Sababu uzalishaji madini ya vito vya thamani kupaa
Ili ukuaji wa ajira zinazozalishwa nchini na mapato yatokanayo na madini uonekane, uongezaji thamani umeendelea kuwa jambo linalopigiwa chapuo na watu tofauti.
Uongezaji thamani utaifanya nchi kunufaika zaidi na kuingiza fedha nyingi kwa kuuza bidhaa zilizotengenezwa badala ya kuuza madini ghafi.
Rai hii inatolewa wakati ambao uzalishaji wa madini ya vito vya thamani umeongezeka hadi kufikia kilo milioni 55.95 mwaka 2023, ikiwa ni mara 14 zaidi ya kilo milioni 3.85 zilizozalishwa mwaka 2021, kwa Mujibu wa Takwimu Msingi za mwaka 2023.
Kupitia takwimu hizo zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), wadau wanataja ongezeko la uzalishaji kuwa huenda umechochewa na kuwapo kwa mazingira mazuri, uhitaji wake sokoni na kudhibiti utoroshaji.
Akizungumzia ongezeko hilo, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka amesema ongezeko la uzalishaji huu huenda limeakisiwa na mazingira rafiki yaliyowekwa, huku akitaka maboresho katika eneo la uongezaji wa thamani.
Pia anasema kwa miaka ya nyuma, baadhi ya madini yalikuwa yanatoroshwa nje ya nchi, hivyo inawezekana mazingira mazuri yaliyowekwa yamefanya shughuli nyingi zifanyike ndani ya mipaka.
Hali hii imesaidia kuratibu na kuwezesha kuwapo kwa kumbukumbu nzuri za takwimu kwa kile kinachofanyika.
Dk Mwinuka anasema ukuaji huu una maana kubwa, kwani shughuli hizi zinawahusisha wadau wengi waliopo kwenye mnyororo wa thamani ya madini kuanzia wanaochimba, wafanyabiashara na wanaoongeza thamani.
“Ongezeko hili limewagusa wadau wengi kwenye mnyororo kuanzia wachimbaji wadogo kwa wakubwa wanaosafirisha madini hayo nje ya nchi kwa kuyaongezea thamani, ambayo imewagusa wengi, wakiwemo Serikali yenyewe na kuongeza kodi kubwa inayopatikana kwenye madini hayo,” anasema Dk Mwinuka
Anasema kama nchi ikiuza zaidi madiini haya inapata fedha nyingi za kigeni ambazo zitasaidia kuboresha huduma nyingine za kijamii.
Mchumi mwingine wa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo anasema kadiri nchi inavyozalisha madini mengi ndiyo fedha nyingi zinavyopatikana na inaongeza mchango wa madini kwenye ukuaji wa uchumi.
“Nikikupa data za harakaharaka mwaka 2017 mchango wa madini kwenye uchumi wetu ulikuwa asilimia 4, sasa hivi umezidi asilimia 10, kadiri tunavyozalisha zaidi ndivyo ambavyo tunapata fedha zaidi, ambapo mchango wa uzalishaji kwenye ukuaji wa uchumi unaongezeka,” anasema Profesa Kiyondo na kuongeza;
“Mpaka sasa hivi japo mchango unaongezeka, hatujafaidika inavyotakiwa katika madini yetu tunayozalisha, sababu kubwa sisi tunauza madini ghafi tunachimba jiwe halafu tunaliuza, lakini ukitaka kupata faida ya kutosha unatakiwa usiuze madini ghafi, inatakiwa uuze yaliyoongezewa thamani,” anasema.
Profesa Kiyondo alitolea mfano kwa mtu anayeuza jiwe la vito vya thamani anapata fedha kidogo ukilinganisha na yule anayeuza hereni na pete wanavyopata faida kubwa.
