Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Si sukari tu, hata viazi, vitunguu havishikiki

Dar es Salaam. Kama ulidhani kupaa kwa bei ya bidhaa kumeishia kwenye sukari pekee mambo ni tofauti, hali hiyo imebainika hata katika viazi mbatata, vitunguu na pilipili hoho.

Kuongezeka kwa bei ya bidhaa hizo, kunazusha hofu kwa waumini wa dini ya Kiislamu ambao Machi 10 au 11, mwaka huu wanatarajia kuanza ibada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Mbali ya hao, waumini wa Kikristo wako katika mfungo wa Kwaresima.

Bidhaa za nafaka na sukari, ndizo hasa zinazotumika zaidi katika maandalizi ya futari kwa waumini hao.


Hali ilivyo mtaani

Kwa upande wa sukari, kwa mujibu wa wakazi wa baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, kilo moja inauzwa kati ya Sh4,500 hadi Sh5,000, huku Arusha hali ikiwa mbaya zaidi, kilo moja ya bidhaa hiyo inapatikana kwa Sh5,000 hadi Sh6,000.

Bei hizo za sukari zinaendelea kipindi ambacho zimepita takriban wiki mbili tangu Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), itangaze bei elekezi ya kuanzia Sh2,800 na isizidi Sh3,200.

Uamuzi wa kutangaza bei hiyo elekezi, ulitanguliwa na kutolewa vibali vya uagizaji wa tani 50,000 za sukari nje ya nchi na tayari imeshaanza kuingia na kusambazwa, lakini hali imebaki kuwa tete.

Matumaini pekee kuhusu kushuka kwa bei ya sukari yamebaki kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo, ambavyo baadhi vimeanza uzalishaji bila kueleza kiwango sahihi.

Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Kilombero Sugar inayozalisha Bwana Sukari, Derick Stanley alisema kiwanda hicho kinaendelea na uzalishaji kwa sasa, isipokuwa si kwa kiwango kilichokuwa kinazalisha awali.

Stanley aliweka wazi kuwa, uwezo halisi wa kiwanda hicho ni kuzalisha kati ya tani 600 hadi tani 700 kwa siku, lakini kwa sasa kinazalisha pungufu zaidi.

“Kwa sasa tunazalisha kidogo mno kutokana na hali ya mvua za El-Nino. Kimsingi tunasuasua lakini hatujasitisha uzalishaji,” alisema Derick.

Kwa upande wa kiwanda cha Bagamoyo Sugar chenye uwezo wa kuzalisha tani 160 kwa siku, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Bakhresa Group inayomiliki kiwanda hicho, Hussein Sufiani alisema wameanza kuzalisha ingawa kwa kiwango kidogo.

“Tunaendelea na uzalishaji lakini kwa kiwango kidogo sana, hatuwezi kusema ni kiasi gani kwa sababu kinatofautiana siku hadi siku kutokana na hali inavyokuwa,” alisema.

Sufiani alisema kinachoamua uzalishaji zaidi ni kutengemaa kwa hali, akimaanisha mvua zitakapokata.


Mbogamboga, viazi

Gunia moja la vitunguu lililokuwa linauzwa kwa Sh250,000 hadi Sh300,000 kwa sasa linapatikana kwa Sh500,000 hadi Sh550,000 katika Soko la Mabibo, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa madalali wa vitunguu na viazi katika soko hilo, Maulid Ally alisema hali si mbaya sana kwa upande wa viazi mbatata.

Alisema gunia moja linapatikana kwa Sh70,000, kukiwa na ongezeko la Sh10,000 kutoka bei ya awali ya Sh60,000.

“Ndoo moja ya viazi hivyo (mbatata) inauzwa kati ya Sh15,000 hadi Sh20,000, zamani iliuzwa Sh13,000,” alisema Ally.

Mudy Ngoma, mfanyabiashara sokoni hapo alisema bei ya pilipili hoho haikamatiki, kiroba kilichokuwa kinauzwa Sh80,000 kwa sasa kinauzwa kati ya Sh250,000 hadi Sh280,000.

Ngoma, anayeuza bidhaa hiyo alisema ahueni ipo kwenye karoti na nyanya ambazo zimeshuka bei.

Alisema kiroba kidogo cha karoti kinauzwa Sh45,000 hadi Sh50,000 ilhali awali kiliuzwa Sh100,000, huku tenga la nyanya linauzwa Sh50,000 kutoka Sh60,000.

Ngoma alisema kupanda bei kwa baadhi ya bidhaa hizo kumetokana na kuadimika kwake sokoni, hivyo wafanyabiashara wanauza bei wanayotaka.


