Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kuboresha eneo la matengenezo ya ndege Kia

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, akikagua eneo la matengenezo na ukarabati wa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati wa ziara yake ya kutembelea na kujionea maendeleo ya huduma za usafiri wa anga, Juni 13, 2026. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Uwekezaji huo unalenga kuimarisha huduma za matengenezo ya ndege ndani ya nchi na kupunguza matumizi ya fedha zinazotumika kupeleka ndege nje ya nchi kwa ajili ya matengenezo.

Hai. Serikali kupitia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) imeanza maboresho makubwa ya eneo la matengenezo na ukarabati wa ndege (hanga) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), hatua inayolenga kupunguza matumizi ya fedha zinazotumika kupeleka ndege nje ya nchi kwa ajili ya matengenezo.

Eneo hilo, ambalo lina uwezo wa kuhudumia ndege tano kwa wakati mmoja, linatarajia kugharimu Sh2 bilioni kwa ajili ya matengenezo yake ikiwemo lango kuu la kuingilia ndege, mifumo ya taa, maeneo kwa ajili ya shughuli za kitaaluma pamoja na ununuzi wa vifaa vya mafunzo kwa wataalamu ili kuimarisha uwezo wa kutoa huduma za matengenezo na ukarabati wa ndege kwa viwango vya kisasa.

Akizungumza leo Juni 13, 2026 baada ya kukagua eneo hilo pamoja na nyumba 38 za watumishi wa ATCL zinazokarabatiwa katika eneo la Kia, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya anga ili kuongeza ufanisi wa huduma na kukuza uchumi wa nchi.

“Kama mnavyofahamu, katika miaka ya hivi karibuni Serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya anga, takribani Sh1 trilioni imeelekezwa katika ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege mbalimbali nchini, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro,” amesema Kihenzile.

Kihenzile amesema maboresho hayo yatawezesha ndege za ATCL pamoja na ndege za mashirika mengine yanayofanya kazi nchini kupata huduma za matengenezo ndani ya Tanzania badala ya kupelekwa nje ya nchi.

“Tunapoboresha eneo hili la matengenezo ya ndege, tunatoa tafsiri kwamba ndege zetu za ATCL tulizonazo 16 pamoja na ndege nyingine zinazofanya kazi nchini zinaweza kutengenezwa hapa. Hii itasaidia kupunguza fedha zinazotoka nje ya nchi na wakati huo huo kuongeza ajira kwa Watanzania,” amesema Kihenzile

Aidha, amesema eneo hilo ni moja ya miundombinu muhimu iliyojengwa miaka iliyopita na limeendelea kuwa mfano wa uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya anga kutokana na ubora wake.

Mbali na maboresho hayo ya matengenezo ya Ndege , amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya watumishi wa ATCL kwa kukarabati nyumba 38 zilizojengwa miaka ya 1990 kwa gharama ya takribani Sh5 bilioni.

“Nyumba hizi zikikamilika zitaboresha maisha ya watumishi wetu wengi ambao kwa sasa wanakabiliwa na changamoto za kupanga nyumba nje ya eneo la kazi, ikiwemo gharama kubwa za kodi na masuala ya usalama,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa shirika hilo, Diamond Kisombe, amesema mradi huo ni sehemu ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuimarisha sekta ya anga nchini.

“Mbali na ukarabati wa miundombinu iliyopo, Serikali inaendelea kufanya maboresho zaidi katika eneo hili kwa kununua vifaa vya mafunzo kwa wataalamu wa matengenezo ya ndege na kuongeza maeneo ya shughuli za mafunzo na kazi mbalimbali za kitaaluma,” amesema Kisombe.

Amesema maboresho hayo yanatarajiwa kukamilika katika mwaka ujao wa fedha, hatua itakayoongeza uwezo wa shirika kutoa huduma za matengenezo na ukarabati wa ndege kwa viwango vya kisasa.

Naye, Mkandarasi anayesimamia miradi hiyo kutoka kampuni ya ujenzi ya Humphrey Construction, Humphrey Soka, amesema mradi wa ujenzi wa nyumba 38 za watumishi umefikia asilimia 77 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitano ijayo.

“Tunashukuru Serikali kwa kuendelea kutuamini kusimamia miradi hii mikubwa hapa Kia. Sisi ni watu wenye historia ya kufanya kazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), hivyo tumejizatiti kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa,” amesema Soka.