NBS yataja viashiria vinne vya kukuza uchumi wa Tanzania

Dodoma. Ofisi ya Taifa ya Takwimu imetoa taarifa ya viashiria vinne vya ukuaji wa uchumi huku ikitaja kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme kwa asilimia 9.5, baada ya Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) kuanza uzalishaji na kuuingiza kwenye gridi ya Taifa.

Taarifa hiyo imetolewa jana, Mei 10, 2024 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Takwimu za uchumi kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu,  Daniel Masolwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu viashiria vya ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024, kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2023.

Masolwa amesema kutokana na ongezeko la uzalishaji wa umeme katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, ambacho ndicho bwawa lilianza kuzalisha, umeme uliongezeka kwa asilimia 9.5 kutoka kilowati 2.7 bilioni kwa saa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2024, kutoka kilowati 2.5 bilioni kwa saa kipindi kama hicho mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la kilowati 236.8 milioni kwa saa.5

“Kiasi kikubwa cha umeme uliozalishwa katika kipindi hicho mwaka 2024 kilitokana na chanzo cha gesi asilia kwa asilimia 65, chanzo cha maji kwa asilimia 33.6 na mafuta kwa asilimia 1.4, wakati uzalishaji wa umeme kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2023 ulikuwa asilimia 73.5 kwa gesi, maji asilimia 25.7 na mafuta asilimia 0.8,” amesema Masolwa.

Amesema kutokana na takwimu hizo, kampeni ya kuhakikisha nchi inatumia nishati safi inakwenda vizuri kwa sababu mafuta yanapotumika ni miongoni mwa vyanzo vya uchafuzi wa mazingira, lakini umeme unaozalishwa na maji ni rafiki kwa mazingira.

Kiashiria kingine alichokitaja, ni kuongezeka kwa idadi ya watalii kwa asilimia 27.2 kutoka 409,000 mwaka 2023 hadi 520,000 mwaka 2024.

Amesema idadi kubwa ya watalii walioingia nchini kwa kipindi hicho ni kutoka nchi za Italia, Ufaransa na Marekani nchi ambazo kwa kawaida huwa zinaleta watalii wengi nchini.

Kwa upande wa Afrika nchi ambazo zilileta watalii wengi nchini ni Burundi, Kenya na Zambia.

Aidha, Masolwa amesema kwa Machi pekee idadi ya watalii waliofika nchini walikuwa 155,000  ikilinganishwa na 118,000 mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia 31.

Amesema idadi ya watalii walioingia Machi ni kubwa  kulinganisha na wale walioingia Januari na Februari kwa pamoja.

Mkurugenzi huyo amesema kiashiria kingine ambacho kwa sasa ni miongoni mwa vichocheo vya ukuaji wa uchumi ni huduma za mawasiliano ya mtandao wa intaneti na kuongea katika kupashana habari, mafunzo na katika shughuli nyingine za kiuchumi.

Amesema katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2024 muda wa kutumia huduma za maongezi uliongezeka hadi dakika bilioni 34.9 ukilinganisha na dakika bilioni 32.04, sawa na ongezeko la asilimia 9.4

“Ukiona huduma za mawasiliano matumizi yake yanazidi kuongezeka kati ya kipindi kimoja hadi kingine ni kiashiria kizuri cha kuonyesha kwamba huduma hizi zinatumika lakini tunaziangalia katika shughuli za kukuza uchumi na kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja,” amesema Masolwa

Kiashiria kingine ni kiasi cha mvua kilichopatikana kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2024, ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2023 ambapo kiasi cha mvua kiliongezeka kwa asilimia 48.1, ukilinganisha  na mwaka 2023.

Amesema kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2024 nchi ilipata milimita za mvua 15,393 ukilinganisha na milimita 10,396 kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita.

“Mvua ni nzuri kwa ajili shughuli za uzalishaji wa  kilimo na pia uzalishaji wa umeme lakini ikizidi ule wastani unaotakiwa ina madhara yake kama mnavyojua mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara imeathirika kutokana na mvua ambazo zimezidi wastani,” amesema Masolwa.

“Kwa hiyo hizi mvua ambazo zimezidi wastani zimeathiri baadhi ya maeneo lakini kwa kiasi kikubwa sehemu kubwa ya nchi imeweza kuzitumia kufanya shughuli za uzalishaji wa mazao ya kilimo lakini vilevile kwenye bwawa letu la mwalimu Nyerere ilifikia kipindi mpaka wakaamua kuyapunguza kutokana na kwamba mvua zilikuwa kubwa.”