Prime
Sababu Watanzania kukopa
Muktasari:
- Ripoti ya BoT yaonyesha kuwa asilimia 67.7 ya mikopo binafsi mwaka 2024 ilielekezwa kwenye matumizi kama ujenzi, elimu, matibabu na magari badala ya uzalishaji. Wachambuzi wanasema hali hiyo inaonyesha ukosefu wa taasisi maalumu za kifedha kwa sekta kama kilimo na nyumba.
Dar es Salaam. Takriban asilimia 67.7 ya mikopo binafsi waliyokopa Watanzania mwaka jana ilielekezwa kwenye shughuli zisizo za uzalishaji kama ujenzi, elimu, matibabu na ununuzi wa magari.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Uhimilivu wa Kifedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyotolewa wiki iliyopita, ujenzi ulikuwa kinara kwa asilimia 19.6, ukifuatiwa na elimu (asilimia 19.2), matibabu (asilimia 14.7) na ununuzi wa magari (asilimia 14.2).
Hali hiyo inaonesha kuwa Watanzania wengi hutumia mikopo kukidhi mahitaji ya maisha badala ya kuwekeza kwenye shughuli za kipato.
Hata hivyo, biashara na kilimo zilipewa kipaumbele na asilimia 16.6 na 15.7 mtawalia, zikionesha juhudi za baadhi ya wakopaji kuelekeza fedha kwenye uzalishaji.
BoT inasema kumekuwa na ongezeko la mikopo binafsi katika miaka sita iliyopita, kutoka asilimia 29.7 mwaka 2019 hadi 36.7 ya mikopo yote mwaka jana, iliyotolewa na benki kutokana na kushuka kwa riba, kuongezeka kwa muda wa marejesho na kiwango cha mikopo.
“Uboreshaji wa mazingira ya biashara na kukua kwa uchumi kumeongeza mapato ya kaya na kuhamasisha matumizi pamoja na uwekezaji,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, BoT ilipunguza kwa asilimia 50 uzito wa hatari katika mikopo binafsi, hatua iliyosababisha benki kupunguza riba, kuongeza kiwango cha mkopo na kurefusha muda wa marejesho, ili kuvutia wakopaji zaidi.
Hata hivyo, wachambuzi wa kifedha wanaonya kuwa ni muhimu kuweka uwiano kati ya matumizi ya kuboresha maisha na uwekezaji wa kipato, ili kudhibiti madeni na kuhakikisha ustawi wa kifedha wa muda mrefu.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa hali ya kifedha ya kaya imeimarika, hivyo wakopaji wamekuwa waaminifu zaidi kwenye marejesho, hali iliyopunguza mikopo chechefu (NPLs).
Baadhi ya kaya zimewekeza kwenye biashara, kilimo na mali za kifedha, hali inayoboresha mtiririko wa fedha na kuimarisha uwezo wao wa kukopa tena, huku zingine zikifanya mali zilizopatikana kwa mkopo kuwa dhamana ya mikopo ijayo.
BoT inasema benki zinaendelea kukopesha kwa masharti nafuu kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na kupungua kwa wakopaji wasiolipa.
Kauli za Wachambuzi
Dk Lutengano Mwinuka, mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), anasema matumizi ya mikopo kwa shughuli za kaya bado ni kawaida kwa kuwa Watanzania wengi wako kwenye hatua za awali za ukuaji wa uchumi.
“Ni jambo la kawaida kutumia mikopo kwa mahitaji ya kaya kwa sababu wengi bado wako kwenye mchakato wa kukuza uchumi wao,” anasema.
Anaongeza:“Hali ya uchumi wa watu bado inakua hatua kwa hatua, hivyo wanaelekeza mikopo yao kwenye masuala ya familia kwanza, kisha huja kuelekeza kwenye uwekezaji.”
Licha ya kukiri kuwa mikopo imeboresha maisha ya Watanzania wengi, Dk Mwinuka anatoa angalizo kwa wafanyakazi wanaotegemea mishahara yao katika kulipa madeni, akisema ni muhimu kutathmini sababu ya kukopa kabla ya kuamua kukopa.
“Ikiwa mikopo inalipwa vizuri si tatizo, lakini ni vyema mikopo ikaelekezwa kwenye uwekezaji kama ujenzi wa nyumba za kupangisha, badala ya kuwa zaidi kwa matumizi ya kawaida ya familia,” anasema.
