Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu za kufungua uchumi mkubwa wa kidijitali nchini

Sababu za kufungua uchumi mkubwa wa kidijitali nchini

Muktasari:

  • Kama ikikuzwa na kutumiwa vizuri, miundombinu ya kidijitali nchini inatoa fursa ya kushika nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Kama ikikuzwa na kutumiwa vizuri, miundombinu ya kidijitali nchini inatoa fursa ya kushika nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Wataalamu wa teknolojia wanasema kufungua uwezo huo na kutumia kimaendeleo taarifa za kitaifa kunatakiwa kushughulikiwa haraka ili kuutumia uwezo huo kwa maendeleo.

Taarifa ni muhimu sana katika kuendeleza uchumi wa kidijitali, la sivyo matokeo yanayotakiwa hayataweza kufikiwa ipasavyo.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, taarifa za ndani ni muhimu sana katika uchumi wa kidijitali kusaidia ukuaji, kuongeza tija na kutengeneza ajira.

Wakati duniani uchumi mpya unaoendeshwa na taarifa umekuwa ukikua katika miaka ya hivi karibuni, hali haijawa nzuri Tanzania. Shirika la Biashara Duniani (UNCTAD) linakadiria kuwa matumizi ya intaneti duniani yataongezeka kutoka GB 45,000 kwa sekunde mwaka 2017 hadi GB 150,700 mwaka 2022.

“Idadi ya taarifa nchini Tanzania imekuwa ikikua, lakini si kwa kasi ya kutosha (kufikia ya dunia),” linasema shirika hilo la kutoa mikopo duniani katika toleo lake la 14 kuhusu uchumi wa Tanzania inayoitwa Tanzania Economic Update (TEU).

Shirika hilo linasema ili uchumi wa kidijitali nchini uwe na matokeo mazuri, hatua kadhaa zinazotakiwa kuchukuliwa kwa wakati mwafaka, haziepukiki, ikiwa ni pamoja na nchi kuachana na vikwazo vya kisheria na kisiasa ambavyo vinazuia uwekezaji.

“Kwa mfano, Airtel ilisimamisha kwa muda uwekezaji kusubiri kutatuliwa kwa mzozo wake na Serikali kuhusu umiliki wa kampuni yake tanzu nchini Tanzania. Mzozo huo ulitatuliwa Januari 2019, huku hisa za Airtel zikipunguzwa kutoka asilimia 60 hadi 51 na za Serikali zikiongezeka kutoka asilimia 40 hadi 49,” inasema Benki ya Dunia.

“Baada ya mzozo kwisha, Airtel ikaanza kuweka mtandao wa 4G, lakini inasemekana makubaliano hayo yalipunguza ushindani, kwa sababu Serikali pia ina hisa katika kampuni ya simu ya TTCL, ambayo ni mshindani wa Airtel,” inasema Benki Kuu.

Tanzania pia haina budi kuandaa mchakato wa sheria za kidijitali kwa ajili ya kusaidia biashara ya kidijitali, kutengeneza mazingira ya kusaidia kukua kwa matumizi huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi na malipo mengine ya kidijitali, ikiwa ni pamoja na miamala ya thamani ndogo na nafuu.

Katika tathmini yake ya hivi karibuni kuhusu uchumi wa kidijitali nchini, taasisi hiyo imeonyesha maendeleo kadhaa katika matumizi ya teknolojia mpya katika shughuli za uzalishaji kama minada ya mtandaoni na kutambua ushahidi wa kielektroniki.

Benki hiyo pia imesifu huduma za Serikali mtandao (e-government) na uwepo wa kanuni kutaarifu makosa kwa kutuma na kupokea ujumbe. Mambo mengine mazuri kuhusu masuala ya kidijitali na taarifa ni nchi kuunganishwa katika mikongo mitatu ya kimataifa inayopita chini ya bahari na uwekezaji wa Halotel wa kuweka mikongo maeneo ya vijijini.

“Katika suala la uunganishaji nchini Tanzania ya saizi kubwa (GB10 na zaidi) ni miongoni mwa zilizo na gharama nafuu Afrika Mashariki,” inasema Taasisi ya Kimataifa ya Fedha (IFI) katika taarifa ya tathmini yake inayoitwa The Potential of the Digital Economy.

Tathmini ya mwaka 2020 imeangazia masuala mengine kadhaa kuhusu uunganishaji, malipo na utambulisho ambayo yanatakiwa kushughulikiwa haraka kuwezesha uchumi wa kidijitali kuchukua nafasi yake katika ujenzi wa Taifa.

Miongoni mwa masuala makubwa ni kupunguza bei ya matumizi ya vifurushi vya GB5 na chini yake ambayo kwa sasa inakwaza utumiaji.

“Tanzania si soko nafuu tena Afrika Mashariki. Kwa ujumla bei za MB100, MB500, na GB1 ni ghali kuliko nchi nyingine. Kwa mfano bei ya MB100 ni mara tatu zaidi ya Uganda na Kenya,” inasema ripoti hiyo.

