Bei ya sukari yafunga kiwanda Arusha
Muktasari:
- Biashara ya magendo kupelekwa nchi jirani yatajwa, Serikali yaingilia kati
Arusha. Kutokana na kupanda kwa bei ya sukari na kukosekana mitaani, kiwanda cha vinywaji vikali cha Raha Beverage Company Ltd, kimesitisha uzalishaji kwa muda kutokana na kukosa bidhaa hiyo hatua ambayo imeifanya Serikali kuingilia kati.
Kiwanda hicho ambacho huzalisha vinywaji vikali vya Banana wine, Raha na vinywaji vingine maarufu mikoa ya Kanda ya Kaskazini na kina wafanyakazi 300.
Mahitaji ya sukari kwa siku ya kiwanda hicho kilichopo eneo la Olorieni jijini Arusha, ni mifuko 200 ya kilo 50 lakini hata hivyo licha ya kupanda bei kutoka Sh120,000 hadi Sh155,000 bado haipatikani.
Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Adolf Olomi akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumatatu Januari 22, 2024, amesema tayari wafanyakazi hao wamejulishwa juu ya mpango huo na kuwataka waanze kujiandaa kisaikolojia
Olomi amesema wamelazimika kuchukua hatua ya kukifunga kiwanda kuanzia Feberuari Mosi, mwaka huu, kutokana na uhaba wa sukari na bei kupanda.
Amesema mazingira yaliyopo ni vigumu kuendelea na uzalishaji kwa kuwa kiwanda kitashindwa kumudu gharama za uendeshaji.
"Tunasimamisha uzalishaji kwa muda kutokana na kupanda kwa bei ya sukari, imekuwa kubwa kutoka Sh120,000 hadi Sh155,000 kwa mfuko wa kilo 50 na haipatikani kabisa, sasa tumeona ni bora kukifunga kidogo,” amesema.
Hata hivyo, amesisitiza kwamba kiwanda hicho hakijafungwa moja kwa moja ila wamesimamisha uzalishaji kwa muda kupisha hali ya sukari hapa nchini itengemae na wanatarajia ifikapo Juni mwaka huu kitafungiliwa.
"Tutakapoanza uzalishaji moja ya changamoto ya kampuni hii ni gharama za uendeshaji zinazotokana na uwepo wa vituo vingi vya mauzo ambavyo havifanyi vizuri hivyo tumekusudia kuvifunga baadhi ya vituo hivyo katika mikoa ya Tanga,Dar es salaam na Morogoro tutavifunga ili kupunguza gharama za uendeshaji,” amesema.
Olomi amesema suala la kufunga kiwanda sio geni kwa kuwa mwaka 2019 waliwahi kukifunga kwa miezi mitatu ili kutatua changamoto za uendeshaji zilizokuwa zikikabili kiwanda hicho.
Msimamo wa Serikali kupaa kwa bei
Akizungumzia adha ya kupanda kwa bei, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa amesema Serikali imeanza uchunguzi kubaini wafanyabiashara wanaoficha sukari na kuuza kwa bei ya juu ili kuleta adha katika Jiji la Arusha.
Mtahengerwa ametangaza bei elekezi ya sukari kwenye jiji hilo ni Sh3,000 na amewataka wanancni watakaouziwa bidhaa hiyo kwa bei tofauti, watoe taarifa kwa watendaji wa kata au ofisini kwake ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Amezitaja hatua hizo ni pamoja na kuwafutia leseni za biashara na kuwafungulia mashauri ya uhujumu uchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, Mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali imefanya uchunguzi wa awali na kubaini kuna sukari kwenye maghala ya wafanyabiashara jijini Arusha, hivyo hakuna sababu za kupandisha bei.
"Nawapongeza wakala wa sukari ya TPC mkoani Arusha, mkurugenzi wa kampuni ya Alpha Group, Karim Dakik kwa kushirikiana na Serikali kuweka mikakati kuhakikisha bidhaa hiyo inawafikia wananchi kwa bei ya Sh3,000 tu,” amesema.
Mtahengerwa amesema ametembelea ghala la kuhifadhi sukari akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kujionea kiasi cha sukari kilichopo.
Anasema wamekuta kuna tani 307 zinatosheleza mahitaji ya jiji la Arusha.