Anasema moja ya utafiti aliowahi kufanya nchini Zambia katika madini ya shaba aliona Wazambia wanavyouza madini ghafi ambayo yalikuwa yakitumika kutengeneza vifaa vya umeme, ikiwemo nyaya za umeme
“Tuliona madini wanapouza nje halafu anakuja kununua nyaya za umeme nje ya nchi ili kupeleka umeme vijijini, thamani ya mawe waliyouza nje ukilinganisha na waya wanaotengeneza wanapata fedha mara 22 kwa kuwa wameongezea thamani,” anasema.
Anasema kuuza madini ghafi maana yake thamani inapelekwa nje ya nchi, jambo linaloenda sambamba na kupotea kwa mapato, lakini pia anayeongezea thamani anapata fedha nyingi za kigeni kuliko mzalishaji.
Mbali na mapato, pia uuzaji wa madini ghafi ni sawa na kuuza ajira nje ya nchi, kwani huko yanakokwenda kuongezewa thamani viwanda huajiri watu na mapato yatakayopatikana yatasaidia kuongeza uchumi wa nchi husika.
“Maana yake sisi kuuza madini ghafi tunapoteza ajira ambazo zingebaki hapa ndani kama tungewekeza katika kuhakikisha kwamba tunaongeza thamani kwanza ili tupate faida kubwa,” anasema.
Kwa upande wa Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi anasema kama nchi, inahitaji kupata fedha nyingi za kigeni kwenye madini inatakiwa kuweka mazingira mazuri katika eneo hilo.
“Kuboresha mazingira yanayovutia katika uchenjuaji wa madini ili tuweze kupata thamani kubwa katika kuongezea thamani kuliko kuuza madini ghafi, kusimamia kodi na utoroshaji wa madini hayo,” anasema Dk Olomi.
Amesema fedha nyingi za kigeni zinapotea kwa kupeleka madini ghafi nje ya nchi, huku akitolea mfano kuwa yanayoweza kuuzwa kwa dola za Kimarekani 1,000 yakiongezwa thamani yanaweza kuuzwa hadi dola za Marekani 3,000.
“Endapo tukifanya hivi, tutapata fedha nyingi na hii itasaidia kupunguza mahitaji yetu kutoka nje ya nchi pamoja na kutufanya tuwe na uwezo wa kugharimia miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inahitaji fedha nyingi,” anasema Dk Olomi.
Kutokana na kutambua umuhimu wa uongezaji thamani, Waziri wa Madini, Antony Mavunde wakati akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2024/2025 alisema kuanzia sasa hawatatoa leseni ya kati na kubwa ya uchimbaji wa madini yote, yakiwemo madini mkakati na madini muhimu kwa mwekezaji yeyote kama hatokuwa na mpango mzuri wa kuongeza thamani madini hapa nchini.
“Lengo ni kuifanya nchi yetu ya Tanzania kunufaika na rasilimali madini ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia,” alisema Mavunde.
Alisema dhamira ya Serikali ni kutekeleza kwa dhati shughuli za uongezaji thamani madini muhimu na madini mkakati nchini kwa kutengeneza bidhaa zitokanazo na madini ghafi.
Ili kufanikisha hilo, Serikali imetenga eneo maalumu la ukanda wa kiuchumi la Buzwagi Special Economic Zone, lililopo Wilaya ya Kahama, lenye ukubwa wa ekari 1,333 ambapo awali lilikuwa na shughuli za uchimbaji madini kupitia Kampuni ya Barrick.
Pamoja na masuala mengine, eneo hilo litatumika kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini na uzalishaji wa bidhaa za migodini.
Ujenzi wa viwanda hivyo utaongeza fursa za ajira, ujuzi kwa Watanzania, kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea upatikanaji wa mapato.
“Pia viwanda vitakavyojengwa kwa awamu ya kwanza ni kiwanda cha usafishaji na uongezaji thamani madini, Steel Balls Manufacture, Mine Conveyor Belts, Solar Farms na Portable Water Plant. Hatua hii itasaidia upatikanaji wa bidhaa za migodini ambazo awali zilikuwa zikiagizwa kutoka nje ya nchi,” anasema Mavunde.