Sukari yauzwa kama bangi mtaani

Muuza duka akipima sukari kwa kutumia mizani.

Dar/mikoani. Sukari sasa imeanza kuuzwa kwa mfumo kama wa biashara haramu katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni siku ya saba tangu Serikali ilipotangaza bei elekezi ya bidhaa hiyo.

Waandishi wa Mwananchi wamebaini baadhi ya maduka yanauza bidhaa hiyo kati ya Sh4,000 hadi 5,000 kwa kilo kwa wateja wanaowafahamu na endapo hujulikani utaambiwa sukari hakuna kwa kuhofia maofisa wa Serikali wanaoendelea na msako kwa maduka yasiyozingatia bei elekezi ya Sh2,700 hadi Sh3,200.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini pia baadhi ya maduka makubwa ya bidhaa yaliyopo maeneo ya Masaki, Kinondoni, Namanga na Mwenge, jijini Dar es Salaam hayauzi bidhaa hiyo kwa sasa.

Hali imekuwa mbaya zaidi kwani baadhi ya wafanyabiashara wameachana na utamaduni wa kuuza sukari kwa vipimo vya kibaba na vijiko, hatua iliyoibua kilio kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam pamoja na mikoa mbalimbali ya Mwanza, Kagera, Manyara, Singida, Kilimanjaro, Kagera na Kigoma.

Hatua hiyo imewafanya wananchi kwenye mikoa minane iliyofikiwa na gazeti hili kuendelea na maumivu ya bei pamoja na uhaba wa bidhaa hiyo, licha ya Waziri Kilimo, Hussein Bashe kuwaonya wafanyabiashara wanaokiuka agizo hilo lililotakiwa kuanza kutumika Januari 23, 2024 kabla ya kufikia ukomo Juni 30, mwaka huu.

Baadhi ya wafanyabiashara walishauri kutazama kiini cha sakata hilo kwa umakini na kutoa msimamo bila kuathiri upande wowote kwa wananchi wa kawaida pamoja na maslahi ya wafanyabiashara.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli aliliambia gazeti hili jana kuwa bado ukaguzi unaendelea mikoa yote kuhakikisha inadhibiti wafanyabiashara wanaouza kinyume na bei elekezi ya Serikali.

“Tunaendelea na ukaguzi kwa kasi kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za mikoa ambazo ziko kazini hadi sasa,” alisema Mweli huku akidai kuendelea na upakuaji wa sukari bandarini kwa ajili ya kuisambaza sokoni. Mweli alidai kutokuwa na taarifa za kina kuhusu upakuaji huo bandarini.

Awali, Bashe aliwahakikishia Watanzania hadi kufikia Februari 15, mwaka huu changamoto ya upatikanaji wa sukari nchini itakuwa imepungua huku Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya mwenendo wa uzalishaji nchini ulioathiriwa kwa asilimia 30.

Uzoefu unaonyesha, hali ya upungufu wa sukari nchini umewahi kutokea mara kadhaa ikiwamo mwaka 2018 hadi 2019 kabla ya Serikali kuchukua hatua kama hizo, ili kukabiliana na changamoto hiyo.


Hali ilivyo

Hadi jana mchana, sukari iliuzwa wastani wa Sh5,000 Kibaha kwa Mfipa, mkoani Pwani, Sh4,600 Mabibo kwa Ustaazi, Sh4,500 Mbezi Luis, Sh4,800 Mbezi Hai kwa Mgalura (Dar es Salaam) na Sh4,400 eneo la Mlandege Magengeni, iliyopo Wilaya ya Mkurunga, mkoani Pwani.

Kwa mikoa ya kanda ya kati bei ni Sh2,800 hadi Sh3,000 kwa kilo moja, bado wakazi wa Dodoma wananunua kwa wastani wa Sh4,200. Kanda hiyo inahusisha mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora.

Mfanyabiashara wa duka, Emmanuel Edwin alisema hawezi kuuza kwa bei elekezi kutokana na mfuko wa kilo 25 kuuzwa kwa Sh95,000 na kiroba cha kilo 50 kwa Sh186,000. “Tusaidieni hii habari ili sukari ianze kupatikana, kwanza sukari haipatikani na ikipatikana bei yake ni kubwa kwa magendo,” alisema.

