Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Namna ya kufanya uwekezaji salama, kuepuka matapeli

Katika miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la mitandao ya utapeli inayojificha katika muundo wa uwekezaji. Hii imekuwa inajirudia mara kwa mara na watu wengi wamejikuta wanapoteza fedha zao kutokana na kukosa elimu ya kutosha kuhusu uwekezaji na kutambua dalili za utapeli.

Kwa bahati mbaya hii imefanywa kwa vivuli mbalimbali, mfano ya kilimo, uchumi, uwekezaji na ujasiriamali. Kuna wakati pia inahusisha watu muhimu kwenye jamii kama viongozi wa dini na wanasiasa. Na kwa imani watu wanafuata mkumbo na kujikuta wameangukia kwenye utapeli wa namna hii. Ni muhimu kuelewa viashiria vya hatari na kujua njia salama za kuwekeza.

Mosi. Tambua dalili za utapeli. Hizi zinafuatana na ahadi za faida kubwa kwa muda mfupi. Kwa mfano unaweza kuambiwa kuwa wekeza shilingi milioni moja upate milioni tano kwa miezi sita. Unaweza kuletewa ushuhuda wa watu lukuki ambao hawajui waliofanikiwa na mpango huo.

Kuna uwekezaji wa namna hii uliokwishafanyika hapa nchini na ulionekana ukiwa na utapeli mkubwa na mwisho wake kulikuwa na majuto mengi sana ya kupoteza fedha na mitaji. Hakuna uwekezaji halali unaoweza kukupatia faida kubwa kwa muda mfupi bila kuwa na hatari kubwa.

Pili. Usikubali shinikizo la kuwekeza haraka. Matapeli hutumia mbinu ya kuwahimiza watu kuwekeza haraka, wakidai kuwa fursa inaisha au bei itapanda, ama anayewekeza wa kwanza atapata ‘bonus’ fulani ambayo haitachukua muda mrefu. Hii ni mbinu ya kuwafanya watu wafanye maamuzi bila kufikiri kwa kina. Uwekezaji halali daima utakupa muda wa kutosha kufanya utafiti na kupanga njia nzuri ya kusaidia kujua namna ya kufanya maamuzi sahihi.

Tatu. Fanya Uhakiki wa Uwekezaji. Uwekezaji wowote lazima uwe na kibali kupitia mamlaka ya Soko la Hisa na Mitaji. Wawekezaji wa naendesha uwekezaji wa kitapeli, hawana ridhaa ya kutunisha mitaji kutoka kwa mamlaka husika. Hawako wazi kuhusu jinsi wanavyopata faida kubwa wanazodai. Huwa hawana ofisi za kudumu na huwezi kuwapata wahusika wenyewe kirahisi ili kujibu maswali husika.

Ili kuepuka utapeli wa uwekezaji, ni vizuri kufanya utafiti kabla ya kuwekeza. Tafiti kuhusu kampuni na wamiliki wake. Angalia kama wana ofisi halisi, leseni zinazotakiwa, na historia inayoweza kuthibitishwa. Wasiliana na wataalamu wa fedha, wahasibu, au washauri wa uwekezaji wenye sifa zinazotambulika. Unaweza kuwapata hawa washauri kwenye benki yako, kwenye vyuo vya elimu, au vyombo vya habari. Usitegemee tu ushauri wa rafiki, watu wakarimu au mitandao ya kijamii.

Ni vizuri pia kujielimisha kuhusiana na njia halali za uwekezaji, kama uwekezaji kwenye mifuko ya fedha kama UTT-AMIS, Dhamana za serikali, kampuni zilizosajiliwa, uwekezaji kwenye mali ambazo hazihamishiki kama ardhi na nyumba, pia kuwekeza kwenye biashara ndogondogo.

Uwekezaji mzuri ni ule unaokupa faida na pia kulinda mtaji. Uwekezaji halali unahitaji muda, uvumilivu na mipango madhubuti. Epuka vishawishi vya utajiri wa haraka na badala yake, jenga msingi imara wa kifedha hatua kwa hatua. Pia kumbuka kwamba fedha yoyote unayopata kwa urahisi, inaweza kupotea kwa urahisi zaidi. Hakikisha kuwa ukiamua kuwekeza usiweke fedha zako zote katika uwekezaji wa aina moja.