Sh700 milioni kuinua uchumi wa wananchi, kuokoa vyanzo vya maji
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli akizungumza mkakati wa kuwekeza wananchi unaotekelezwa na Bonde la Rufiji kupitia mradi wa NBS-USANGU. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Fedha hizo zimetolewa na Taasisi ya Bonde la Mto Rufiji kupitia mradi wa NBS – Usangu, unaotekelezwa wilayani humo.
Mbarali. Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, imepokea Sh700 milioni kwa ajili ya kuviwezesha kiuchumi vikundi 30 vya wananchi ili kupisha shughuli za kijamii kwenye maeneo ya hifadhi za mito na vyanzo vya maji.
Fedha hizo zimetolewa na Taasisi ya Bonde la Mto Rufiji kupitia mradi wa NBS – Usangu, unaotekelezwa wilayani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli ameliambia Mwananchi leo Jumapili Juni 14, 2026 kuwa lengo ni kuwasaidia wananchi kujijengea uchumi imara huku wakishiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mito, vyanzo vya maji na maeneo mengine nyeti ya mazingira.
Amesema mradi huo unalenga kubadilisha maisha ya wananchi kwa kuwapatia fursa mbadala za kujipatia kipato badala ya kuendelea kufanya shughuli ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa.
“Kupitia Taasisi ya Bonde la Mto Rufiji, Sh700 milioni zitawanufaisha wananchi kwa kuwawezesha kuanzisha miradi ya biashara, kilimo na shughuli nyingine za uzalishaji mali ambazo zitawapa uhuru wa kiuchumi,” amesema Mweli.
Amesema pamoja na kuinua kipato cha wananchi, mradi huo utasaidia kuondoa shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi za mito na vyanzo vya maji, hivyo kuyarejesha katika hali yake ya asili na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mweli amesema halmashauri imepewa jukumu la kusimamia na kufuatilia vikundi vyote vitakavyonufaika ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na miradi inayotekelezwa inakuwa endelevu.
“Tutawatumia watendaji wa kata, madiwani na wataalamu wetu kuhakikisha vikundi vinasimamiwa ipasavyo, vinapata ushauri wa kitaalamu na vinaendelea kustawi kiuchumi huku vikiheshimu masharti ya uhifadhi wa mazingira,” amesema.
Aidha, amesema halmashauri itaunganisha vikundi hivyo na fursa nyingine za mikopo ya asilimia 10 ili kuviwezesha kupanua shughuli zao za uzalishaji na kuongeza mchango katika uchumi wa wilaya na Taifa.
Mweli amesema uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ni sehemu ya mkakati wa halmashauri wa kutekeleza maelekezo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga jamii yenye uchumi imara unaokwenda sambamba na matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira.
Matumaini ya wananchi
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Madaba wilayani humo, wameeleza kuwa mradi huo utakuwa suluhisho la changamoto kiuchumi na kuwasaidia kuachana na shughuli zilizo kuwa zikifanyika ndani ya maeneo ya hifadhi.
“Serikali imetupatia mbadala wa kujipatia kipato kupitia fedha hizi tutalinda mazingira kwa wivu mkubwa na kuboresha kipato cha maisha ya familia zetu,” amesema.