Kuchenjua dhahabu Geita yaingiza Serikali Sh3.2 bilioni kila mwezi

Waziri wa Madini, Antony Mavunde (katikati alivaa shati jeupe) akikata utepe kuzindua kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha kampuni ya Jema Africa LTD kilichopo eneo la Mpomvu Wilaya ya Geita. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Jema Africa LTD, Jumanne Mokiri na kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

Kwa miaka miwili iliyopita, Mkoa wa Geita ulizalisha kilo 47,000 za dhahabu zenye thamani ya zaidi ya Sh5.053 trilioni, kati ya hizo, kilo 11,000 zikizalishwa na wachimbaji wadogo.

Geita. Uwekezaji na mabadiliko ya sheria katika sekta ya madini nchini imeiwezesha Serikali kukusanya zaidi ya Sh3.2 bilioni kila mwezi kutoka kwenye mitambo 57 ya kuchenjua na kuchakata dhahabu mkoani Geita.

Mapato haya ni sehemu ya ufanisi wa Mkoa wa Geita ambao Kitaifa umepewa lengo la kukusanya maduhuli ya Serikali ya Sh243 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023/24 kupitia sekta ya madini.

Akizindua ofisi na mtambo wa kuchenjua dhahabu wa kampuni ya Jema Africa LTD Novemba 12, 2023, Waziri wa Madini, Antony Mavunde ameupongeza uongozi wa Serikali, taasisi zake na wadau wa madini kwa kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji na biashara ya madini.

Pamoja na pongezi hizo, Waziri Mavunde amewahimiza viongozi na wadau wa sekta ya madini mkoani Geita kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za biashara ya madini, hasa ya shughuli zote za kibiashara kufanyika kupitia masoko rasmi ya madini.

‘’Kuna tabia imeanza kuibuka ya baadhi ya watu wachache kuuza madini nje ya masoko rasmi na hivyo kuikosesha Serikali mapato; ni lazima sote tushirikiane kudhibiti vitendo hivyo kwa manufaa na faida ya Taifa,’’ amesema Mavunde

Ameiahidi kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua shahiki za kisheria ikiwemo kufungia au kufuta leseni za wafanyabiashara watakaothibitika kujihusisha na mtandao wa kutorosha madini.

‘’Nilikuwa Wilaya ya Chunya hivi karibuni ambako tumebaini upotevu wa zaidi ya Sh900 milioni kutokana na utoroshaji wa madini…Wilaya ya Kahama pia kunadaiwa kuwepo vitendo hivyo. Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya wote watakaothibitika kujihusisha na vitendo hivyo,’’ amesema Waziri huyo

Mkurugenzi wa Jema Africa LTD, Jumanne Mokiri amehakikishia Waziri Mavunde kuwa kampuni hiyo itaendelea kuzingatia na kufuata sheria za madini na uhifadhi wa mazingira kulingana na maelekezo ya Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC).

‘’Katika hili, kampuni yetu imetekelezaji agizo la Serikali la kuhamishia mtambo wetu wa kuchenjua dhahabu eneo la Mpomvu Wilaya ya Geita kutoka kwenye maeneo ya makazi ili kulinda afya ya watu. Tumetumia zaidi ya Sh1 bilioni kutekeleza agizo hilo,’’ amesema Mokiri

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ametumia hafla hiyo kuwahimiza wote wenye mitambo ya kuchenjua dhahabu katika maeneo ya makazi kuyahamishia eneo la Mpomvu kulinda usalama na afya ya wananchi.

Kuhusu uzalishaji, Shigella amesema kwa miaka miwili iliyopita, mkoa huo umezalisha kilo 47,000 za dhahabu zenye thamani ya zaidi ya Sh5.053 trilioni, kati ya hizo, kilo 11,000 zikizalishwa na wachimbaji wadogo.

Kutokana na mchango wa wachimbaji wadogo wa madini nchini, Serikali imefuta leseni kadhaa za utafiti na kugawa maeneo hayo wa wachimbaji wadogo ambao walipewa takribani leseni 2,411.