Ilivyo Buguruni

Katika Soko la Buguruni, Katibu wa wafanyabiashara, Juma Kizuki alisema kumekuwa na bei zisizoridhisha kwa bidhaa za mizizi tangu ilipoanza Februari mwaka huu.

“Kwa mihogo tumepokea gari nane wakati kwa kawaida huwa tunapokea gari 24 hadi 25 na kiroba kimoja kinauzwa Sh150,000 kutoka Sh70,000 za awali,” alisema Kizuki.

Kwa upande wa viazi vitamu, alisema kiroba kinauzwa Sh150,000 hadi Sh160,000 badala ya Sh54,000 iliyokuwa inauzwa awali.

Bei ya njegere nayo imepanda katika soko la Buguruni, Kizuki alisema kilo moja iliyokuwa inauzwa Sh5,000 hadi Sh6,000 kwa sasa inauzwa Sh9,000 hadi Sh10,000.

Alisema kwa njegere ambazo hazikumenywa kilo moja ni Sh5,000 kutoka Sh3,000 hadi Sh2,500 iliyokuwa inauzwa awali.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na bei zisizotabirika kwa nyanya chungu na bamia, kwa kuwa ni mazao ya bustani.

Kizuki alisema kiroba cha nyanya chungu jana kiliuzwa Sh90,000, ikiongezeka kutoka Sh60,000 iliyouzwa siku tatu zilizopita.

Alisema gunia linalohusisha kabichi 70, limepanda hadi Sh350,000 kutoka Sh150,000 bei iliyokuwepo awali, huku kabichi moja kwa sasa inauzwa Sh2,500 hadi Sh3,000 kutoka Sh500 hadi Sh1,000 ya awali.

Kuhusu ongezeko la bei, Kizuki alisema limesababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha zilizokwamisha uzalishaji na wakati mwingine kuozesha mazao kabla hayajafika sokoni.


Ahueni katika nafaka

Wakati mbogamboga zikishuhudiwa kupanda, hali ni shwari kwa bidhaa za nafaka.

Mwenyekiti wa soko la Tandale, Juma Dikwe alisema gunia la mahindi limeshuka bei kutoka Sh90,000 miezi mitatu iliyopita hadi Sh60,000, huku kilo ikiuzwa Sh600 kutoka Sh900.

“Maharagwe yameshuka kutoka Sh350,000 kwa gunia moja hadi Sh250,000, huku kilo ikitoka kuuzwa Sh3,500 hadi Sh2,500,” alisema Dikwe.

Kwa upande wa mchele, alisema gunia lililokuwa linauzwa Sh400,000 sasa linauzwa Sh300,000 kwa ule wa daraja la kwanza, huku kilo iliyokuwa ikiuzwa Sh4,000 sasa ni Sh3,000.

“Mchele wa daraja la chini kabisa kwa sasa gunia ni Sh200,000 na kilo ikiwa Sh2,000,” alisema mwenyekiti huyo.

Kushuka kwa bei ya bidhaa za nafaka, alisema kunatokana na wingi wa upatikanaji wake uliosababishwa na mavuno makubwa kutoka kwa wakulima.

Dikwe alieleza kwa sasa sokoni hapo wanapokea magari kati ya 100 hadi 200 kwa siku kutoka mikoa mbalimbali yanayoleta nafaka, tofauti na awali magari takribani 50 tu ndiyo yaliyokuwa yanafika.

Alisema kuna matarajio ya bei ya mahindi kushuka zaidi kwa kuwa wiki hii nafaka mpya kutoka Tanga inatarajiwa kuingia.

Kutokana na bei hizo, Radhia Abdallah, mkazi wa Gongo la Mboto, Dar es Salaam alisema hali hiyo inaongeza gharama za maisha.

Alisema ni vyema Serikali iangalie sababu za kupanda kwa bei ya bidhaa hizo ili itatue changamoto zilizopo na kufanya mazao yasalie kuwa na bei himilivu kulingana na maisha ya wananchi.

Mkazi wa Tandale, Othuman Chipaka alionyesha hofu ya kuwepo mazingira magumu ya upatikanaji wa futari katika mwezi wa Ramadhan kutokana na kuongezeka kwa bei ya bidhaa za mizizi.

Mkazi wa Tabata, Benard Alphonce alisema bado kuna umuhimu wa kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza bei ya mafuta yanayosababisha kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa bidhaa hizo.

“Pamoja na kwamba bei katika kipindi cha miezi mitatu mfululizo ilishuka, lakini Serikali iangalie namna ya kuhakikisha bei ya mafuta inashuka zaidi ili itupe unafuu wa bei ya bidhaa sisi wananchi,” alisema Alphonce.