Wadau waanika mbinu udhibiti, upatikanaji sukari Tanzania

Muktasari:

  • Udhibiti mdogo wa mawakala wa usambazaji sukari na uwiano usio sawa wa uzalishaji na mahitaji, vimetajwa kuwa chanzo cha kuadimika na upandaji holela wa bei ya bidhaa hiyo nchini.

Dar es Salaam. Udhibiti usiokidhi wa mawakala wa kusambaza sukari na kutokuwepo uwiano sahihi wa uzalishaji na mahitaji, ni miongoni mwa vyanzo vya kuadimika na upandaji holela wa bei ya bidhaa hiyo.

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Januari 24, 2024 na Mhariri wa Jarida la Uchumi wa Gazeti la Mwananchi, Ephrahim Bahemu wakati akichokoza mada katika Mwananchi X-Space iliyokuwa inajadili mada isemayo ‘Lipi Suluhisho la Kudumu uhaba wa sukari nchini.’

Amesema kuna mawakala ambao huenda hawazidi 10 ambao wanauza sukari yote nchini, hivyo kuna haja ya Serikali kukaa nao au kuweka utaratibu utakaowabana kushughulikia tatizo la upandaji wa bei.

“Lakini katika suala la kudhibiti uhaba na bei kuwa kubwa ni vyema kuongeza uzalishaji zaidi ya kile tunachokitumia ili inapotokea kuna upungufu kidogo, usiathiri matumizi yetu ya ndani,” amesema Bahemu.

Akitolea mfano, amesema kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo sasa hivi hapa nchini zinatumika tani 1,500 za sukari kwa siku, hivyo kukiwa na uwezo wa kuzalisha tani 3,000, hata ukitokea upungufu hauwezi kufika tani 1,500.

Cosmas Makune, mchangiaji wa mada hiyo amesema haitatokea hata siku moja bei ya sukari ikashuka, kwa sasa watawaambia hakuna tatizo lakini bei haitashuka kama ambavyo bodi ya sukari Tanzania imeelekeza isiuzwe zaidi ya Sh3,200.

“Ni njama kutoka viwanda vya uzalishaji kwenda kwa watumiaji mwisho, ili kudhibiti suala hili ni lazima tuwe na viwanda vingi vya wazawa kuliko viwanda ambavyo vimewekezwa na kampuni za kimataifa,” amesema Makune.

Naye Josephat Masanja, mshiriki wa mjadala huo amesema sukari kutumika kwa wingi majumbani kama kutengeneza chapati na  maandazi, hivyo kupanda kwake bei kunaongeza gharama za maisha kwa wakazi wengi.

“Ukiona kelele unajua kuwa umegusa kundi kubwa la watu, ambalo lilikuwa linapata riziki yake,” amesema Masanja.

Hata hivyo, amesema Serikali imeonyesha jitihada za kupunguza tatizo, akisema miaka mitano nyuma kulikuwa na upungufu mkubwa na uhaba ulifikia tani 50,000 kutoka tani 250,000 ya miaka mitano nyuma.

Amesema tatizo lililopo katika upatikanaji wa bidhaa hiyo ni ustawi katika uzalishaji wa miwa inayotumika kuzalishaji sukari na kuwa suala la uzalishaji litaisha endapo jitihada zitafanyika kuongeza idadi ya wawekezaji kama Bakhresa.

Takwimu zimasemaje?

Kwa upande wake, Mhariri wa Takwimu Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Halili Letea ameelezea viwanda vinavyozalisha sukari nchini ambavyo ni saba, sita vikiwa vikubwa na kimoja ni kidogo kilichopo Manyara.

Amesema ukijumuisha uzalishaji unaofanywa kwa sasa na viwanda vyote ni takribani tani 700 badala ya tani 1,500 zinayzohitajika kwa siku, hivyo uzalishaji unakuwa chini ya nusu ya mahitaji na hapo ndipo uhaba unapotokea.

Kwa kuwa matumizi ya sukari kwa mwaka kwa mujibu wa wizara ni tani 490,000 hadi tani 500,000, waziri wa kilimo amesema mwaka 2023 tani 460,000 zilizalishwa, sawa na asilimia 94 ya mahitaji.

“Tulikuwa na upungufu wa asilimia 6 sawa na tani 30,000 kikiwa ni kiwango kidogo cha upungufu ambacho kimewahi kufikiwa na Tanzania,  kwa sababu miaka mitatu nyuma upungufu ulikuwa unaweza kufikia hadi tani 200,000, hivyo inaonyesha kwa namna gani pengo limepunguzwa lakini mvua nazo zimekuja kuharibu,” amesema Halili.

Wasemavyo wachumi

Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi, Oscar Mkude amesema linapotengenezwa pengo linazilazimu mamlaka husika kuanza kusimamia upatikanaji wa sukari na ndiyo maana kukawa na utoaji ruzuku kwa wazalishaji na waingizaji wa sukari, kutoa tozo za uingizaji wa sukari na kutolewa vibali maalumu.

“Hivi vyote vinatatua tatizo la sukari kwa kipindi kifupi, pia uwepo wa ahueni hizi zenyewe ni tatizo, ukimwambia mtu nitakupa ruzuku fulani, nitakupa kitu fulani ni mazingira ya kutengeneza mtu anavyoweza kupata kipato,” amesema Mkude.

Pia, amesema kukosekana kwa sukari ni sehemu za watu kujipatia kipato kutokana na mazingira hayo, kwani yanafanya wao wanufaike kupitia uhaba huo.

Amesema kwa sababu wananufaika, hivyo kutakuwa na namna ya kutengeza uhaba mara kwa mara ili ile fedha zinazopatakana ziendelee kuwepo na wakati mwingine hata rushwa inatengenezeka hapo.

“Wanaoshiriki katika uagizaji wa sukari ni kundi la watu wachache, wanapokuwa wachache uhaba unakuwa ni tatizo kwa walaji na watu wanapokuwa na nguvu ya fedha hawapendi kuipoteza kirahisi, wanaitunza, hali hii inafanya watengeneze uhaba usiokuwa wa kawaida,”amesema.

Mtaalamu mwingine wa Uchumi, Kiama Mwaimu amesema sukari ni moja vitu vinavyotumika kwa watu wa kawaida na wengine wanaitumia kama chanzo cha kupata kipato chao.

“Unapopanga bei unaharibu mfumo mzima wa kujipatia kipato kwa watu walio wengi, katika mtazamo huo hata shughuli za uchumi kwa nchi zinapungua,” amesema Kiama.