Nyama ya ng’ombe yapanda bei Moshi

Monday April 05 2021
nyama pc
By Florah Temba

Moshi. Bei ya nyama ya ng’ombe imepanda kutoka Sh7,000 kwa kilo moja hadi Sh8,000 mjini hapa kutokana na gharama za mfugo huo kuwa juu mnadani.

Wakizungumza juzi baadhi ya wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali walisema bei ya nyama ilianza kupanda kuanzia Machi 21 baada ya ng’ombe kupanda bei katika minada.

Mfanyabiashara wa nyama, Thomas Aloyce alisema katika Soko Kuu la Kati mjini Moshi, ng’ombe walikuwa wakiuzwa kwa Sh800,000 mnadani, lakini kwa sasa wananunua kwa Sh1 milioni hadi Sh1.2 milioni, jambo linalowalazimu kupandisha bei ya nyama.

“Nyama imepanda bei na sasa tunauza Sh8,000 kwa kilo, lakini kwa stake (mnofu) tunauza kwa Sh9,000 kwa kilo, bei hizi sio mpya kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka, bei hii ilianza kupanda Machi 21, lakini inaonekana watu wengi hawajanunua nyama hivi karibuni ndiyo maana wanaona kama mpya,” alisema Thomas.

Mfanyabiashara eneo la Pasua, Raphael John alisema biashara hiyo imekuwa ngumu na hawana matumaini ya kupata wateja wengi katika kipindi hiki cha sikukuu, kama ilivyokuwa ikitegemewa miaka ya nyuma.

“Ni kweli bei ya nyama imepanda na kufikia Sh8,000, tofauti na awali iliuzwa Sh7,000, hii ni kwamba na sisi tunauziwa ng’ombe ghali sana, lakini pia biashara imekuwa ngumu, watu wamepunguza kula nyama, siyo kama miaka ya nyuma,” alisema John.

Advertisement

Baadhi ya wakazi wa mjini Moshi walisema bei hiyo ni kubwa ikilinganishwa na vipato vya watu wengi, hali inayosababisha wapunguze matumizi ya nyama na kubaki kwenye mboga za majani.

“Bei ya Sh8,000 kwa kilo ni kubwa, mimi mwenyewe siwezi kununua, nilizoea kununua nyama nusu kwa Sh3,000 hadi Sh3,500,” alisema Raphia Mohamed.

Advertisement