Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaonya waongoza watalii kuvunja sheria za hifadhi

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Catherine Mbena, akizungumza na waandishi wa habari katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Muktasari:

  • Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka waongoza watalii nchini kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya hifadhi, hususan katika kipindi hiki cha ongezeko la wageni, ikisema baadhi yao wamekuwa wakikiuka kanuni ikiwemo kuendesha magari kwa mwendokasi, kutoka nje ya barabara rasmi na kuruhusu wageni kuwagusa wanyamapori, hali inayohatarisha usalama wa watalii na wanyama hao.

Serengeti. Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka waongoza watalii nchini kuhakikisha wanazingatia kikamilifu sheria, taratibu na miongozo ya hifadhi wanapokuwa ndani ya maeneo ya hifadhi, hususan katika kipindi hiki ambacho idadi ya watalii wanaoingia nchini imeongezeka.

Serikali imesema baadhi ya waongoza watalii wamekuwa wakikiuka taratibu mbalimbali za uhifadhi, ikiwemo kuendesha magari kwa mwendokasi usioruhusiwa, kutoka nje ya barabara zilizotengwa pamoja na kuruhusu wageni kuwagusa au kuwachezea wanyamapori.

Imeelezwa kuwa vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha usalama wa watalii wenyewe pamoja na ustawi wa wanyamapori wanaolindwa ndani ya hifadhi.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Catherine Mbena, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana Juni 29, 2026 katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Amesema waongoza watalii wana nafasi kubwa katika kuhakikisha wageni wanaoingia nchini wanafuata sheria za uhifadhi, kwa kuwa wao ndiyo mabalozi wa kwanza wa Tanzania kwa watalii hao.

Amesema wajibu wao ni kutoa elimu sahihi kwa wageni na kuhakikisha taratibu zote za uhifadhi zinafuatwa wakati wote wanapokuwa ndani ya hifadhi.

Amesema kumekuwa na matukio yanayoonyesha baadhi ya wageni wakikiuka taratibu za hifadhi, ikiwemo kuwagusa wanyamapori, jambo ambalo amesema linaweza kuwa hatari kwa binadamu na mnyama.

“Watalii wameanza kuingia kwa wingi katika hifadhi zetu. Tunatoa onyo kwa waongoza watalii kuhakikisha wanazingatia kikamilifu taratibu zote. Kumekuwa na matukio ya baadhi ya wageni kuwagusa wanyamapori, kama kushika masikio au mikia yao.

“Hawa ni wanyama wa porini na wako katika mazingira yao ya asili, hivyo kitendo hicho ni hatari kwa mnyama na kwa mtalii mwenyewe,” amesema Catherine.

Amesema pamoja na kuwepo kwa miongozo ya uendeshaji wa magari ndani ya hifadhi, ikiwemo kuzingatia mwendo unaoruhusiwa na kutotoka nje ya barabara rasmi, bado baadhi ya waongoza watalii wamekuwa wakikiuka maelekezo hayo.

Amesema ni muhimu waongoza watalii kutumia taaluma na mafunzo waliyopewa ili kuhakikisha wageni wanapata uzoefu mzuri wa utalii bila kuhatarisha uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

“Tunawaomba waongoza watalii watumie mafunzo waliyopewa. Tukizingatia sheria kwa pamoja, tutalinda hifadhi zetu na kuhakikisha wageni wanaondoka na taswira nzuri ya Tanzania,” amesema.

Kwa upande wake, mtafiti wa duma, Dennis Minja, amesema matukio ya baadhi ya wageni kuwagusa wanyamapori, ikiwemo video iliyosambaa mitandaoni ikimuonyesha mtalii akimgusa duma, ni hatari kwa usalama wa binadamu na ustawi wa wanyama hao.

Amesema mradi wa Serengeti Cheetah Project ni miongoni mwa tafiti zinazofuatilia maisha ya duma katika ikolojia ya Serengeti na Ngorongoro, unaotekelezwa chini ya Africa Range-Wide Cheetah Conservation Initiative (CCI) kwa ushirikiano na Zoological Society of London (ZSL) na ufadhili wa The Howard Buffett Foundation.

“Mnyama wa porini hawezi kutabirika. Leo anaweza kuwa mtulivu, kesho akageuka hatari. Pia kuna hatari ya maambukizi ya magonjwa kati ya binadamu na wanyamapori,” amesema.

Amesema ongezeko la magari ya utalii limeongeza msongo kwa wanyamapori, hususan duma, hali inayoweza kubadilisha tabia zao za asili kama kuwinda na kulea watoto.

Amesema duma wanapozungukwa na magari mengi au magari yanapotoka nje ya barabara rasmi hupata msongo mkubwa unaoathiri maisha yao ya kila siku.

“Tunapozungumzia duma, tunazungumzia mnyama aliye katika hatari ya kushinikizwa na mazingira mengi. Magari mengi yanapomzunguka au kutoka nje ya barabara rasmi yanamletea msongo na kubadilisha tabia yake ya kawaida,” amesema.

Kwa upande wao, baadhi ya waongoza watalii wamesema changamoto kubwa inatokana na baadhi ya wenzao kutofuata mafunzo na miongozo ya kitaaluma.

Mwongoza watalii, Godson Miti, amesema baadhi ya matukio ya wageni kuvunja taratibu husababishwa na madereva wachache wasiokidhi viwango vya mafunzo ya uhifadhi.

Amesema mtalii anapaswa kupewa maelekezo sahihi kabla ya kuingia mbugani ili kuepuka changamoto zinazoweza kuharibu taswira ya sekta ya utalii nchini.

“Kuna baadhi ya madereva hawafuati kabisa taratibu. Mtalii anapaswa kupewa maelekezo sahihi kabla ya kuingia mbugani. Ukiachia mambo yaende kiholela, unaharibu taswira ya kazi yetu na ya nchi kwa ujumla,” amesema.

Naye Semle Michael amesema wengi wa waongoza watalii wanafanya kazi kwa weledi, lakini wachache wanaokiuka taratibu huathiri taswira ya sekta nzima ya utalii.

Amesema mafunzo yaliyotolewa na Serikali pamoja na wadau wa utalii yamewasaidia kuboresha utendaji wao, lakini bado kuna haja ya kuwepo kwa usimamizi mkali dhidi ya wanaokiuka miongozo hiyo.

Akizungumzia hali ya utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, Catherine amesema idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo inaendelea kuongezeka.

Amesema kati ya Januari hadi Juni 17, 2025, watalii 155,000 walitembelea hifadhi hiyo, huku mwaka huu katika kipindi hicho idadi hiyo imefikia watalii 160,000.

Amesema ongezeko hilo ni sawa na watalii 5,000 zaidi, sawa na asilimia 4.5.

Amesema takwimu zinaonyesha kuwa ongezeko la watalii kwa asilimia 11 linatarajiwa kufikiwa mwishoni mwa mwaka wa fedha kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya utalii wa wanyamapori duniani.