Serikali yaeleza mafanikio ya miradi ya miundombinu Iringa
Iringa. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika Mkoa wa Iringa, akisema hatua hiyo imeufanya mkoa huo kunufaika kiuchumi kupitia miradi ya ujenzi wa uwanja wa ndege, reli na maboresho ya bandari.
Akizungumza Mei 24, 2026 katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba uliofanyika katika Viwanja vya Stendi ya Luganga mkoani Iringa, Kihenzile amesema kukamilika kwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Uwanja wa Ndege wa Nduli kumesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza shughuli za biashara, kilimo na utalii.
Amesema zaidi ya Sh60 bilioni zimetumika katika uboreshaji wa uwanja huo wa kihistoria, hatua ambayo imefungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakazi wa Iringa na maeneo jirani.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo ameeleza dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kufufua upya reli ya TAZARA, akisema ukarabati wake utaongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo, hususan mazao kutoka wilayani Kilolo.
Amebainisha kuwa mwaka 2022, Serikali ilisaini mkataba wa ukarabati wa reli hiyo wenye thamani ya Sh trilioni 3.3, hatua ambayo inalenga kurejesha uwezo wa reli hiyo kama ilivyokusudiwa awali.
“Hii ni reli ya kihistoria… ilijengwa ikiwa na uwezo wa kubeba mizigo mikubwa, lakini ilipungua ufanisi kutokana na changamoto za miundombinu. Ukarabati huu utairejesha hadhi yake,” amesema Kihenzile.
Aidha, amezungumzia pia maboresho yanayoendelea katika sekta ya bandari, akisema yameongeza ufanisi wa huduma na kuvutia wadau mbalimbali wa uendeshaji, jambo ambalo tayari linaonyesha matokeo chanya kiuchumi.