Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahitimu walilia mitaji, maeneo ya uwekezaji

Baadhi ya wahitimu wa kozi mbalimbali Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (FDC ) wakiwa kwenye sherehe za mahafali ya 51 yaliyofanyika chuoni hapo. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Wahitimu kozi mbalimbali kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) mkoani Pwani wamelilia mikopo, sanjari na kutengewa maeneo maalumu ya kufanyia shughuli za uzalishaji ili waweze kurejesha mikopo kwa urahisi.

Kibaha. Wahitimu wa kozi mbalimbali kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kibaha Mkoa wa Pwani, wameziomba halmashauri nchini kuwapa kipaumbele kwenye mikopo na hivyo kuwawezesha kufanyakazi kulingana na taaluma walizosomea.

 Wametoa ombi hilo wakati wa mahafali ya 51 ya chuo hicho yaliyohusisha jumla ya wahitimu 170 wa kozi mbalimbali, huku 51 wakishindwa kumaliza kozi hizo za miaka miwili kutokana na sababu mbalimbali.

“Tumepata ujuzi wa kufanya shughuli kulingana na taaluma tulizosoma hapa kwa miaka miwili ikiwemo kilimo, ufugaji, uselemara, ufundi magari na ubunifu wa mitindo ya ushonaji na tumesoma kwa kujibana kulingana na hali za uchumi,” amesema Pendo Ngobile mmoja wa wahitimu hao na kuongeza;

“Sasa ili tuweze kusimama kwa miguu yetu tunaomba halmashauri zitupe kipaumbele kwenye mikopo ya ama fedha au vifaa, tuna nia na uwezo wa kujijenga kiuchumi kupitia taaluma zetu, mikopo hiyo itatusaidia kujiajiri.”

Kwa upande wake Peter Jackson ambaye pia ni mmoja wa wahitimu, ameshauri kuwa pamoja na ombi hilo, kuna umuhimu kwa halmashauri kuwatengea maeneo maalumu ya kufanyia shughuli zao, hali itakayowawezesha kupatikana kiurahisi.

“Watukopeshe mitaji, iwe ni pesa au vifaa, lakini pia watutegee maeneo maalumu ili tunapozalisha bidhaa, iwe rahisi kwa wateja kujua tupo wapi na hata halmashauri au taasisi za fedha zitakuwa ni rahisi kututambua, tutazalisha, kuuza na kurejesha hiyo mikopo,” amesema.

Mkuu wa chuo hicho, Joseph Nchimbi amesema kuwa pamoja na mafanikio mbalimbali ambayo wameendelea kuyapata hasa kwa kuongeza kozi mpya na hata kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa, bado kuna changamoto zinazowakabili ikiwemo upungufu wa vitendea kazi vya kufundishia.

Nchimbi amesema kuwa kutokana na hali hiyo wameendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa bila kujali muda, lengo likiwa kuwaivisha wanafunzi wao na kupata ujuzi bora ambao utawasaidia maishani mwao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mussa Ndomba aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mahafari hayo aliyemwakilisha Mbunge wa Kibaha Mjini, amewataka wahitimu hao kutobweteka na kusubiri urithi kutoka kwa wazazi wao na badala yake wajiendeleze katika ujuzi na maarifa waliyopata.

Kuhusu ombi la wahitimu hao juu ya mikopo kiongozi huyo amesema kuwa uwezekano huo upo na takwimu zinaonyesha kuwa akikopeshwa mtu mwenye ujuzi na asiye na ujuzi, yule mwenye ujuzi ni mwepesi wa kurejesha mkopo kwa wakati.