoT imejipanga kununua tani sita za dhahabu kwa ajili ya kuweka akiba katika mfumo wa fedha za kigeni.


Kwa upande wake Gillian Doran ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na kuahidi kuwa yataimarisha zaidi ushirikiano na Serikali kupanua uzalishaji wa madini nchini.


Ameahidi kuufanyia kazi ushauri uliotolewa wa kuiuzia Serikali dhahabu kama njia ya kutunza fedha za kigeni, lakini pia kuendelea kusaidia huduma za kijamii katika eneo la mgodi wa dhahabu wa Geita kwa manufaa ya wananchi.