Sababu Watanzania kufanya ununuzi dakika za mwisho
Msimu wa sikukuu na mapumziko unapofikia tamati huwa ni jambo la kawaida kushuhudia wimbi kubwa la watu wakielekea sokoni kununua mahitaji ya shule kwa muhula mpya unaoanza.
Hali kama hiyo hujitokeza pia katika misimu ya sherehe kama Eid na Krismasi, ambapo kadiri siku ya sherehe inavyokaribia, ndivyo masoko, maduka na mitaa inavyojaa watu wanaofanya ununuzi kwa haraka.
Mtu akitazama hali hiyo, hujiuliza maswali kadhaa, kwa nini watu hawa wote husubiri hadi siku za mwisho? Kwa nini waingie kwenye msongamano mkubwa, gharama za juu za bidhaa na usumbufu wa usafiri, ilhali walikuwa na muda wa kufanya ununuzi mapema?
Moja ya maelezo ya jambo hili linaweza kupatikana katika saikolojia ya wanunuzi hususani kupitia dhana ya kiuchumi inayojulikana kama temporal discounting. Kwa mujibu wa dhana hii, binadamu huwa na mwelekeo wa kuthamini zaidi mahitaji ya sasa kuliko yale ya baadaye.
Katika muktadha wa ununuzi, watu wengi huahirisha maandalizi ya siku zijazo, wakitanguliza matumizi yanayoonekana kuwa ya haraka zaidi huku ununuzi wa sikukuu ukisubiri hadi pale yanapokuwa ya lazima au ya dharura.
Kwa uzoefu wa kijamii, Watanzania wengi hutambua mapema kwamba kuchelewesha ununuzi katika misimu ya sikukuu huleta changamoto nyingi, ikiwemo kupanda kwa bei na msongamano mkubwa wa watu.
Hata hivyo, uelewa huo hauwazuii kuacha tabia ya kusubiri hadi siku za mwisho, pale ambapo kauli ya “lala salama” inapogeuka kuwa msukumo wa kwenda sokoni kesho au keshokutwa ndiyo sherehe.
Sababu nyingine muhimu ni hali ya kipato. Idadi kubwa ya Watanzania hawana mapato ya kudumu au yanayotabirika. Takwimu za utafiti wa FINSCOPE wa mwaka 2023 zinaonyesha kuwa takribani asilimia 89 ya Watanzania wanategemea shughuli za msimu, vibarua au biashara ndogondogo za kujiajiri kama chanzo kikuu cha kipato.
Katika mazingira haya, kupanga ununuzi kwa mwezi ujao huwa changamoto hasa pale fedha iliyopo ikiwa inahitajika kukidhi mahitaji ya msingi kama chakula.
Kwa hali hiyo, familia nyingi hulazimika kusubiri hadi pale zitakapopata fedha, mara nyingi karibu na tarehe ya sherehe ndipo zikamilishe manunuzi yao.
Hii ni tofauti na watu wanaopata mishahara ya kila mwezi, ambao wana uhakika wa mapato na hivyo wana nafasi kubwa zaidi ya kupanga bajeti na kufanya manunuzi mapema.
Mfumo wa biashara nao una mchango wake. Katika masoko makubwa kama Kariakoo jijini Dar es Salaam, wafanyabiashara wengi wa nguo, viatu, mapambo na bidhaa za sherehe hulazimika kwanza kuuza mzigo uliopo ili kupata mtaji wa kuagiza bidhaa mpya kutoka nje ya nchi kama Dubai au China.
Hali hii husababisha bidhaa mpya na mitindo ya kisasa kuchelewa kufika sokoni. Matokeo yake, hata wanunuzi wanaotaka kununua mapema hukosa chaguo walizokusudia. Kauli kama “mzigo mpya unaingia karibuni” zimekuwa sehemu ya lugha ya kila siku ya biashara.
Bidhaa hizo mpya zinapowasili, mara nyingi huwa ni muda mfupi tu kabla ya kilele cha sherehe hali inayosababisha msongamano mkubwa wa watu wanaoharakia kupata walichoona kuwa kizuri zaidi.
Katika kipindi hicho, wauzaji huongeza saa za kazi, wakitangaza kuwa wako wazi hadi usiku, huku wanunuzi wakimiminika kwa wingi kufanya manunuzi ya dakika za mwisho.
Shinikizo la muda, hofu ya bidhaa kuisha na hamasa ya sikukuu humfanya mnunuzi kufanya maamuzi ya haraka mara nyingi bila kulinganisha bei au ubora.
Nadharia za tabia za wanunuzi zinaonya dhidi ya ununuzi wa aina hii unaojulikana kama ununuzi wa dharura au wa msukumo.
Ununuzi wa “lala salama” mara nyingi humgharimu mnunuzi zaidi, humnyima nafasi ya kufanya uamuzi wa busara na hatimaye huathiri vibaya bajeti ya mtu binafsi au familia. Si ajabu, baada ya msimu wa sherehe, familia nyingi hujikuta katika hali ngumu ya kifedha, wakisema “nimebaki mweupe”.
Kwa msingi huo, kuna haja kwa wadau mbalimbali hususan taasisi za kifedha na kielimu, kuimarisha elimu ya fedha binafsi.
Elimu hiyo inapaswa kusisitiza umuhimu wa kupanga bajeti, kuweka akiba, na kufanya ununuzi mapema. Ingawa kibiashara msongamano wa manunuzi ya msimu wa sikukuu huonekana kuwa fursa ya faida, kwa upande wa mlaji, si lazima iwe faida ikiwa haijaendeshwa kwa mipango na nidhamu ya kifedha.