Serikali yakamata tani 40 za sukari iliyofichwa

Baadhi ya shehena ya sukari iliyokutwa kwenye ghala Mtwara mjini. Florence Sanawa.

Muktasari:

  • Wanatuhumiwa kuficha zaidi ya tani 40 za sukari na kuuza bidhaa hiyo bei ya juu tofauti na iliyoelekezwa na Serikali.

Mtwara. Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Mtwara linawashikilia wafanyabiashara watatu wanaotuhumiwa kuficha zaidi ya tani 40 za sukari na kuuza bidhaa hiyo bei ya juu tofauti na elekezi ya Serikali.

 Akizungumza wakati wa msako Mtwara mjini, Mkuu wa Tehama wa SBT, Faustine Mgimba amesema wamebaini uwepo wa sukari iliyofichwa ndani ya mji huo.

Amesema kufichwa kwa sukari kumesababisha bidhaa hiyo kuuzwa bei kubwa, mlaji wa mwisho akinunua kati ya Sh Sh5,000 na Sh5,500 kwa kilo licha ya kiwandani kuuzwa kati ya Sh2,230 na Sh2,270.

“Tumebaini sukari iliyofichwa zaidi ya tani 40, tunachukua hatua kwa kuwakamata wafanyabishara wote ambao wanapandisha bei kiholela kwa nia ya kujinufaisha,” amesema.

Amesema agizo ni kwamba sukari iuzwe kwa bei elekezi ya Serikali ya Sh2,700 hadi Sh3,000.

“Zaidi ya hapo tutachukua hatua kwa atakayekiuka. Huu ni mchezo mchafu, wafanyabishara wanapaswa waache mara moja,” ameagiza.

Amesema sukari ipo mkoani Mtwara licha ya uzalishaji kushuka nchini, lakini haisababisha kupanda bei kwa kuwa hata viwandani haijapanda.

Kuanzia Januari 24, 2024 amesema sukari itaanza kuingia nchini kutoka nje.

Mulichi Yusuph, mfanyabiashara wa sukari kwa bei ya jumla mjini Mtwara, ambaye anatuhumiwa kuficha bidhaa hiyo, amesema uhaba wa bidhaa hiyo umetokana na Serikali.

“Serikali inatakiwa kutoa vibali mapema ili sukari iletwe kwa wingi si kusubiri watu wahangaike, bei ipande ndipo iagizwe. Hata sisi tunauziwa kwa bei kubwa ndiyo maana tunauza kwa bei hii,” amesema.

Mfanyabiashara huyo amesema, “Siuzi sukari kwa bei ya juu, nauza kutokana na masilahi yangu, naangalia manunuzi na usafirishaji Sh85,000 kwa mfuko wa kilo 25, Mtwara tunauza kwa Sh95,000,” amesema Mulichi

Mfanyabiashara mwingine anayetuhumiwa katika suala hilo, Ramadhan Yusuph, amesema wanauza mfuko wa kilo 25 kwa Sh100,000 kwa sasa lakini awali ilikuwa Sh105,000.

“Huwa nanunua kwa wafanyabishara sinunui kiwandani, sipandishi bei ila nauza kulingana na pesa ambayo nimenunulia, mfano hii sukari nilinunua mfuko wa kilo 25 kwa Sh100,000, awali tulinunua Sh68,000 nasi tukauza Sh70,000,” amesema.

Mfanyabiashara ya rejareja ya sukari mkoani Mtwara, Shakira Malianus amesema kwa zaidi ya wiki hajapata bidhaa hiyo kwa kuwa kila anapoenda kuulizia huambiwa haipo.