Kwa upande, Dk Tobias Swai, Mhadhiri Mwandamizi wa Fedha na Benki kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema matumizi ya mikopo binafsi kwa zaidi ya asilimia 36.2 kufadhili biashara ndogo, makazi na magari ni ishara ya upungufu katika mfumo wa kifedha nchini.
“Matumizi haya ni kiashiria kuwa hatuna taasisi maalumu kama benki za nyumba, kampuni za ukodishaji magari na taasisi za kufadhili biashara ndogo. Hivyo watu wanalazimika kutumia mikopo binafsi kufadhili hata shughuli za uzalishaji,” anasema.
Anaongeza kuwa hali hiyo inazua mkanganyiko kati ya matumizi ya kawaida na ya uzalishaji, jambo ambalo linaathiri ujumuishwaji wa kifedha na ukuaji wa uchumi.
Biashara ndogo nyingi bado hazijasajiliwa rasmi, jambo linalowazuia kupata mitaji ya gharama nafuu kwa muda mrefu, na hivyo kudhoofisha ukuaji wao na kuongeza changamoto za kulipa kodi.
Anaeleza mikopo kwa kilimo imepanda hadi asilimia 12.4, lakini bado sehemu kubwa ya fedha hizo hupitia mikopo ya binafsi.
Dk Swai anahimiza umuhimu wa kuwa na taasisi za kifedha maalumu kwa sekta kama kilimo, akitolea mfano benki mpya ya Ushirika ya Biashara kama hatua nzuri ya kuelekeza fedha kwenye vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, mchambuzi huru wa uchumi Oscar Mkude anasema watumishi wa umma na wafanyabiashara wanakopa kwa kutumia mikataba ya ajira na mishahara yao kama dhamana, huku akibainisha kuwa maofisa wa Serikali ndiyo wanakopa zaidi kutokana na uhakika wa kipato chao.
Mkude anaongeza kuwa uhitaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya elimu pia unasababisha watu wengi kukimbilia mikopo ya benki, hasa kutokana na masharti magumu ya kukopa kutoka serikalini.
“Wengi hulazimika kukopa kwa ajili ya elimu kutokana na ugumu wa kupata mkopo wa HESLB, hivyo wanatafuta njia mbadala kupitia benki,” anasema.
Anaeleza mfumo wa benki nchini haujaendelezwa vya kutosha katika huduma za mikopo ya nyumba kama ilivyo Ulaya, ambako mikopo ya ujenzi hupangwa vizuri na kuwa na hatari ndogo zaidi.
Anaongeza kuwa upungufu wa uaminifu kwa baadhi ya waombaji wa mikopo pamoja na taarifa zisizo sahihi za mahitaji hupunguza utayari wa benki kukopesha, hasa kwenye sekta kama kilimo.
“Kilimo bado ni hatari kwa sababu ya mvua zisizotabirika na tija ndogo, lakini kama tungewekeza kwenye mifumo ya umwagiliaji, wakulima wengi wangeweza kufikiwa na huduma za kifedha kwa urahisi zaidi,” anaeleza.
Ripoti ya Finscope Tanzania ya mwaka 2023, inaonesha zaidi ya asilimia 42 ya Watanzania waliopata mikopo walikopa kupitia taasisi rasmi kama benki na taasisi za mikopo ya kijamii (Saccos), huku asilimia 29 wakitegemea wakopeshaji binafsi au vikundi vya kijamii.
Ripoti hiyo pia inaeleza ongezeko la matumizi binafsi ya mikopo linachangiwa na kasi ya mabadiliko ya maisha ya kijamii, ambapo Watanzania wengi wanazidi kuingia kwenye mfumo wa kifedha rasmi, lakini bado wanakopa zaidi kwa ajili ya matumizi ya kawaida kuliko uwekezaji.
Aidha, Ripoti ya Tanzania National Panel Survey (2020–2021) iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonesha asilimia 53 ya kaya nchini zilieleza kuwa zilishindwa kukidhi mahitaji muhimu ya maisha bila mikopo, ikiwa ni pamoja na ada za shule, matibabu na ujenzi wa nyumba.