Riba bado janga kwa biashara

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Soko la Kimataifa la Kariakoo wameshinikiza taasisi za kifedha nchini kupunguza riba za mikopo ya kibiashara kwa ajili ya kupanua mitaji yao pamoja na kutumia fursa za upangishaji na ununuzi wa maduka katika Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC).

Tayari Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Cathy Wang jana aliahidi kuchangia asilimia tatu ya riba kwa mfanyabiashara yeyote atakayenunua au kukodisha duka katika kituo hicho, huku taasisi nne za kifedha zikidai kuandaa muundo maalumu utakaokuwa na riba tofauti katika soko hilo.

Mradi huo wenye thamani ya dola milioni 110 (Sh275 bilioni), utakuwa na maduka 2,060 na tayari nusu ya maduka hayo yameshapata wanunuzi na wapangaji kabla ya kufunguliwa Juni, mwaka ujao.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki mkutano wa kutangaza fursa za soko hilo jana walisema umiliki wa maduka hayo utawasaidia kupunguza changamoto za usalama wa mizigo yao wanayoagiza China, kuepuka athari za kubadilisha Dola ya Marekani na gharama za madalali.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana alisema riba zinazotolewa na taasisi za kifedha hapa nchini ni kubwa ikilinganishwa na benki za mataifa mengine, ikiwamo China.

“Benki zetu zinakata riba kubwa mno, kwa hiyo tunaomba mpunguze, inaumiza sana wafanyabiashara wanaotamani kuwekeza katika soko hilo,” alisema Mbwana anayewakilisha wafanyabiashara zaidi ya 3,000 wa soko hilo.

Malalamiko hayo yanaibuka wakati Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiwa imeshusha riba ya kuzikopesha benki za biashara nchini (discount rate) kutoka asilimia tisa awali hadi asilimia saba mwaka 2018.

Kwa mujibu wa taarifa ya hatua za kisera kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi na kupunguza viwango vya riba mwaka 2021, benki hizo zimeendelea kutoza wastani wa asilimia 17 ya viwango vya riba kwa mikopo ya biashara, licha ya ongezeko la ukwasi na hatua nyingine zilizochukuliwa.

Wakizungumza na gazeti hili, mwakilishi wa kitengo cha biashara kutoka NMB, Mashaga Changarawe alisema huchukua kati ya asilimia 14 hadi 18, huku mwakilishi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Jaha Khamis akidai kwa sasa kuendelea kuchukua pia asilimia 14.5 ya riba kwa miaka kumi.

Meneja wa tawi la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Judith Kihwele alisema pamoja kutoza asilimia 18 hadi 22, wafanyabiashara watakaohitaji mikopo ya kuingia kituo hicho wataandaliwa riba maalumu.

Kwa mujibu wa EACLCL, kituo hicho kitaokoa Dola 4bilioni za Kimarekani zinazotumik kuagiza mizigo kila mwaka China baada ya wazalishaji wa bidhaa wanazofuata huko China kufungua maghala nchini ili kurahisisha huduma katika kituo hicho kitakachohudumia karibu watu milioni 500 wa ukanda huo.

Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Manispaa ya Ubungo, Mary Mwakyosi alisema tayari manispaa hiyo imeshaanza kunufaika kupitia mapato na ajira huku meneja masoko wa kituo hicho, Yang Zhen akiahidi ziara ya miji minne ya China kwa watakaolipia hadi Desemba mwaka huu.

Mfanyabiashara mwenye uzoefu katika uagizaji wa mizigo China, Peter Benda alisema ofa hizo zitaongeza unafuu kwani amekuwa akitumia wastani wa Sh5milioni katika safari ya kufuata mizigo