Mkoani Mbeya, bei ya sukari kwa mjini inauzwa wastani wa Sh4,000 na vijijini Sh4,500 huku wafanyabiashara wa rejareja wakidai bei hizo kuathiriwa na bei wanayochukulia katika duka la jumla.

Mfanyabiashara Rukia Mwakifuna alisema licha ya Serikali kutoa bei elekezi wameshindwa kushusha huku mfanyabiashara wa jumla, Alex Mwaipopo akishauri Serikali kudhibiti bei ya bidhaa hiyo kuanzia viwandani inakotoka kabla ya kudhibiti wanaosambaza mitaani.

Katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wananchi jana walidai kuendelea na maumivu kwa kununua sukari kwa Sh6,000 kwa kilo, bila kuzingatiwa bei elekezi katika kanda ya kaskazini ambayo ni kati ya Sh2,700 hadi Sh3,000.

Maumivu ya bei ya bidhaa hiyo pia yameonekana kwa mikoa ya Kigoma na Singida huku wafanyabiashara wakiendelea kuitupia lawama Serikali kwenye bei elekezi.

Mfanyabiashara Elia Digha alidai kununua kiroba cha kilo 25 kwa Sh92,500 bila kuhusisha gharama za Sh1,000 ili kusafirisha hadi dukani kwake.

“Kwa hesabu hiyo ukigawanya kwa thamani ya kilo moja ni sawa na Sh3,700 kwa kilo, bei itakayonilazimu kuuza zaidi ya hapo ili nipate faida,” alisema.

Hata hivyo, wakala wa usambazaji sukari mkoani Singida, Karim Nagji alisema haoni sababu ya wafanyabiashara kupandisha bei. Alisema kiroba cha kilo 50 anauza Sh140,000.

Kwa upande wa Mkoa wa Kigoma, bei ya sukari katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ni kati ya 3,500 hadi 4,000 na wafanyabiashara wanasema bei hiyo ni kutokana na bidhaa hiyo kununua kwa bei ya juu na kuwalazimu kuongeza bei hiyo. Mfanyabishara wa sukari, Rashid Salim alisema ananunua sukari kwa Sh80,000 kilo 25 kwa jumla, hivyo lazima aongeze bei kwenye kuuza ili apate faida.

Mkazi wa Mwasenga, Christina James alishauri Serikali kusimamia bei hiyo ili kumsaidia mwanachi wa kawaida.


Kagera, Mwanza

Mkoani Mwanza, sukari inauzwa kwa wastani wa Sh4,000 kwa kilo kutokana na sababu za kuathiriwa na bei wanayonunulia kama ilivyoelezwa katika mikoa ya Dodoma, Tanga, Singida na Manyara.

Mkazi wa Igogo, mkoani Mwanza, Ester Daniel alisema hatua hiyo imesababisha wafanyabiashara waliokuwa wakiuza sukari kwa kibaba kuacha kwa madai ya kupata hasara.

Alisema hali imezidi kuwa ngumu zaidi kwa wananchi wengi wanaotegemea vipimo hivyo.

“Wakati sukari ikiuzwa Sh3,000, tusiokuwa na uwezo kifedha tulinunua kipimo cha Sh500 badala ya kununua robo Sh750, lakini tangu bei ipande hakuna sukari ya Sh500 tena, kipimo cha mwisho ni robo,” alisema.

Mkazi wa Bulale jijini Mwanza, Msafiri Haruna alisema baadhi ya wakazi wameamua kutokunywa chai huku Hanipha Jonsin akiiomba Serikali kutotumia nguvu kubwa kwa wafanyabiashara wadogo, badala yake iangalie tatizo la msingi kwenye sakata hilo.

Kwa upande wa Kagera, bei ya sukari ni kati ya Sh4,000 hadi 4,300 huku baadhi ya wananchi wakiendelea kulia maumivu ya bei hiyo kwa zaidi ya wiki mbili sasa.


Imeandaliwa na Kelvin Matandiko (Dar), Rajabu Athumani (Tanga), Jamaldini Abuu (Singida), Joseph Lyimo (Manyara), Florah Temba (Moshi).