Rais wa Msumbiji kushiriki ufunguzi maonyesho ya Sabasaba
Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo.
Muktasari:
- Washiriki 3,722 kutoka mataifa 23 wajitokeza, Serikali yaeleza imani kwa uchumi wa Tanzania yazidi kuongezeka.
Dar es Salaam. Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo anatarajiwa kuwa mgeni maalumu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi rasmi wa Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DiTF) unaotarajiwa kufanyika Julai 3, 2026.
Maonyesho hayo yanayofanyika kwa siku 16 kuanzia Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu, yanaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake huku yakiendelea kujijengea nafasi kama jukwaa la biashara, uwekezaji, viwanda na diplomasia ya uchumi nchini.
Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua maandalizi ya mabanda ya maonyesho kabla ya ufunguzi rasmi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema maonyesho ya mwaka huu yameweka rekodi ya ushiriki wa waoneshaji 3,722 kutoka nchi 23.
Amesema idadi hiyo inaakisi kuongezeka kwa imani ya wawekezaji na wafanyabiashara kwa uchumi wa Tanzania na mazingira yake ya biashara.
“Ushiriki huu mkubwa unaonyesha jinsi Tanzania inavyoendelea kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara,” amesema Kapinga.
Amesema maonyesho hayo yanakwenda kuzinduliwa wakati waonyeshaji wakileta bidhaa na huduma kutoka sekta mbalimbali zikiwamo viwanda, kilimo biashara, teknolojia, huduma na ubunifu huku msisitizo mkubwa ukiwa kwenye kuongeza thamani ya bidhaa na kukuza ujasiriamali.
Kapinga amesema pia programu za Serikali zinazowawezesha wanawake na vijana kiuchumi zimepewa nafasi kubwa katika maonyesho hayo, ambapo wanufaika mbalimbali wanaonyesha bidhaa walizozalisha baada ya kupata mafunzo, mitaji na huduma za maendeleo ya biashara.
“Sabasaba imeendelea kuwa zaidi ya soko la biashara, kwani sasa ni jukwaa la kubadilishana uzoefu, kujenga mitandao ya biashara na kuunganisha wadau katika minyororo ya thamani, hali inayofungua fursa mpya kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati,” amesema.
Kutokana na ongezeko la washiriki na wageni, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeboresha miundombinu katika viwanja vya maonyesho kwa kupanua maeneo ya maegesho, kuboresha barabara za ndani pamoja na huduma za maji na umeme.
Pia mamlaka hiyo imeanzisha mifumo ya kidijitali ya kurahisisha huduma, ikiwamo mfumo wa kuwaongoza wageni kutambua maeneo mbalimbali ndani ya viwanja kwa kutumia simu janja pamoja na programu ya TanTrade Biashara App, inayowezesha ununuzi wa tiketi mtandaoni na kutoa taarifa kuhusu waoneshaji na ratiba ya shughuli mbalimbali.
“Tunaendelea kuboresha huduma ili kuhakikisha washiriki na wageni wanapata mazingira bora, huduma zenye ufanisi na uzoefu mzuri wanapotembelea maonyesho haya,” amesema.
Katika maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu, TanTrade pia itaandaa hafla maalumu Julai 6, 2026 ya utoaji wa tuzo kwa ajili ya kutambua watu binafsi na taasisi zilizotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita.
Hafla hiyo ya Golden Jubilee Night itafunguliwa na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi.