Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NMB yaibuka kinara Afrika Mashariki huduma kwa wafanyabiashara wadogo

Muktasari:

  • Benki ya NMB imetwaa Tuzo ya Euromoney 2026 kama Benki Bora kwa Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati, ikitambuliwa kwa huduma bunifu za kifedha zinazochochea ukuaji wa biashara na uchumi wa Tanzania.

Dar es Salaam. Wakati wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) wakitajwa kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa kuchochea uzalishaji, kuongeza ajira na kuimarisha sekta binafsi, Benki ya NMB Plc imetwaa Tuzo ya Euromoney 2026 kama Benki Bora inayowapatia huduma.

Tuzo hiyo imetambua mchango wake katika kuwawezesha wafanyabiashara hao kupitia huduma za kifedha, mitaji na suluhisho za kidijitali zinazowawezesha kukuza biashara zao.

Tuzo hiyo ilitangazwa kupitia Jarida la Euromoney kuchapisha orodha ya washindi wa Tuzo za Ubora 2026 zinazotolewa kila mwaka kwa taasisi za fedha zilizoonyesha utendaji bora, ubunifu katika utoaji wa huduma na matokeo chanya kwa wateja katika masoko mbalimbali duniani.

Washindi walitunukiwa Julai 16, 2026 katika hafla iliyofanyika Peninsula Hotel, London, Uingereza.

Akizungumzia ushindi huo, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alisema tuzo hiyo ni matokeo ya dhamira ya muda mrefu ya benki hiyo ya kuwezesha biashara zinazochochea ukuaji wa sekta binafsi na uchumi wa taifa.

Alisema mafanikio hayo hayaishii kwa NMB pekee bali ni utambuzi wa juhudi zinazofanywa kila siku na maelfu ya wafanyabiashara wadogo na wa kati wanaojenga biashara zao, kuajiri Watanzania, kufanya biashara na kuendelea kuleta ubunifu katika uchumi wa nchi.

“Tuzo hii ni ya wajasiriamali na wafanyabiashara wanaoendelea kujenga, kuajiri, kufanya biashara na kuleta ubunifu nchini,”

“Wafanyabiashara wadogo na wa kati ni injini muhimu ya ukuaji jumuishi na jukumu letu ni kuwapatia ufadhili wa uhakika, mifumo salama ya malipo, ushauri wa kibiashara na zana za kidijitali zinazowawezesha kukua kwa kujiamini,” alisema Zaipuna.

Alisema uwezeshaji wa wafanyabiashara wadogo na wa kati umeendelea kuwa moja ya maeneo muhimu katika Agenda 2030 ya NMB mpango wa muda wa kati wa benki hiyo wa mwaka 2026 hadi 2030 unaolenga kujenga mfumo jumuishi wa huduma za kibenki kwa wafanyabiashara, kuboresha huduma kwa wateja, kupanua suluhisho katika minyororo ya thamani na kuendeleza maeneo mapya ya biashara.

Zaipuna alisema mkakati huo umejengwa kwa kuzingatia mabadiliko ya mazingira ya biashara na mahitaji ya wafanyabiashara wanaotafuta mitaji, teknolojia na huduma za kifedha zinazowawezesha kushindana katika soko la ndani na la kimataifa.

Agenda hiyo pia inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga sekta binafsi yenye ushindani, jumuishi na yenye uwezo wa kuchochea ubunifu, uwekezaji na ukuaji endelevu wa uchumi.

“Dira hii pia inaitambua sekta ya wafanyabiashara wadogo na wa kati kuwa muhimu katika urasimishaji wa biashara, ujenzi wa kampuni za Kitanzania zenye ushindani wa kimataifa na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa,” alisema.

Ushindi huo unakuja wakati Benki ya NMB ikiendelea kuimarisha nafasi yake katika sekta ya fedha nchini, huku thamani yake ya soko ikifikia takribani Sh8.1 trilioni sawa na karibu dola bilioni 3 za Marekani.

Benki hiyo kwa sasa inatoa huduma kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati katika mikoa yote 31 ya Tanzania kupitia huduma mbalimbali zikiwemo mikopo ya biashara, huduma za malipo ya kidijitali, miamala ya kifedha, ushauri wa biashara pamoja na bidhaa zinazolenga kukidhi mahitaji halisi ya wafanyabiashara kulingana na hatua ya ukuaji wa biashara zao.

NMB pia inashikilia zaidi ya asilimia 20 ya soko la huduma za kibenki kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini, jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika kuhudumia kundi hilo.