Uchumi wa Tanzania wapaa miaka miwili ya Rais Samia - IMF

Muktasari:

  • Pato la Taifa lafikia Sh200 trilioni kwa mwaka 2023 kutoka Sh163 trilioni ya mwaka 2021.
  • Uchumi wa Tanzania sasa ni mkubwa kuliko baadhi ya nchi za Ulaya na ni wa sita kwa ukubwa kwa nchi zote za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Dar es Salaam. Takwimu mpya za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zinaonesha kuwa pato la Taifa la Tanzania kwa bei ya sasa limeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 85.42 (Shilingi200 trilioni) kwa mwaka huu wa 2023, ikiwa ni ishara kuwa sera za uchumi za Rais Samia Suluhu Hassan zinaleta mageuzi makubwa nchini.

Ongezeko hilo la Pato la Taifa ni kutoka Dola za Marekani Bilioni 69.9 (Shilingi163.5 trilioni) kwa mwaka 2021, wakati ambapo Rais Samia alipoingia madarakani.

Takwimu hizo za IMF zinaonesha kuwa Pato la Taifa la Tanzania huenda likaongezeka zaidi hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 136.09 (Sh276 trilioni) ifikapo mwaka 2028.

Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia ametekeleza sera rafiki kwa sekta binafsi, ambayo imeongeza kasi ya uwekezaji, biashara na ukuaji wa uchumi nchini.

Kwa mujibu wa takwimu hizo mpya za IMF, pato la Taifa la Tanzania kwa mwaka 2023 ni kubwa kuliko nchi kadhaa ndogo za Ulaya, ikiwemo Croatia (Dola 78.8 bilioni), Lithuania (Dola 78.3 bilioni), Serbia (Dola 73.9 bilioni) and Slovenia (Dola 68.1 bilioni).

Kwa upande wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ni nchi ya sita kwa ukubwa wa Pato la Taifa.


Kwa mujibu wa takwimu za IMF, nchi 10 zinazoongoza kwa ukubwa wa Pato la Taifa Kusini mwa Jangwa la Sahara ni hizi zifuatazo;

1. Nigeria Dola 506.6 bilioni

2. South Africa Dola 399 bilioni

3. Ethiopia Dola 156 bilioni

4. Kenya Dola 118.1 bilioni

5. Angola Dola 117.8 bilioni

6. Tanzania Dola 85.4 bilioni

7. Còte d'Ivore Dola 77 bilioni

8. DRC Dola 69.4 bilioni

9. Ghana Dola 66.6 bilioni

10. Uganda Dola 49.7 bilioni.