Puma kusukuma zaidi mageuzi ya uchumi Tanzania
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, anasema kampuni itaendelea kuunga mkono mabadiliko ya uchumi wa Tanzania kupitia uwekezaji endelevu katika miundombinu ya kimkakati ya nishati pamoja na suluhisho bunifu za nishati.
Fatma alisema hayo juzi katika hafla ya siku ya gawio ambapo mashirika ya umma na taasisi ambazo Serikali inamiliki hisa zilikuwa zikiwasilisha magawio yao, mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
"Katika miaka ya hivi karibuni, tumewekeza kwa kiwango kikubwa katika kupanua mtandao wetu wa vituo vya huduma, kuimarisha usambazaji wa mafuta ya ndege, kukuza biashara ya gesi ya LPG na kuanzisha matumizi ya nishati safi kama vile Gesi Asilia Iliyobanwa (CNG),” anasema Fatma.
Anasema uwekezaji huo unaweka msingi imara wa ukuaji wa baadaye, unaunga mkono ajenda ya nchi ya maendeleo ya viwanda na mabadiliko ya matumizi ya nishati, huku ukiendelea kuhakikisha tunatoa huduma za nishati za kuaminika zinazochangia maendeleo endelevu ya uchumi na ustawi wa Tanzania.
Kadhalika anasema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Puma Energy Tanzania imechangia zaidi ya Sh1.4trilioni kupitia kodi na tozo mbalimbali kwa Serikali ikiwamo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ikiwa na zaidi ya vituo 100 vya huduma za mafuta, kituo kikubwa cha kuhifadhi mafuta pamoja na maghala kadhaa yaliyopo maeneo mbalimbali nchini, Puma Energy Tanzania imejenga mtandao imara wa huduma kote Tanzania. Kampuni hiyo pia inasambaza mafuta ya ndege katika viwanja vya ndege vinane, ikiwamo viwanja vyote vya kimataifa nchini Tanzania, na inaendelea kuongoza mabadiliko ya matumizi ya nishati safi kupitia Kituo Kikuu cha CNG (CNG Mother Station) kikubwa zaidi barani Afrika pamoja na mtandao unaokua wa vituo vya CNG jijini Dar es Salaam na Morogoro.
Katika Siku ya Gawio Puma ilikabidhi Sh15 bilioni ambazo ni nusu ya faida iliyopatikana, ikiwa ni gawio kubwa zaidi kuwahi kutolewa katika historia ya kampuni hiyo inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 50.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Puma Energy Tanzania, Balozi George Madafa, alisema gawio hilo la kihistoria linaakisi uimara wa misingi ya biashara ya kampuni pamoja na mafanikio ya mkakati wake wa ukuaji wa muda mrefu.
"Makabidhiano ya gawio la leo yanaakisi utendaji mzuri wa Puma Energy Tanzania, uimara wake na dhamira ya kuendelea kuzalisha thamani endelevu kwa wanahisa wetu na taifa kwa ujumla,” alisema Balozi Madafa.
Anaongeza kuwa kampuni hiyo inajivunia kuhakikisha kuwa mafanikio yetu yanawanufaisha moja kwa moja Watanzania kupitia gawio kwa wanahisa, ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali, uwekezaji pamoja na uundaji wa fursa za ajira.