Serikali yataka mfuko mabadiliko ya tabianchi upatiwe ithibati

Muktasari:

  • Waziri Jafo ameutaka Mfuko wa Kimataifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) ukamilishe mchakato wa kupata ithibati ya pili kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc).

Dar es Salaam.  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo ameutaka Mfuko wa Kimataifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund), ukamilishe mchakato wa kupata ithibati ya pili kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc).

Kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira mchakato hupo utaiwezesha Nemc kupata fedha ambazo zitasaidia kwenye shughuli za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) iliyotolewa Desemba 5, 2023 imesema, Waziri Jafo ameyasema hayo katika mkutano wa Mkuu wa Sekretariati ya Mfuko huo, Mikko Ollikainen pamoja na timu yake, ikiwa ni sehemu ya mikutano ya COP28 unaoendelea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UEA)

Dk Jafo amesema, “Nemc ambayo ndiye msimamizi wa fedha za mfuko huo nchini Tanzania ilipatiwa na mchakato wa ithibati kwa takriban miaka miwili sasa hivyo inapaswa ikamilishiwe mchakato huo.”

Vilevile Waziri Jafo ameisisitiza sekretariati ya mfuko huo kuongeza kasi katika kupitia taarifa za mwaka za miradi inayoendelea kutekelezwa, kuzipitisha na kuruhusu fedha za mwaka unaofuata kutolewa.

Mfuko wa dunia wa kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi kupitia bodi ya taasisi hiyo ulipitisha na kusaidia utekelezaji wa miradi miwili kati ya minne iliyowasilishwa NEMC yenye thamani ya dola 2.2 milioni (Sh5.5 bilioni) mwaka 2020.

Miradi hiyo ni pamoja na wa Kukabili Mabadiliko ya Tabia ya Nchi katika Jamii ya Wafugaji na Wakulima Wilaya ya Kongwa na wa Kukabili Mabadiliko ya Tabia ya nchi katika jamii za Pwani ya Zanzibar.

Miradi hiyo iliyoratibiwa na Nemc na kutekelezwa na taasisi zilizoshinda miradi hiyo, ni pamoja na mradi wa Kongwa (FECE) unayoshirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa na mradi wa Zanzibar ni Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

Meneja programu wa ForumCC, Msololo Onditi alisema zipo taratibu mbili za kupata fedha kutoka Mfuko wa dunia wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi ambazo ni ya moja kwa taasisi zilizo na ithibati njia isiyo ya moja kwa moja kwa ambazo hazina ithibati.

“Hapo kilichotokea NEMC ilipata ithibati na kupata fedha kwa awamu ya kwanza na baada ya utekelezaji wanahaki ya kupata tena ithibati, mara nyingine kama umefanya vizuri unaweza kupewa hata mara mbili ya fedha za mwanzo,” amesema.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo, Serikali itaendeelea kuhakikisha taasisi zote zinazoomba usajili katika Mfuko huo zinafanikiwa kupata usajili ili kunufaika na faida zake.

Mbali na ujumbe kutoka Mfuko huo, mkutano umehudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira wa Nemc, Dk Menan Jangu na Fredrick Mulinda pia kutoka Nemc.