Dk Mwigulu abanwa fedha za matengenezo ya barabara

Muktasari:

  • Bunge limeazimia Serikali ikamilishe utoaji wa fedha za dharura za utengenezaji wa barabara kama zilivyoombwa na Tarura na Tanroads

Dodoma. Wabunge wamemwashia moto Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba kuhusu ahadi yake ya kupeleka fedha za dharura za matengenezo ya barabara zilizoharibiwa na mvua.

Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) uliomba Sh66 bilioni, huku Wakala wa Barabara za Mijini na Vijini (Tarura) ukiomba Sh65 bilioni kwa ajili ya matengenezo hayo.

Hatua hiyo ilitokana na mbunge wa Rorya, Jafar Chege kuomba mwongozo wa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson leo Alhamisi Februari 15, 2024 baada ya kipindi cha kuwatambulisha wageni kumalizika bungeni.

Akiomba mwongozo, Chege amesema mawasiliano ya barabara katika maeneo mengi nchini yamekatika kutokana mvua zinazoendelea kunyesha.

Chege  amesema Januari 31, 2024, Dk Mwigulu alitoa ahadi kuwa Sh131 bilioni za dharura zitakuwa zimeenda kabla yakumalizika kwa Bunge lakini hadi leo hazijaenda.

Baada ya Spika Tulia kuruhusu suala hilo kujadiliwa, mbunge wa viti maalumu, Sophia Mwakagenda amesema Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa inayozalisha vyakula kwa wingi lakini barabara zake zimeharibika,  hivyo wakulima kushindwa kusafirisha mazao na bei  kupanda kwa sababu mazao yameshindwa kufika sokoni.

Amesema fedha za ukarabati zilizoahidiwa zitapelekwa kabla ya kumalizika kwa mkutano wa 14 unaoisha kesho hazijapelekwa, hivyo akamtaka Spika kutoa onyo kali kwa Serikali.

Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa amesema kuna mikataba iliyokuwa ikitakiwa kusainiwa na Tarura lakini haikusainiwa kwa sababu wakala hana fedha.

“Ndiyo maana tunataka kujua pesa iko wapi, upande wa Tarura wamejitahidi kutangaza hizo barabara. Hawajasaini mikataba, ukiuliza unaambiwa wanasema tumeambiwa tusubiri hali ya fedha ndipo tusaini,” amesema akitaka Serikali imese itapeleka lini fedha ili wabunge watakaporudi majimboni wawaambie wananchi kwenye mikutano ya hadhara.

Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda amesema Mkoa wa Tabora umetenganishwa na Mbeya baada ya barabara kukatika vipande sita, hivyo kutopitika.

“Tunahitaji fedha ziende Tanroads na Tarura. Kati ya kilometa 900 zinazosimamiwa na Tarura kilomita 400 hazipitiki katika jimbo langu. Serikali ipeleke fedha ili barabara ziweze kupitika,” amesema.

Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu amesema maeneo mengi jijini Dar es Salaam hali ya barabara ni mbaya na hazipitiki, akitaka Dk Mwigulu kuona umuhimu wa kupeleka fedha.

Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde ameiomba Serikali kuthamini watu wa vijijini kama inavyowathamini wanaoishi mijini.

“Kuna madaraja sugu vijijini kila mwaka lazima yakatike. Ujenzi wa madaraja hayo lazima uwe tofauti na ule wa ya mijini. Tunapozungumza hivi sasa Daraja la Manda limekatika, Daraja la Mlowa limekatika lakini ujenzi wake baada ya mwaka linakatika,” amesema Mtemvu.

Ameomba Serikali ipitie madaraja yanayokatika kila mwaka ili wayatengeneze kwa uimara zaidi.

Wengine waliounga mkono na kuchangia hoja hiyo ni mbunge wa Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris, Stella Manyanya (Nyasa), John Kanyasu (Geita Mjini) na Abdallah Chikota (Mtwara Vijijini).

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Serikali imefanya tathimini ya uharibifu wa barabara nchi nzima na kubainisha hasara ya Sh200 bilioni ambayo imetokana na kuharibika kwa miundombinu ya barabara na madaraja.

“Lakini kutokana na mvua bado zinaendelea kunyesha yapo masuala ya kitaalamu, kuna mambo tunaweza kuyafanya kurudisha mawasiliano lakini kuna mambo inabidi tusubiri mvua iishe ili kurudisha kama hali ilivyokuwa kawaida,” amesema Bashungwa.

Amesema waliomba Sh66 bilioni (Tanroads) za dharura ili waendelee kurejesha miundombinu kipindi cha mvua na kwamba Wizara ya Fedha inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo hayo.

Hata hivyo, Dk Mwigulu amesema Serikali inaungana na wabunge kushughulikia miundombinu iliyoharibika.

