Wafanyakazi kampuni ya uchimbaji madini wapima VVU

Baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa GGML wakisubiri huduma ya upimaji wa VVU inayotolewa mgodini hapo ikiwa ni mwendelezo wa kuandhinisha siku ya Ukimwi duniani inayoadhimishwa kila mwaka Disemba Mosi.
Muktasari:
- Wafanyakazi wa Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Geita (GGML) hufanya vipimo vya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kila mwaka ili watambue afya zao.
Geita. Imeelezwa kuwa wafanyakazi 2,500 wa Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Geita (GGML), wamejitokeza kupima maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Desemba 12, 2023 wakati wa upimaji huo, Dk Subira Joseph kutoka hospitali ya mgodi huo amesema kampuni hiyo hufanya vipimo kwa wafanyakazi wake kila mwaka ili watambue afya zao.
Dk Subira amesema wanapojua hali zao, ni rahisi kujilinda wasipate maambukizi na kwa wale watakaobainika kuambukizwa, wanapata nafasi ya kuanza kutumia dawa za kufubaza maambukizi hayo mapema.
“Tuko kwenye kampeni ya kupima VVU, ni ya kila mwaka. Mwaka huu tumeongeza kipimo cha Kifua Kikuu, lengo ni kufanya ‘awareness’ kwa wafanyakazi kuhusu VVU. Desemba mosi kila mwaka ni Siku ya Ukimwi Duniani, sisi GGML huwa tunachukua wiki mbili kupima wafanyakazi wetu,” amesema Dk Subira.
Amesema maambukizi mapya ya VVU yamepungua kutoka 0.26 mwaka 2021 hadi kufikia 0.16 mwaka 2022.
“Hadi sasa kati ya watu 2,500 waliopimwa ni chini ya 10 wamebainika kuwa na maambukizi mapya, na mfanyakazi anayebainika kuwa na VVU, huendelea na kazi kawaida; ila hupewa elimu ili aanze dawa mapema ya kufubaza virusi,” amesema.
“Na ili uwepo usiri juu ya taarifa zao, tunawatoa madaktari kutoka hospitali za Serikali ambao hawawafahamu wafanyakazi.”
Akizungumzia kuhusu kuongeza kipimo cha Kifua Kikuu (TB), Dk Subira amesema maeneo ya uchimbaji madini ya dhahabu, huwa na vumbi ambali likimpata mtu kwa kiasi kikubwa linaweza kumsababishia ugonjwa huo.
Mfanyakazi wa mgodi huo, Juma Hassan amesema upimaji huo unawasaidia kujua afya zao, hivyo kuishi kwa tahadhari.
Veronika Joseph ambaye ni mfanyakazi, amepongeza uamuzi huo wa kuleta wataalamu kutoka nje kwa ajili ya kuwachukua vipimo.
“Kwanza linaleta ujasiri kwamba anayekuhudumia hamfahamiani, pia inasaidia maana wengi wetu tunachukua muda mrefu bila kujua afya zetu kutokana na kukosa muda wa kwenda kupima na matokeo yake mtu unaishi kwa wasiwasi,” amesema.
Mkoa wa Geita una wakazi milioni 2.9 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na hali ya maambukizi ya VVU kwa mkoa huo ni asilimia 4.9