Uchumi wa Tanzania kukua kuliko wa Kenya, Uganda
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti ya Tathmini ya Ustawi wa Kiuchumi(MEO), uchumi wa Rwanda ndiyo utakua kwa kiwango cha juu zaidi mwaka huu Afrika Mashariki, kwa asilimia 7.2
Dar es Salaam. Uchumi wa Tanzania umetabiriwa kukua kuliko ukilinganisha na Kenya na Uganda mwaka huu 2024.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Jumatano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 6.1, kiwango ambacho ni cha juu, ikilinganishwa na mataifa mengine katika ukanda wa Afrika Mashariki, isipokuwa Rwanda.
Kwa mujibu wa ripoti ya Tathmini ya Ustawi wa Kiuchumi(MEO), uchumi wa Rwanda ndiyo utakua kwa kiwango cha juu zaidi mwaka huu Afrika Mashariki, kwa asilimia 7.2
Tanzania pia, imeorodheshwa namba tisa miongoni mwa mataifa 11 bora ambayo uchumi wake utakua kwa kiwango cha juu zaidi mwaka huu barani Afrika.
Mataifa hayo ni Niger utakua kwa asilimia 11.2, Senegal (asilimia 8.2), Libya (asilimia 7.9), Rwanda (asilimia 7.2), Cote d’ Ivoire (asilimia 6.8), Ethiopia (asilimia 6.7), Benin (asilimia 6.4 na Djibouti (asilimia 6.2).
Mataifa yanayofuata ni Togo na Uganda, yaliyotarajiwa uchumi wake kukua kwa kiwango cha asilimia sita kila moja.
Kwa mujibu wa mkuu wa benki hiyo, Dk Akinwumi Adesina, kiwango cha ukuaji wa wastani barani Afrika kitakua asilimia 3.8.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kiuchumi, tathimini hiyo ya inaakisi mipango ya Serikali za kila nchi, ambazo zimekuwa zikielezea kuhusu mikakati iliyoweka katika kuboresha uchumi wa nchi.
Pia, matumaini ya gharama ya maisha kupungua, kuanza kuimarika dhidi ya sarafu za kigeni,
Wachambuzi wanadokeza tathmini hiyo inaonyesha nafasi ya kila nchi katika kuimarisha uchumi hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Kwa muda mrefu, Kenya imekuwa ikitajwa kama Taifa lenye uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki. Hata hivyo, hali inaonekana kubadilika, kwani mataifa kama vile Tanzania, yameanza kuamka kiuchumi,” amesema mchambuzi wa masuala ya kiuchumi wa Kenya, Tony Watima.
Imeandaliwa kwa msaada wa Taifa Leo.