Utajiri wa watu wa Dar waongezeka

Dar es Salaam. Takwimu mpya za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesa ongezeko la asilimia 5 katika wastani wa kipato cha Mtanzania kwa mwaka ikichangiwa na kukua kwa uchumi wa kanda ya Dar es Salaam, kanda ya ziwa na kanda ya kaskazini.

Katika ripoti ya BoT ya ufanisi wa uchumi katika kila kanda iliyotolewa Oktoba 5 mwaka huu inaonyesha kuwa wastani wa kipato cha Mtanzania (GDP per Capita) mmoja mmoja kimeongezeka kutoa wastani wa Sh2.70 milioni hadi Sh2.84 milioni.

Wastani wa kipato cha wakazi wa Dar es Salaam kimeongezeka zaidi kuliko maeneo mengine ya nchi kutoka Sh4.81 milioni hadi Sh5.39 milioni mwaka 2022 sawa na ukuaji wa asilimia 12, hivyo ikinganishwa na mwaka uliopita kila mkazi wa Dar es Salaam aliongeza Sh500, 000 katika mapato yake ya mwaka.

“Hicho kiasi wanachokisema mbona mimi sina wala sijawahi kufunga mwaka hata nikiwa na nusu yake, hata wanaposema ongezeko hilo mimi kwangu hakuna kilichoongezeka zaidi ya gharama za maisha,” alisema Salum Mohammed ambaye ni muuza machungwa wa Tabata jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo hesabu ya pato la mtu mmoja mmoja inapatikana kwa kugawa pato la Taifa au eneo fulani (GDP) kwa idadi ya watu waishio humo. Na kwa mujibu wa Shirika la fedha dunia (IMF) GDP hupimwa kwa kuangalia thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa katika kipindi husika na si zote zinazojumuishwa.

Miongoni mwa shughuli ambazo hazijumuishwi katika ukokotozi ni zile ambazo mtu halipwi (yaani za kujitolea) pamoja na biashara haramu na zisizo rasmi kwakuwa ni vigumu kupima thamani yake.

Aidha ukiachilia mbali Dar es Salaam kanda inaofuatia kwa wananchi wake kuwa na kipato kikubwa ni Kaskazini ambako takwimu za BoT zinaonyesha kuwa wastani wa kipato kwa mwaka ni Sh3.38 milioni kikiongezeka kwa asilimia 8.4 ikilinganishwa na mwaka 2021.

Kanda inayofuatiwa kwa wananchi wake kuwa na kipato kikubwa ni Nyanda za juu kusini ambako wastani wa kipato cha wananchi huko ni Sh3.10 milioni kwa mwaka ikifuatiwa na kanda ya kusini Mashariki ambayo kipato cha watu wake ni Sh2.7.

Kanda ya ziwa yenyewe imerekodi ukuaji mkubwa wa uchumi kwa kipindi cha mwaka 2022 kwa wastani wa kipato cha wananchi wake kiliongezeka kwa asilimia 10.6 hadi kufikia Sh2.27 milioni kikiongezeka kutoka Sh2.05 milioni mwaka 2021.

Ripoti hiyo inaonyesha licha ya kuwepo kwa ukuaji wa jumla kanda mbili kati ya sita za nchi zilishuhudia ukuaji hasi wa pato la watu wake, Kanda ya kusini mashariki kipato cha watu wake kilipungua kwa asilimia 6.5 huku kanda ya kati kikipungua kwa asilimia 2.7.

“Kanda zote zilishuhudia ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja isipokuwa kanda ya kati na kanda ya kusini mashariki. Hali hiyo kwa kiasi kikubwa inatokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu katika maeneo hayo. Dar es Salaam, Kaskazini na nyanda za juu kusini walikuwa na kipato kilichovuka viwango vya kitaifa,” imeeleza ripoti hiyo.

Kuhusu mwenendo huo Mhadhiri wa Idara ya Uchumi kutoka Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Dk Lutengano Mwinuka amesema ukuaji chanya na hasi wa uchumi wa ukanda husika unatokana na aina ya shughuli zao za kiuchumi wanazozifanya.

“Kanda ambazo zimekuwa na ukuaji mdogo au hasi wa pato lake maana yake shughuli zake za uchumi zimedorora au zimekuwa na ukuaji mdogo ikilinganisha na ongezeko la watu,” alisema Dk Lutengano.

Alisema ili kuongeza ukuaji wa uchumi katika kanda zenye kasi ndogo ni muhimu kuwa na matumizi mazuri ya ardhi na kuwekeza zaidi katika viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa na mazao yanayozalishwa katika maeneo hayo.

“Bado kuna fusa kubwa ya kukuza uchumi wa kanda nan chi kwa ujumla kwa kutumia fursa ya rasilimali za asili tu tulizonazo kama ardhi, hata suala la ongezeko la watu linapaswa kuchukuliwa kama fursa kwani matumizi mazuri ya rasilimali watu huongeza tija katika uchumi,” alisema Dk Lutengano.


Mchango wa kanda katika pato la Taifa

Kwa upande wa mchango wa kanda katika pato la Taifa Kanda ya ziwa inachangia zaidi ya robo ya pato lote la nchini (asilimia 25.9 sawa na Sh44.18 trilioni) ikifuatiwa na kanda ya Kaskazini asilimia 17.2 (Sh29.29trilioni) kisha kanda ya Dar es Salaam asilimia 17.1 (Sh29.02trilioni).

Kanda ya nyanda za juu kusini inachangia asilimia 15.8 (Sh26.92 trilioni) ya pato lote la Taifa , kanda ya kati inachangia asilimia 13.5  (Sh22.92trilioni) huku kanda ya kusini mashariki ikiwa na mchango mdogo zaidi wa asilimia 10.5 (Sh17.89trilioni).

Ripoti hiyo kwa ujumla ilionyesha ukuaji wa Pato la Taifa ambalo lilitajwa kuwa Sh170.25 trilioni likiongezeka kutoka Sh156.37 trilioni, ongezeko likitajwa kuchangiwa zaidi na sekta ya kilimo, ujenzi, madini, viwanda na biashara.

Aidha katika mwaka huu Serikali inakadiria kuwa GDP itakuwa kwa asilimia 5.2 kutoka asilimia 4.7 ya mwaka 2022 mbali na vipaumbele vikuu vya Serikali, Waziri wa fedha Dk Mwigulu Nchemba alitaja maeneo mengine ambayo yatakuza kipato cha wananchi na kuongeza pato la taifa.

“Serikali itaendelea na uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji na ujenzi wa mabwawa makubwa 100. Miradi hiyo inatarajiwa kuwa na matokeo makubwa na ya haraka katika uchumi, ikiwemo kuzalisha ajira na kuongeza kipato,” amesema Dk Mwigulu.

Aidha Mchumi huyo mwenye dhamana ya fedha nchini alisema kuna mabadiliko makubwa yatafanyika mwaka huu katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi ili kuziwezesha sekta hizi ziweze kuchangia kwa kasi jitihada za kupunguza umaskini kwa watanzania na kukuza Pato la Taifa.