Serikali yatoa mbinu ya kuepuka mikopo umiza

Kamishna wa idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha katika Wizara ya Fedha Dk Charles Mwamaja.

Muktasari:

  • Wakati baadhi ya watu wakiumizwa na mikopo, Wizara ya Fedha imetaja miongoni mwa mambo ambayo yatakufanya kutambua haki zako kabla ya kuhudumiwa katika sekta ya fedha.

Dodoma. Wizara ya Fedha imesema ni haki ya mteja kufahamu masharti ya huduma ya kifedha kabla ya kuhudumiwa ili kuepuka kuingia katika mikopo umiza.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Novemba 15, 2023 na Kamishna wa Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha Dk Charles Mwamaja alipokuwa akizungumzia wiki ya huduma za fedha.

Amesema katika wiki hiyo itakayofanyika jijini Arusha kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid kuanzia Novemba 20 hadi 26, mwaka 2023, watatoa elimu juu huduma ya fedha.

“Tutawajengea uwezo wananchi kufahamu ni haki yao masharti ya mkopo kabla ya kukopa, wakati mwingine (changamoto) hutokea kutokana na mtu kutoelewa. Mtu anaambiwa fomu ya mkopo hii hapa akitaka kuuliza vipengele vya huko mbele anaambiwa huko acha saini hapa,” amesema.

Amesema huo sio utaratibu na kwamba wanataka wananchi waelewe kuwa mkopeshaji aliyeruhusiwa ni yupi, anatakiwa awe na nini na mambo gani ambayo unaweza kuyaona ukaanza kupata viashiria hatarishi kwamba huyu mkopeshaji si sahihi.

Amesema lakini kwa kutumia elimu hiyo ya huduma ya fedha, mteja ataweza kufahamu ni wapi atoe taarifa anapoona kuwa mahali pamepinda.

Aidha, Dk Mwamaja amesema takwimu zinaonyesha katika kila Sh10 ambayo iko katika mfumo takribani zaidi ya asilimia 60 haiko katika mfumo rasmi.

Amesema utafiti uliofanywa na FinScope wa mwaka 2023 nchini, ulibaini kuwa ni asilimia 53.8 tu ya nguvu kazi wanatumia huduma rasmi za fedha.

Amesema hali hiyo inafanya idadi kubwa ya Watanzania ambao hawafaidiki na huduma hizo na hivyo kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo zingewawezesha kuchangia katika kukuza pato la Taifa.

Naye Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha, Jonasia Mjema amesema ni muhimu watu kutotumia huduma ya fedha bila kupata elimu na anapoenda kwa mtoa huduma yoyote ahakikishe kuwa anapata uelewa.

“Ni nafasi pekee ya kufika katika maonyesho hayo ili kupata elimu ya fedha na hivyo mwananchi anapopata tatizo lolote kufahamu ni wapi aende kutoa taarifa,” amesema.