Kihenzile awahimiza wawekezaji kutumia fursa sekta ya usafiri
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, akizindua rasmi Maonesho ya Usafiri Endelevu Ardhini yenye kauli mbiu Nishati safi na Ubunifu katika usafirishaji yanayofanyika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam Novemba, 24 hadi 29 2025 ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini mwaka 2025.
Muktasari:
- Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kuwekeza katika sekta ya usafiri, ikiboresha reli, barabara na usalama wa abiria, hatua itakayopunguza ajali, gharama na kuongeza ufanisi wa usafirishaji nchini.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya usafiri, akisema Serikali imeweka mazingira wezeshi, hususani katika miundombinu ya reli na usafiri wa barabara, ikiwamo mfumo wa mabasi ya mwendokasi.
Amesema kuwa katika mijadala kuhusu kuhamasisha usafiri unaozingatia matumizi sahihi ya nishati, utunzaji wa mazingira na kupunguza ajali, lengo kuu ni kuhakikisha binadamu anaposafiri anajiona yuko salama kuanzia anapotoka hadi anapofika.
Hatua hizi zitachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya wananchi vinavyotokana na ajali pamoja na kupunguza gharama za usafirishaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Novemba 24, 2025 wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Wiki ya Usafiri Endelevu Duniani, ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza nchini, Kihenzile amesema Serikali imefanya maboresho katika sera, kanuni na sheria ili kuruhusu sekta binafsi kuwekeza moja kwa moja kwenye shughuli za usafiri, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
“Serikali imejenga miundombinu sasa mwekezaji binafsi anaruhusiwa kuja na mabehewa yake, kuleta mitambo yake na kuendesha. Tumefanya hivi kwa sababu tunaendelea kujenga reli katika maeneo mengi, hivyo rasilimali tulizonazo zinajielekeza kwenye kuendeleza miundombinu hiyo,” amesema Kihenzile
Kihenzile amesema hatua hiyo inalenga kuwashirikisha wananchi na wadau kushika nafasi katika uchumi, sambamba na kuvutia wawekezaji kutoka mataifa mengine kuleta teknolojia na ubunifu utakaowezesha sekta ya uchukuzi kuendana na mahitaji ya sasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Habib Suluo amesema maonyesho hayo yamevutia kampuni zaidi ya 60 kutoka ndani na nje ya Tanzania, jambo linaloonesha kutambuliwa kwa hatua zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuboresha sekta ya usafiri.
Amesema maonyesho hayo yataenda sambamba na kongamano maalumu linalotarajiwa kuanza kesho Novemba 25, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Usafiri Duniani ambayo huadhimishwa Novemba 26 kila mwaka.
Amesema maonyesho ya mwaka huu yanajikita katika mapendekezo mapya ya kimataifa ya kupunguza uchafuzi wa mazingira kupitia miongozo ya Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), inayozitaka taasisi za umma na binafsi kutoa taarifa za uzalishaji hewa ukaa ili kubaini maeneo yanayochangia uharibifu wa mazingira.
“Tunazungumzia hewa ukaa zinazotokana na uzalishaji wa moja kwa moja kama magari na mitambo. Unapunguza matumizi ya vyanzo hivyo ili kupunguza mchango wako katika uchafuzi wa mazingira,” amesema Suluo.
Pia, amesema kuwa uchafunzi mwingine unahusisha athari zisizo za moja kwa moja zinazojitokeza kutokana na matumizi ya nishati au huduma nyingine zinazotumika katika uendeshaji.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Reli Kusini mwa Afrika (SARA), Raymond Shoniwa amesema Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kutokana na kasi ya maendeleo inayoendelea kushudiwa katika sekta ya reli na miundombinu mingine ya usafiri.
Shoniwa amesema uongozi wa SARA unaendelea kuvutiwa na hatua kubwa zinazochukuliwa na Tanzania, kiasi kwamba bodi nzima ya jumuiya hiyo ingetamani kuwepo nchini kujionea hali halisi.
“Tuna hamasa kubwa na maendeleo yanayoendelea kutokea nchini. Tulitamani bodi nzima iwe hapa wakurugenzi wote wangependa sana kuwepo lakini tunalipanga hilo. Mwezi Juni mwakani tutafanya kikao chetu cha bodi hapa ili tujifunze,” amesema Shoniwa.
Ameongeza kuwa mara nyingi wananchi wa nchi husika hawatambui thamani ya maendeleo waliyo nayo, tofauti na wageni wanaoyaona kwa mtazamo wa nje.
“Wakati mwingine ukiwa ndani ya nchi hutambui ulichonacho, lakini sisi tunapoona kutoka nje tunaona maendeleo makubwa. Tunayapenda, tunayashangaa na tunajifunza kutoka kwenu. Ndio maana tulipanga kuwaleta wakurugenzi wote wa reli kutoka ukanda huu waje kujifunza mnachofanya hapa,” amesema.
Shoniwa amesema katika ziara zake za miezi ya hivi karibuni katika nchi mbalimbali kama Msumbiji na Angola, ameona tofauti kubwa katika maendeleo ya reli ukilinganisha na Tanzania.