Serikali yazindua mradi wa Sh10.5 bilioni kuimarisha usambazaji umeme Kongwa
Kituo cha kubadilisha njia za usambazaji umeme na transifoma ya kudhibiti umeme kilichopo Wilayani Kongwa mkoani Dodoma
Muktasari:
- Mradi huo unalenga kuongeza uhakika wa huduma ya umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda huo.
Dodoma. Serikali imeendelea kuimarisha uwekezaji katika sekta ya nishati kwa kuzindua mradi wa zaidi ya Sh10.5 bilioni wa kuboresha mfumo wa usambazaji wa umeme katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma na maeneo ya jirani.
Mradi huo unalenga kuongeza uhakika wa huduma ya umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda huo.
Akizindua kituo cha kubadilishia njia za usambazaji umeme pamoja na transfoma ya kudhibiti umeme (AVR) katika eneo la Mbande, Wilaya ya Kongwa, leo Jumanne, Juni 16, 2026, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema Serikali imeendelea kuipa sekta ya nishati kipaumbele kutokana na mchango wake katika maendeleo ya viwanda, biashara, uwekezaji na ustawi wa wananchi.
Ndejembi amesema Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati, ukiwamo wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP), miradi ya kuimarisha Gridi ya Taifa na uwekezaji katika nishati jadidifu.
Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi akizungumza katika uzinduzi wa kituo cha kubadilishia njia za usambazaji umeme pamoja na transfoma ya kudhibiti umeme (AVR) katika eneo la Mbande, Wilaya ya Kongwa, Juni 16, 2026.
Hatua hizo zimeongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini kufikia zaidi ya megawati 4,000.
“Upatikanaji wa umeme wa uhakika ni msingi wa maendeleo ya viwanda, biashara, uwekezaji, huduma za kijamii na ustawi wa wananchi. Ndiyo maana Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta hii,” amesema Ndejembi.
Amesema Mkoa wa Dodoma umepewa kipaumbele maalumu katika uwekezaji wa miundombinu ya nishati kutokana na hadhi yake ya kuwa makao makuu ya nchi na kitovu cha shughuli za Serikali.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mradi huo unahusisha ujenzi wa kituo cha kubadilishia njia za usambazaji wa umeme, usimikaji wa transfoma ya kudhibiti umeme yenye uwezo wa MVA 20, pamoja na ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Zuzu hadi Mbande yenye urefu wa kilomita 92.
Amesema mradi huo umeondoa utegemezi wa njia moja ya umeme iliyokuwa ikihudumia Kongwa kutoka Dodoma Mjini, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto za upatikanaji wa umeme wa uhakika kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo.
“Miundombinu hii itaongeza uthabiti wa mfumo wa usambazaji wa umeme, kupunguza athari za hitilafu, kuboresha viwango vya umeme na kuongeza uwezo wa Tanesco kuhudumia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wananchi na wawekezaji,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange amesema mradi huo umetokana na tathmini iliyobaini ongezeko la mahitaji ya umeme kufuatia ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii katika Wilaya ya Kongwa na maeneo ya jirani.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange akizungumza katika uzinduzi wa kituo cha kubadilishia njia za usambazaji umeme pamoja na transfoma ya kudhibiti umeme (AVR) katika eneo la Mbande, Wilaya ya Kongwa, Juni 16, 2026.
Twange amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha huduma ya umeme katika Wilaya za Kongwa, Gairo, Chamwino na baadhi ya maeneo ya Mpwapwa, huku ukiweka mazingira bora kwa uwekezaji, biashara na uzalishaji mali.
“Miundombinu hii imejengwa kwa lengo la kuimarisha uthabiti wa mfumo wa usambazaji wa umeme, kuongeza uhakika wa huduma kwa wananchi na kuweka mazingira bora ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema.
Ameongeza kuwa Tanesco itaendelea kutekeleza miradi mingine ya kimkakati, ikiwemo Mradi wa Chalinze–Dodoma unaolenga kuongeza uwezo wa Gridi ya Taifa na kuboresha usambazaji wa umeme katika Mkoa wa Dodoma na maeneo mengine nchini.
Twange pia ametoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya umeme ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali unaendelea kutoa manufaa yaliyokusudiwa.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wenye Viwanda Wilaya ya Kongwa, Nemes Ritte, amesema wafanyabiashara wameupokea kwa furaha mradi huo kutokana na changamoto za muda mrefu za kukatika kwa umeme na kushuka kwa nguvu ya umeme zilizokuwa zikikwamisha shughuli za uzalishaji.