Amesema Serikali imeona changamoto hiyo mapema na Rais Samia Suluhu Hassan alitoa tamko mara tu mvua zilipoanza kunyesha la kuwaelekeza watoe fedha kwa ajili ya ukarabati huo.

“Tumetoa fedha kwa mafungu, mwanzo tulitoa Sh21 bilioni lakini leo tutatoa Sh30 bilioni. Kinachojitokeza baada ya kuwa tumeshaongeza sana fedha kwenda kwenye ujenzi wa barabara sasa tumekuwa na barabara nyingi zenye urefu mkubwa,” amesema.

Dk Mwigulu amesema kutokana na kujengwa kwa barabara nyingi uharibifu wa barabara unakuwa mkubwa kuliko bajeti ya awali iliyopangwa.

Akimpatia taarifa, mbunge Condester Sichwalwe amesema Serikali iliitengea Tarura Sh808 bilioni lakini hadi sasa wamepeleka Sh89 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 12.

Amesema hoja ya wabunge ni kwa nini Serikali hajapeleka fedha zilizotengwa na Bunge, wakati imebaki miezi minne kukamilisha mwaka wa bajeti wa 2023/24.

Akiendelea kuchangia, Dk Mwigulu amesema mvua zimezuia upelekaji wa fedha kwenye utengenezaji wa barabara.

Amesema wameshapeleka Tarura zaidi ya Sh300 bilioni na zilizobakia Sh600 bilioni zipo lakini mvua zimezuia.

Dk Mwigulu amesema katika bajeti ijayo watakuja na fungu la ukarabati wa barabara na akawaomba wabunge kupitisha.

Akimpa taarifa mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka amesema bajeti ilipitishwa Julai mwaka jana lakini hadi kufikia Desemba 2023,  fedha hizo zilikuwa hazijaenda wakati mvua zilianza Desemba.

“Labda useme (Dk Mwigulu) kuwa TMA (Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania) walivyosema kutakuwa na mvua kubwa basi mkaweka hii (bajeti ya Tarura) fedha hadi mvua ipite,” amesema.

Dk Mwigulu amesema fedha za ujenzi wa barabara haziendi zote kama zilivyopangwa katika bajeti kwa mara moja bali zinaenda kwa mafungu.

Kauli hiyo ilimfanya Spika wa Bunge, Dk Tulia kuingilia kati akitaka kufahamu kiasi kilichopelekwa kwa Tarura hadi kufikia leo Februari 15, 2024.

Akijibu Dk Mwigulu amesema fedha zilizopelekwa ni Sh309 bilioni na P4R wametoa Sh350 bilioni.

Amesema mvua zitakapoisha makandarasi waliopo nchi nzima wataendelea na kazi ya ujenzi wa barabara.

Hata hivyo, Dk Tulia alimhoji waziri huyo iwapo Sh309 bilioni ni sehemu ya fedha zinazopelekwa kwa ajili ya dharura.

Akijibu Dk Mwigulu amesema Sh309 bilioni ni za bajeti ya mwaka 2023/24.

Amesema fedha za dharura walizoomba Tanroads ni Sh66 bilioni wakati Tarura waliomba Sh65 bilioni, hivyo kufanya jumla ya fedha zilizoombwa na taasisi hizo mbili kuwa Sh131 bilioni.

Amesema tayari wamepeleka Sh21 bilioni na leo anadhani watapelekewa Sh30 bilioni kwa Tarura, huku Tanroads wakiwa hawajapelekewa hata kidogo.

Akihitimisha hoja, Chege amesema changamoto ni pale wanapotenga fedha kwenda katika miradi ya maendeleo lakini hazifiki kwa wakati.

“Hata tukizungumza kwa uzuri gani kuwa fedha imeongezeka kutoka Sh300 bilioni kwenda Sh800 bilioni na ushee kama haiendi kwa wananchi bado haionekani na hatuwezi kupata matunda,” amesema Chege.

Amesema hoja yake ni kuhakikisha Sh818 bilioni iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa upande wa Tarura inakwenda yote.

“Hatuwezi kujitetea kwa hoja kuwa sababu ya mvua zinanyesha kwa kuwa tulikuwa na miezi sita ya utekelezaji. Pia, kuna makandarasi wameshafanya kazi huko wanadai fedha zao,” amesema.

Amesema hoja yake nyingine anakwenda kuwaambia nini wananchi wakati Dk Mwigulu aliwaambia watulie kwa sababu fedha zote Sh131 bilioni zilizoombwa kwa ajili ya dharura zitakuwa zimefika kabla ya Bunge kuisha.

Dk Tulia alilihoji Bunge ambalo liliazimia Serikali ikamilishe utoaji wa fedha za dharura za utengenezaji wa barabara kama zilivyoombwa na Tarura na Tanroads.