Hivyo, amesisitiza kuwa anao uhakika wa bei aliyotangaza inatekelezeka kwa kuwa walifanya majadiliano ya kina na kampuni ya Alpha Group ambayo ni wakala wa TPC anayesambaza sukari jijini Arusha.
Amesema wakala huo unawauzia wafanyabiashara wa jumla kwa Sh2,800 kwa kilo moja, hivyo inawezekana kabisa kwa wananchi kuuziwa sukari kilo moja kwa Sh3,000 bei ya rejareja.
Mutahengerwa amewasihi wafanyabiashara wasitumie nafasi hiyo kuwaumiza wananchi kwa kuwapa bei kubwa na watakaokiuka watawanyang'anya leseni ya biashara sanjari na kuwachukilia hatua za kisheria ikiwemo kuwafungulia kesi za uhujumu uchumi.
"Wiki iliyopita niliwaelekeza wafanyabiashara kuuza bei iliyopangwa na serikali ya Sh3,000 .tulitembelea kata zote tukateua wafanyabiashara kadhaa ambao tutawapelekea sukari na gharama ya usafiri sisi serikali ndiyo tutaingia ili kuhakikisha wanauza sukari kwa bei elekezi ya Sh3,000," amesisitiza na kuongeza:
"Wafanyabiashara sitaki kusikia mfanyabiashara yoyote anauza sukari kwa bei ya zaidi Sh3,000 kwa kilo" amesema.
Amesema Serikali imeunda kikosi cha kufuatilia wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ya zaidi ya hiyo watakamatwa watafungulia kesi za uhujumu uchumi.
Amewaelekeza viongozi wa tarafa na kata kusimamia zoezi hilo, kuhakikisha wananchi wanauziwa sukari kwa bei ya Sh3,000 kwa kilo.
"Mwananchi yeyote akiuziwa sukari kwa bei ya zaidi ya Sh3,000 akatoe taarifa kwa mtendaji wa kata au aje kwangu na nitaenda kwa muuzaji husika na kumchukulia hatua za kisheria," amesisitiza Mtahengerwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Alpha Group, Karim Dakik amesema anaunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata sukari kwa bei ya Sh3,000 kwa kilo moja.
Amesema kwa kushirikiana na maofisa tarafa, wamekuwa wakipeleka sukari hiyo kwenye Kata mbalimbali za jiji la Arusha.
"Tumeweka matangazo kila sehemu kuonyesha kuwa hapa kwa sasa (kwenye ghala na ofisi zake zilizopo eneo la viwanda Unga Limitedi) nawahudumia wananchi wote sukari si lazima iwe kilo 50. Mtu yeyote anayetaka sukari aje kwangu nitawahudumia," amesema Dalia na kuongeza;
"Tumeamua kupeleka sukari kwenye Kata ili kuwaondolea wafanyabiashara gharama za usafirishaji jambo litakalowawezesha kuuza sukari kwa bei elekezi na wao wapate faida.
"Kuna changamoto ya mahesabu kwa sababu kuna maeneo yanayozunguka Arusha ikiwemo Wilaya ya Karatu na Mkoa wa Manyara wakikosa sukari huko kwao wanakimbilia hapa kuchukua," amesema.
Naye Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe katika taarifa yake juzi kwa vyombo vya habari alisema hali uzalishaji wa sukari katika viwanda saba nchini imeshuka hadi kufikia tani 1,000 kwa siku kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.
Amesema mvua hizo zimeathiri hali ya uvunaji wa miwa mashambani na kupunguza kiwango cha sukari.
Bashe amesema katika kukabiliana na upungufu wa sukari ambao sasa umefikia tani 30,000, Serikali imetoa kibali kwa wenye viwanda kuagiza sukari tani 100,000 ambayo inatarajiwa kuwasili nchini kati ya Januari 23 – 24 Januari mwaka huu.
Amesema mahitaji ya sukari kwa siku nchini ni tani 1,500 na kutokana na hali hiyo bei ya sukari imepanda kutoka 2,700, 3000 hadi kufikia 4000.
Wakati huo huo, uhaba mkubwa wa Sukari mkoani Arusha na Kilimanjaro unadaiwa kuchangiwa na biashara ya magendo kwenda nchi jirani.
Rehema Peter mkazi wa Namanga, amesema kuna biashara ya magendo ya sukari kwenda nchi jirani.
"Sina uhakika kama sukari inayovushwa inalipiwa kodi lakini ninachojua kuna biashara ya magendo kwa muda mrefu hapa,” amesema.