Profesa Kitila: Uchumi wa Dola 1 trilioni hauwezekani bila sekta binafsi
Makamu wa Rais wa Uendelevu na Ushirikishwaji wa Wadau wa Geita Gold Mining Limited (GGML), Simon Shayo ambaye pia Mwenyekiti wa Bodi ya Global Compact Network Tanzania (GCNT), akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo (katikati), pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa GCNT, Marsha Macatta-Yambi, wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za Business SDG Awards 2026 iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- GGML yaunga mkono Tuzo za Business SDG Awards, yataka ushirikiano kuimarishwa
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Tanzania haiwezi kufikia lengo la kuwa na uchumi wa Dola1 trilioni za Marekani ifikapo mwaka 2050 bila sekta binafsi kuwa mstari wa mbele katika uwekezaji, uzalishaji na uundaji wa ajira.
Profesa Mkumbo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Business SDG Awards 2026 iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, huku Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ikiwa miongoni mwa wadhamini wakuu wa hafla hiyo kupitia udhamini wa ngazi ya Dhahabu (Gold Sponsor).
Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 itakayoanza kutumika Julai mosi, 2026 imeweka sekta binafsi katika nafasi ya kipekee kutokana na mchango wake katika kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira.
"Kila tunachofanya lazima tujiulize tunazalisha ajira ngapi. Hili ni jambo la msingi sana," amesema Profesa Mkumbo akiongeza kuwa tangu kuanza kwa maandalizi ya Dira ya Maendeleo 2050, wadau wa sekta binafsi walishiriki kutoa maoni yaliyochangia kuweka lengo la Tanzania kuwa na uchumi wa Dola1 trilioni za Marekani.
"Namna dira ilivyoandaliwa, sekta binafsi ndiyo ipo katikati. Lengo la kuwa na uchumi wa Dola 1 trilioni lilitokana kwa kiasi kikubwa na mchango wa viongozi wa sekta binafsi," amesema.
Tuzo hizo zilizoandaliwa na Global Compact Network Tanzania (GCNT), zilifanyika kwa mwaka wa nne mfululizo zikiwa na lengo la kutambua kampuni zinazotekeleza kwa vitendo Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), huku zikikusanya pamoja viongozi wa Serikali, sekta binafsi, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wa maendeleo.
GGML iliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Uendelevu na Ushirikishwaji wa Wadau, Simon Shayo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya GCNT Tanzania ambaye alisema wananchi yamekuwa msingi wa falsafa ya maendeleo ya Tanzania tangu enzi za uhuru, akisisitiza kuwa sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kufanikisha malengo hayo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza na Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za Business SDG Awards 2026 iliyofanyika jijini Dar es Salaam
"Maendeleo yanayomlenga mwananchi yamekuwa sehemu ya mjadala nchini tangu tupate uhuru. Hiyo ndiyo ilikuwa falsafa ya Mwalimu Julius Nyerere kuhusu mustakabali wa Taifa. Aliamini kuwa maendeleo yenye maana ni yale yanayowawezesha na kuwaondoa wananchi katika umaskini," amesema.
Mafanikio ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo.
Shayo pia amepongeza hatua za Serikali za kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), akisema zimeongeza imani ya wawekezaji na kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa GGML, udhamini wake katika Tuzo za Business SDG Awards unaakisi dhamira ya kampuni hiyo ya kuunga mkono shughuli za Global Compact Network Tanzania pamoja na juhudi za kufanikisha Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030.
Kwa zaidi ya miaka 25 ya shughuli zake katika Mkoa wa Geita, GGML imesema imeajiri zaidi ya watu 7,000, huku asilimia 98 ya wafanyakazi wake wakiwa Watanzania.
Kampuni hiyo pia imetoa zaidi ya Dola 3.7 bilioni za Marekani kama kodi kwa Serikali, sambamba na kuwekeza katika maendeleo ya jamii, uhifadhi wa mazingira na kukuza uchumi wa Taifa.