Tanzania kupokea uwekezaji mwingine utafiti wa madini

Muktasari:

  • Kampuni ya AngloGold Ashanti inayomiliki kampuni ya mgodi wa dhahabu mkoani Geita (GGML), inatarajia kuongeza uwekezaji nchini katika eneo la utafiti wa madini.

Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kupokea uwekezaji katika eneo la utafiti wa madini, unaotarajiwa kufanywa na kampuni ya AngloGold Ashanti inayomiliki mgodi wa dhahabu mkoani Geita (GGML).

Kampuni hiyo ya utafiti wa madini ya Greenfields Mineral Exploration Limited, inatarajiwa kuanzishwa nchini ili kushirikiana na GGML katika kuongeza uchimbaji wa dhahabu.

Ikumbukwe AngloGold Ashanti inashika nafasi ya nne kwa uzalishaji wa madini duniani, ikifanya shughuli hizo katika mataifa ya Australia, Marekani na Colombia.

Taarifa kuhusu ujio wa kampuni hiyo, imetangazwa leo Jumatatu, Januari 16, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa AngloGold Ashanti, Alberto Calderon alipozungumza kuhusu maandalizi ya sherehe za kumbukumbui ya miaka 25 ya GGML.

Kulingana na mkurugenzi huyo, ujio wa kampuni hiyo nchini  utashirikiana na kampuni ya GGML ili kuiongezea ufanisi katika uchimbaji wa rasilimali hiyo.

"Kwa kuzingatia hadhi yake (GGML) kama mojawapo ya mchimbaji bora wa dhahabu duniani, ni wazi tungependa kuongeza uwepo wetu hapa Tanzania na viwango vya uzalishaji nchini, ndiyo maana tunafanya uwekezaji huu kutafuta hifadhi nyingine ya dhahabu ya kiwango cha kimataifa,” amesema.

Hata hivyo, amesema utekelezaji wa shughuli za kampuni hiyo unatarajiwa kuanza na miradi mitatu katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga na Singida, inayotajwa kuwa na hifadhi ya dhahabu kama Geita.

Mwaka 2023 kampuni hiyo iliwekeza Dola za Marekani milioni 35 katika utafiti kwenye eneo la mgodi pekee na imejitolea kuwekeza zaidi ya Dola za Marekani 31 milioni kwa mwaka 2024, kama sehemu ya kampeni yake ya kupanua zaidi maisha ya mgodi huo.

"Tumejitolea kuimarisha shughuli za GGML na wadau wake nchini Tanzania kuwa endelevu zaidi. Mgodi huu upo kwenye mpango wetu wa muda mrefu katika kampuni zetu zinazomilikiwa na AngloGold Ashanti," amesema.

Mkurugenzi huyo amesema GGML inatekeleza mradi wa kuunganisha mgodi huo kwenye gridi ya Taifa ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Mpango huo, amesema sio tu kwamba utapunguza nusu ya gharama ya uendeshaji mgodi, pia utakuwa na uwezo wa kupunguza utoaji wa kaboni kwa 81Kt CO2-e ifikapo mwaka 2030.

“GGM tangu kuanzishwa kwake imeshirikiana na Serikali kufadhili na kutekeleza miradi ya uwekezaji ya kijamii katika sekta za kimkakati kama vile elimu, afya, maji na barabara,” amesema.

Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa na mgodi huo ni ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu inayochukua zaidi ya wanafunzi 1,000 kuanzia shule za msingi hadi sekondari.

Mwingine ni mradi wa maji safi wa Mji wa Geita uliosaidia kuinua idadi ya kaya zinazopata maji safi na salama kwa zaidi ya asilimia 65.

Ubora katika utendaji wake, ndiyo ulioifanya GGML kupata tuzo mbalimbali zikiwemo za utunzaji wa mazingira, ukuzaji wa biashara za ndani na usalama kazini.