Serikali kutumia Sh700 milioni kujenga soko la kisasa Mamsera, Rombo
Baadhi ya viongozi wakikagua mradi wa ujenzi wa soko la Mamsera Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kuongeza fursa za masoko kwa wazalishaji wa mazao mbalimbali, huku ukiimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo katika eneo hilo.
Rombo. Serikali imeanza ujenzi wa soko la kisasa la Mamsera katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, hatua inayotarajiwa kusaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuboresha mazingira ya biashara kwa wakulima na wafanyabiashara.
Mradi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh700 milioni, ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya masoko ya mazao ya kilimo na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika eneo hilo.
Akizungumza leo Juni 14, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Profesa Peter Msofe amesema soko hilo ni sehemu ya miradi inayotekelezwa na Serikali nchini kote kwa lengo la kuboresha masoko ya mazao ya kilimo na kuwawezesha wakulima kupata maeneo salama ya kuuza bidhaa zao.
Profesa Msofe amesema kukamilika kwa soko hilo Septemba 30, 2026 kutasaidia kuongeza uhakika wa masoko kwa mazao yanayozalishwa katika eneo hilo, ikiwamo ndizi na parachichi, sambamba na kuongeza ajira na mapato ya wananchi.
“Huu ni miongoni mwa miradi ambayo Serikali inaitekeleza nchini kote ili kuhakikisha wakulima wanapata maeneo salama ya kuuza mazao yao. Soko hili litakuwa kubwa na tunatarajia litakapokamilika litahudumia wafanyabiashara zaidi ya 700 kwa wakati mmoja,” amesema Profesa Msofe.
Amesema uwepo wa soko hilo pia utasaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, changamoto ambayo imekuwa ikiikabili sekta ya kilimo nchini kwa muda mrefu.
“Tanzania bado ina changamoto kubwa ya upotevu wa mazao baada ya mavuno. Ujenzi wa masoko ya kisasa kama hili ni moja ya njia za kupunguza upotevu huo na kuongeza mapato kwa wakulima pamoja na halmashauri,” amesema Profesa Msofe.
Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi kupitia uwekezaji katika miundombinu ya masoko, miradi ya umwagiliaji na masoko ya kimkakati ya mipakani ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumzia soko la kimkakati la Holili, amesema Serikali imetenga fedha katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kufanya tathmini ya mradi huo kabla ya kuanza ujenzi wake.
“Soko la Holili ni miongoni mwa masoko ya kimkakati yanayopangwa kujengwa katika maeneo ya mipakani kwa lengo la kunufaika zaidi na biashara za kuvuka mipaka,” amesema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda ameishukuru Serikali kwa kuanza ujenzi wa soko hilo akisema litakuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi wa wananchi wa eneo hilo.
Aidha, Profesa Mkenda amesema Rombo ina fursa kubwa ya uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula, hususan ndizi, ambazo zimeanza kupata masoko ya kimataifa ikiwamo Urusi.
Mmoja wa wakazi wa Mamsera, Joshua James amesema ujenzi wa soko hilo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya wakulima wa Rombo kwa kuwa utasaidia kupunguza changamoto ya kukosa masoko ya uhakika kwa mazao yao.
“Ninaamini soko hili litatusaidia kuuza mazao yetu kwa urahisi zaidi na kwa bei nzuri tofauti na ilivyokuwa awali ambapo tulilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta wanunuzi," amesema.
Naye, mfanyabiashara wa eneo hilo, Agripina Tesha amesema uwepo wa soko la kisasa utarahisisha shughuli za biashara na kuvutia wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali, jambo litakaloongeza mzunguko wa fedha katika wilaya hiyo.