“Kwa kulinganisha, ripoti hiyo inaongeza kuwa bidhaa zinazotumiwa sana (zaidi ya 10 GB) zina ushindani mkubwa, licha ya kwamba bei bado si ya chini. Wakati hilo linaweza kuwa zuri kibiashara, bei ni kubwa sana kwa mtumiaji wa kawaida. Vivyo hivyo, kodi kubwa zinafawafanya maskini wasiweze kumudu huduma hizo,” inaeleza IFI.

Benki ya Dunia inaonya kuwa taarifa zisizo sahihi kuhusu kusambaa kwa mtandao kunaathiri mipango na kusisitiza kuwa kunapokuwa na udhaifu katika kuchukua hatua kisheria, kunaathiri mwamko wa kidijitali na matumizi yake.

Inasema udhaifu huo unaonyesha umuhimu wa kufanya tathmini kubwa ya uamuzi wa kisheria na kuwa na mkakati wa pamoja wa sheria (katika hili ni usajili wa laini za simu na utoaji wa vitambulisho vya Taifa) kama kuna nia ya kukuza uchumi wa kidijitali.

Kuhusu njia za malipo, tathmini inaonyesha matumizi ya simu kupata huduma za fedha bado yapo chini, japokuwa ndio njia pekee ya uhakika ya kufikisha huduma hizo kidijitali kwa wananchi, kwani ndio nafuu zaidi.

Licha ya ukweli kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoendelea zaidi katika matumizi ya huduma za fedha kupitia simu ya mkononi duniani, yenye historia ya kuruhusu mwingiliano wa laini katika kuwasiliana, hoja ya Benki ya Dunia bado ina mashiko.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mifumo ya Taifa ya malipo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bernard Dadi, fedha za simu za mkononi zimekuwa zaidi ya mara 300,000 kati ya mwaka 2008 wakati zilipoanzishwa nchini na mwaka jana.

Huduma hizo kwa sasa ni moja ya biashara zenye fedha nyingi katika uchumi ambazo zimesaidia kubadilisha kila nyanja ya maisha na kwa kiasi kikubwa kuchangia kuongezeka kwa ujumuisha wa kifedha nchini.

“Idadi ya miamala kwa njia ya mtandao imefikia milioni 20, kutoka 174,315 wakati huduma ilipoanza Oktoba 2014,” alinukuliwa Dadi alimwambia mwandishi wa makala hii Julai mwaka jana.

“Matumizi ya fedha za simu za mkononi yamekua kiajabu. Idadi ya sasa ya miamala ya kila mwezi ni wastani ni kati ya Sh231.3 milioni ikiwa na thamani ya jumla ya Sh8.43 trilioni kulinganisha na miamala 601 iliyokuwa na thamani ya Sh25.3 milioni mwaka 2008,” aliongeza.

Taasisi ya Kukuza Huduma za |Fedha Tanzania (FSDT), ambayo inasaidia ubunifu na masoko katika sekta ya fedha ili kuendeleza ajenda ya ujumuishwaji wa kifedha kitaifa, inasema hatua ya Tanzania kuanza kutumia mapema matumizi ya fedha za simu imekuwa na matokeo mazuri.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, Tanzania ilikuwa na theluthi moja ya akaunti za fedha kwenye simu katika Afrika Mashariki mwaka 2015, huku watu na mashirika yakifanya miamala inayofika zaidi ya asilimia 50 ya pato la Taifa (GDP) kila mwezi.

Wataalamu wanasema baada ya kutatua kwa mafanikio tatizo la upatikanaji, changamoto kubwa inayofuata ni haja ya ujumuishaji wa kidijitali na huduma jumuishi za kifedha, ni kupunguza tofauti kati ya kufikia huduma hizo na matumizi yake.

“Ingawa zaidi ya asilimia 90 ya watu wazima Tanzania wanaweza kufanya malipo ya kidijitali, ni watu sita tu kati ya 10 wanaoweza kufanya matumizi ya maana ya mitandao ya kidijitali,” gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu ameandika katika chapisho lake linaloitwa Financial Innovation and Financial Inclusion in Tanzania - The Role of Banks (Ubunifu na Ujumuishaji Kifedha Tanzania—Jukumu la Benki).

Tanzania bado haina sheria zinazosaidia kukua kwa uchumi wa kidijitali kama vile ya kulinda taarifa au kuhusu siri za wateja. Tatizo la kisheria ni kikwazo katika kujenga uaminifu unaohitajika kusisimua biashara ya kidijitali.

Kwa Benki ya Dunia, majukwaa ya kidijitali yanaweza kufanikiwa kama yatajenga hali ya kuaminiwa na watumiaji.

Tanzania inahitaji Sheria ya Kulinda Uhuru wa Watumiaji na inatakiwa kuanzisha kitengo cha makosa ya kimtandao katika Jeshi la Polisi.

Makala hii imeandikwa na Costantine Muganyizi