Serikali kuweka nguvu kiwanda cha kutengeneza ndege Morogoro

Muktasari:
- Baada ya wawekezaji kuwekeza katika uunganishaji wa ndege nchini, Serikali sasa kuangalia jinsi ya kuwasaidia wawekezaji hao.
Dodoma. Wizara ya Uchukuzi imesema inategema kukutana na Wizara ya Fedha ili kuweka utaratibu wa kusaidia sekta ya anga hasa kwa kampuni zinazounganisha na kutengeneza ndege nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyrara ameyasema hayo baada ya kutembelea Kampuni ya Airplane Africa Limited iliyopo Mazimbu mkoani Morogoro.
Kampuni inayomilikiwa na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Czech, inafanya kazi ya kuunganisha na kutengeneza ndege za kubeba abiria wawili mpaka wanne.
“Uwekezaji huu ni mkubwa na hivyo nitawasiliana na Wizara ya Fedha ili tuone naona ya kuwekea mazingira mazuri wawekezaji hawa,” amesema Kahyrara katika taarifa kitengo cha mawasiliano cha Wizara ya Uchukuzi.
Amesema mafundi wanaofanya kazi katika kiwanda hicho wengi wao wamesoma Chuo cha Usafirishaji (NIT), hivyo kiwanda hicho ni muhimu kwasababu kitasaidia kutoa uzoefu kwa wanafunzi wa kutoka vyuo vya vikuu, vyuo vya kati na vyuo vya ufundi.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Igor Stratl amesema wamevutiwa kuwekeza Tanzania kwa sababu ni nchi yenye usalama, utulivu, amani na hivyo imewarahisishia kufanya kazi zao muda wote.
Mmoja wa mafundi, Lilian Petrol amesema ufundi wa kutengeneza ndege ameupata kutoka NIT, hivyo umesaidia kufanya kazi katika kiwanda hicho.
Ameiomba Serikali kuendelea kuongeza vivutio zaidi ili wawekezaji zaidi waweze kuja na vijana kuendelea kupata ajira.
Amesema kiwanda hicho kilichoanza mwaka 2021 mpaka sasa kimeunganisha na kutengeza ndege zaidi ya tatu na ndege hizo zinaweza kuuzwa katika nchi mbalimbali.