Rais Samia azindua meli kukuza uchumi wa bluu
Muktasari:
- Rais Samia ametoa maagizo sita kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, akitaka sekta hiyo kuongeza kasi ya mageuzi ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa buluu na kuongeza tija katika uvuvi nchini.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uzinduzi wa meli ya uvuvi ni hatua muhimu unaowekea msingi wa utekelezaji wa sera na mikakati katika kukuza mchango na tija ya sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu ikiwamo uchumi wa Taifa.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Aprili 25, 2026 alipokuwa akizindua meli ya kwanza ya uvuvi wa bahari kuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (Tafico), hafla iliyofanyika Chuo cha Mwalimu Nyerere, Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.
“Hatua hii inaakisi maono na mabadiliko ya kimkakati katika udhibiti na usimamizi wa rasilimali za bahari kuu.
“Kwa dhati kabisa tumedhamiria kulifufua na kuliimarisha shirika letu la uvuvi ili liweze kushiriki ipasavyo katika kusimamia rasilimali za bahari kuu,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa kwa muda mrefu uvunaji wa rasilimali za bahari kuu umekuwa unafanywa na meli na makampuni kutoka nje ya nchi hali iliyozorotesha uwezo wa nchi kunufaika na rasilimali hizo kimapato na ustawi wa wananchi kwa ujumla.
“Kwa msingi huo kuliwezesha shirika letu la uvuvi kwa vifaa na teknolojia za kisasa ni muhimu na ni jambo la lazima na tunaendelea kufanya hivyo kwa lengo la kuiwezesha nchi na wananchi kwa ujumla kunufaika na fursa zitokanazo na rasilimali za uvuvi wa bahari kuu,”amesema Rais Samia.
Mwonekano wa meli ya kwanza ya uvuvi wa bahari kuu mara baada ya uzinduzi leo Aprili 25, 2026 katika makao makuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Amezitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na kukuza ajira kwa vijana wetu, kuongeza mapato ya serikali, kuboresha lishe na afya za watu wetu na kuimarisha mnyororo wa thamani na ugavi katika sekta nyingine a kiuchumi.
Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini, Yoichi Mikamia amesema uzinduzi wa meli iliyotengenezwa nchini kwake unaonesha namna taifa hilo na Tanzania walivyokuwa na uhusiano imara uliodumu kwa muda mrefu.
Amesema Japan imekuwa ikiimarisha sekta ya mifugo Tanzania tangu miaka ya 1980 kwa kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya masoko mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza (Kirumba) na Malindi Mjini Unguja.
"Najisikia faraja leo kushuhudia tukio la kihistoria, ninatarajia kuwa uwezo wa meli hii utaleta ufanisi wa operesheni ikiwemo upatikanaji wa samaki," amesema Balozi Mikami.
Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Dk Bashiru Ally amesema ujenzi wa uwekezaji wa bandari ya uvuvi ya Kilwa Masoko mkoani Lindi, umefikia asilimia 97 huku, uendeshaji wake akitarajiwa kupewa sekta binafsi.
Dk Bashiru amesema katika asilimia chache zilizobaki za ujenzi huo wa bandari ni ni kupima mitambo kabla haijazinduliwa rasmi.
Kuhusu uzinduzi wa meli, Dk Bashiru amesema ni dhamira ya Rais Samia ya kuifanya nchi inufaike na rasilimali za uvuvi wa bahari kuu.
Waziri huyo ameeleza kuwa hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uzalishaji katika ukanda wa bahari hususani bahari kuu, kuboresha upatikanaji wa samaki wa ubora wa juu kwa ajili ya soko la nje na hatimaye kuongeza mchango wa sekta katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Pia, Dk Bashiru amesema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwenye uvuvi wa asili na ukuzaji viumbe maji kupitia mradi wa kuendeleza usimamizi wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji wa bahari Tanzania.
“Mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 117 utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030 kwa ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Dunia
“Lengo ni pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi kwa kujenga miundombinu ya uvuvi ikiwemo masoko, mialo, viwanda vya kuchakata samaki na kuwezesha mafunzo na tafiti,”amesema Waziri Bashiru.