Serikali yatangaza bei kikomo ya sukari, wafanyabiashara wang’aka

Muktasari:

 Baadhi ya wafanyabiashara wamelalamikia bei kikomo ya sukari ya Sh3, 200 iliyotangazwa na Serikali wakisema haiendani na bei wanayonunulia

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitangaza bei elekezi ya uuzaji wa sukari kwa rejareja na jumla nchini isiyozidi Sh3, 200 kwa kilo, baadhi ya wafanyabiashara wamesema bei hiyo haiendani na bei ya kununua, hivyo itawanyonga kibiashara.

Bei hiyo inatangazwa ikiwa zimebaki siku chache tangu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuahidi kuwa kuanzia Februari mwaka huu bei hiyo itaimarika.

Tangazo lililotolewa jana Januari 23, 2024 na Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari  Tanzania (SBT), Profesa Keneth Bengesi, limesema bei hiyo isiyozidi Sh3,200 kwa kilo imeanza kutumika jana na itakoma Juni  30, 2024.

 Kwa mujibu wa taarifa ya SBT, mikoa yote itatakiwa kufuata bei elekezi iliyotolewa na huku uzingatiaji wa amri hiyo ukitarajiwa kusimamiwa.

"Bei elekezi zilizoainishwa katika amri hii zitafanyiwa mapitio na bodi mara kwa mara kadri ya mahitaji," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, kilo moja ya sukari katika mikoa ya nanda za juu kusini inayojumuisha mikoa Iringa, Mbeya, Songwe na Njombe itauzwa kati ya Sh2,700 hadi Sh3, 000 na Sh2,600 hadi Sh2,800 kwa jumla.

Kanda ya Mashariki inayounganisha mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani kilo moja itauzwa kwa kati ya Sh2,700 hadi Sh3,000 huku bei ya jumla ikiwa kati ya Sh2,600 na 2,800.

Kanda ya kati inayobeba na mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora bei ya jumla kwa kilo moja itakuwa Sh2,650 hadi Sh2, 800 huku bei ya rejareja ikiwa kati ya Sh2, 800 hadi Sh3, 000.

Kanda ya Kusini (Lindi Mtwara na Ruvuma) bei ya jumla itakuwa kati ya Sh2,650 hadi Sh2,900 huku rejareja ikiwa Sh2,900 hadi Sh3,200.

Kanda ya ziwa inayobebea na mikoa ya Mwanza Geita Shinyanga Simiyu na Mara bei ya rejareja itakuwa Sh2,800 hadi Sh3, 000 huku bei ya jumla ikiwa kati ya Sh2,650 hadi Sh2,800.

Kanda ya kaskazini yenye mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara bei ya jumla itakuwa kati ya Sh2, 600 hadi Sh2,800 huku rejareja ikiwa kati ya Sh2,700 hadi Sh3,000.

Kanda ya magharibi inayobebwa na mikoa ya Kagera, Kigoma, Katavi na Rukwa sukari kilo moja bei ya rejareja itauzwa kwa Sh2,800 hadi Sh3,200 huku bei ya jumla ikiwa kati ya Sh2,600 hadi Sh2,900.

Tangazo hili linatolewa ikiwa ni siku chache tangu Bodi ya Sukari kutangaza kuwakamata wafanyabiashara zaidi ya 40 katika maeneo tofauti nchini kwa madai ya kupadisha bei ya sukari kiholela.

Awali, msako huo ulifanyika baada ya Profesa Bengesi wa SBT kueleza kuwa wamebaini kuwapo kwa wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu wanaotumia mwanya wa uhaba wa sukari kujipatia kipato licha ya kuwa wanaipata nchini kwa bei ya kawaida.

Wafanyabiashara wang’aka

Wafanyabiashara wa rejareja waliozungumza na Mwananchi Digital wamepinga suala hilo huku wakieleza kuwa, upangaji wa bei haujazingatia mahitaji na upatikanaji wa bidhaa husika.

Mfanyabiashara Meshack Kizenzye amesema anafikiria kuacha kuuza sukari kwa muda hadi pale hali itakapokuwa sawa.

"Hili suala ni gumu kutekelezeka, sasa hebu fikiria sukari mfuko wa kilo 25 bei yake ni kati ya Sh95,000 hadi Sh100, 000 hapa Dar es Salaam.

“Hii ni sawa na kilo moja kwa Sh3,800 hadi Sh4,000 halafu eti bei elekezi ni Sh2,800 hadi Sh3, 000," amesema Kizenzye.

Amesema ikiwa jitihada za makusudi hazitafanyika, hali hiyo itaendelea kuumiza wananchi badala ya kuwasaidia kuondokana na tatizo hilo.

Martha Njau ni mfanyabiashara anayekiri kuwa mmoja wa wafanyakazi wake amekamatwa kwa kuuza sukari Sh4,500 kwa kilo moja.

"Bei ya jumla tu sukari imepanda, unanunua hadi Sh4,000 kwa bei ya jumla wewe utauza shilingi ngapi na nipate nini? Hii biashara itatushinda," amesema Martha.

Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude ameshauri kuangaliwa namna bei hizo zinavyopangwa kwa kuzingatia bei za ununuaji wa sukari katika masoko ya nje na ile inayozalisha ndani.

"Kama Serikali inajua bei ya sukari inavyouzwa nje ya nchi, bei kikomo itakuwa na maana kama hawajui bei ikoje nje na kuweka bei kikomo inaweza kuwaumiza waingizaji,  itawafanya washindwe kuingiza," amesema Mkude.

"Kama bei ikipangwa bei wakati ambao waingizaji wameshaleta bidhaa kwa kujua bei waliyonunulia na gharama walizotozwa inaweza kuwa na maana lakini kama utawekwa tu haitakuwa na maana," amesema Mkude.

Akitolea mfano wa upangaji wa bei kikomo za mafuta, amesema huwa unafanyika wakati ambao bidhaa imeshaingia nchini na kujua gharama halisi zilizotumika.

"Kama hatutazingatia haya, hatutazingatia mtu aliyeingiza sukari kanunuaje na gharama alizotumia, tukataka kuweka bei kikomo sawa na ile iliyozalishwa nchini tunaweza kutengeneza masoko haramu,” amesema.