Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kihenzile aipongeza TCAA utekelezaji mradi wa VHF

Muktasari:

  • Kihenzile ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo uliopo eneo la Lolkisale, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kusimamia kwa mafanikio utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayoendelea kuboresha sekta ya usafiri wa anga nchini kwa niaba ya Serikali.

Akizungumza katika ziara yake yenye lengo la kukagua miradi kwenye eneo la Lolkisale, wilayani Monduli ambayo ni mojawapo ya maeneo ya utekelezaji wa Mradi wa Mawasiliano ya Sauti baina ya Rubani na Mwongozaji Ndege (VHF), Kihenzile amesema TCAA imeonesha dhamira ya dhati katika kuboresha huduma za anga, jambo linaloongeza usalama na ufanisi katika usafirishaji wa anga.

Mradi huo wa mawasiliano kupitia mfumo wa VHF umegharimu Sh31.6 bilioni na unatekelezwa katika vituo vikubwa 18 na visaidizi 12 kote nchini. 

Kwa mujibu wa Meneja wa mradi, Mhandisi Francis Chale, utekelezaji umefikia asilimia 90 na tayari baadhi ya vifaa vimeanza kufanya kazi katika kipindi cha majaribio.

"Mradi huu ni miongoni mwa hatua muhimu zinazolenga kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Tunaamini utasaidia kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto zilizokuwa zikijitokeza awali," amesema Mhandisi Chale.

Katika ziara hiyo, Kihenzile pia ametembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambako alishuhudia kwa karibu mazingira ya kazi ya waongozaji ndege na namna miundombinu mipya inavyorahisisha kazi zao.

“Hatua hizi ni sehemu ya maono ya Serikali katika kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha usafiri wa anga katika ukanda huu wa Afrika. Kufuatia ufungaji wa rada nne za kisasa za kuangazia anga, sasa tunaongeza uwezo wa mawasiliano ya moja kwa moja na rubani, hatua inayoinua kiwango cha usalama na udhibiti wa anga letu,” amesisitiza Waziri Kihenzile.

Amesema kwa mafanikio hayo, Serikali inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuwekeza katika miundombinu ya usafiri wa anga ili kuhakikisha usalama, ufanisi na ushindani wa sekta hiyo unakuwa wa hali ya juu.