Sababu Watanzania kutonunua bidhaa za ndani

New Content Item (1)


Muktasari:

 Ubora na unafuu wa bei za bidhaa zinazotoka nje ya nchi ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuwafanya Watanzania kuchangamkia bidhaa hizo kuliko zianzozalishwa ndani ya nchi.


Dar es Salaam. Ubora na unafuu wa bei ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuwafanya Watanzania kuchangamkia bidhaa zianzozalishwa nje ya nchi kuliko za ndani.

Nyingine ni ushindani wa bei sokoni unaodhoofishwa na changamoto za kisera, kikodi hatua inayoathiri  baadhi ya  bidhaa zinazotengenezwa ‘kiujanja ujanja’.

Wakati wazalishaji wakiendelea kulalamika kukosa wateja, watafiti wanaendelea kuumiza vichwa kuhusu mkwamo huo, ikiwamo Taasisi ya Utafiti Repoa iliyofuatilia changamoto hiyo kiutafiti.

Hali hiyo inajitokeza ikiwa ni siku tatu zimepita baada ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji kutoa rai kwa Watanzania kuacha kununua bidhaa zinazotoka nje.

“Tanzania ina viwanda vinavyotengeneza bidhaa nzuri zisizokuwa na mashaka, zina viwango vyote vinavyotakiwa na taasisi za ukaguzi,” alisema Dk Ashatu wakati wa ziara yake katika Viwanda vya Motisum (IMMI Steel).

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Repoa, Dk Donald Mmari amesema yako maeneo ya kufanyia marekebisho kisera, kikodi kwa kuwa kikwazo ni ushindani wa bei ya bidhaa sokoni.

Dk Mmari amefafanua akisema unafuu wa bei ya bidhaa husika huathiriwa na gharama za uzalishaji katika viwanda vya ndani kuliko zinazotoka nje.

“Kiwanda kikitumia jenereta ya mafuta kuzalisha badala ya umeme inaathiri bei ya bidhaa, mfano ni bidhaa zinazotoka China, nguo, viatu ziko chini kuliko zinazozalishwa na viwanda vya ndani,” amesema Dk Mmari.

Kuhusu hoja ya ushindani wa bei ya bidhaa, Katibu Mkuu wa Chama cha Wadau wa Ngozi Tanzania (LAT), Fred Kabala ameshauri Serikali kutazama sera zake kwa mzalishaji wa ndani.

“Kwa mfano, mzalishaji wa Afrika Kusini ni tofauti kabisa na mzalishaji wa Tanzania, wao wanapata umeme kwa bei nafuu na Serikali yao haiwatozi kodi wakati wa kuanza ila baada ya kukua ndio wanaanza kuwatoza kodi, tofauti na sisi, utitiri wa kodi unapoanza,”amesema  Kabala.

Kwa mujibu wa takwimu za Ripoti ya Tanzania in figure ya mwaka 2022, Tanzania imeendelea kuwa na tofauti kubwa kati ya ununuzi wa bidhaa kutoka nje kuliko inavyouza nje.

Kati ya mwaka 2018/2022, mauzo ya Tanzania nje yaliongezeka kwa asilimia 35.7 ikilinganishwa na asilimia 48 ya ilivyokuwa ikiagiza kutoka nje. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda, hadi Machi mwaka jana, kulikuwa na jumla ya viwanda 80,976.

Idadi ya vidogo sana ilikuwa 62,400, vidogo ni 17,274, vya kati ni 684 na vikubwa ni 618 huku Wizara ya Viwanda ikiahidi ujenzi wa viwanda vipya 500 kabla ya mwaka 2025.