Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh991.5 milioni zakopeshwa vikundi vya Wanawake, Kibaha

Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo leo Jumatano Juni 10, 2026 iliyofanyika mjini Kibaha. Picha na Sanjito. Msafiri

Muktasari:

  • Mikopo hiyo ni mtaji wa kuwawezesha wananchi kuboresha maisha yao, kuongeza uzalishaji na kupanua shughuli za biashara.

Kibaha.Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani imetoa mikopo yenye thamani ya Sh991.5 milioni kwa vikundi 51 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.

Akizungumza leo Jumatano, Juni 10, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo hiyo, Mbunge wa Kibaha Mjini, Sylvestry Koka amewataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili ziwe chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwao na kwa jamii kwa ujumla.

Amesema mikopo hiyo ni mtaji wa kuwawezesha wananchi kuboresha maisha yao, kuongeza uzalishaji na kupanua shughuli za biashara.

“Fedha hizi si za matumizi ya kawaida, ni mtaji wa kujenga maisha bora. Zitumikeni kwa nidhamu, ongezeni uzalishaji, panua biashara zenu na mrejeshe kwa wakati ili wananchi wengine wapate fursa kama mlivyozipata nyinyi,” amesema Koka.

Aidha, amebainisha kuwa urejeshaji wa mikopo kwa wakati utaiwezesha Manispaa ya Kibaha kuwanufaisha wananchi wengine zaidi kupitia mpango huo, hivyo kuongeza idadi ya wanufaika kila mwaka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk Rogers Shemwelekwa amesema mikopo hiyo ni ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha na imetokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

Amesema lengo la utoaji wa mikopo hiyo ni kuendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi na kukuza shughuli za uzalishaji katika manispaa hiyo.

“Tunaendelea kutenga fedha kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha makundi maalumu yanapata mitaji ya kuanzisha au kukuza biashara zao. Pia tunaendelea kusimamia kwa karibu vikundi hivi ili kuhakikisha fedha zinatumika kama ilivyokusudiwa,” amesema Dk Shemwelekwa.

Ameongeza kuwa mafanikio ya wanufaika yatakuwa mafanikio ya Manispaa ya Kibaha na wananchi wake kwa ujumla.

Mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo, Adelina Mgonja, amesema mikopo ya halmashauri imewawezesha kuongeza mtaji wa biashara zao na kuboresha kipato cha familia.

“Tunashukuru Serikali na Manispaa ya Kibaha kwa kutuamini. Kupitia mikopo hii tumepanua biashara zetu na baadhi yetu tumeweza kuajiri watu wengine, jambo ambalo linachangia kupunguza ukosefu wa ajira,” amesema.

Naye Salome Mwenda amesema mikopo hiyo imekuwa kichocheo cha maendeleo kwa wanawake wengi waliokuwa wanakabiliwa na changamoto ya mtaji wa kuendesha shughuli zao za uzalishaji.