Tanzania kuondokana na uhaba wa sukari mwaka 2030

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa akizungumza kwenye kongamano la Wataalamu na watafiti wa Sukari nchini lenye lengo la kujadili changamoto za Sukari. Picha na Lilian Lucas

Morogoro. Rais wa Chama cha Wataalamu wa Sukari Tanzania (TSSCT), Geryson Kakigwa amesema hadi kufikia mwaka 2026 Tanzania itakuwa imeondokana na uagizaji wa sukari ya nyumbani huku sukari ya viwandani hadi mwaka 2030.

Kakigwa amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto ya sukari wataalamu hao bado wamekuwa wakifanya jitihada za upatikanaji wa Sukari ikilinganisha na miaka ya 1970 ambapo uzalishaji ulikuwa mkubwa ikilinganishwa na idadi ya watu kipindi hicho.

Hayo ameyasema leo Jumapili Aprili 30, 2023 katika kongamano la wataalamu na watafiti wa zao la miwa na sukari nchini lililofanyika mkoani Morogoro.

“Pamoja na kiwango cha uzalishaji sukari kuongezeka ikilinganishwa na miaka ya 1970, Tanzania bado haijitosherezi kwa mahitaji ya sukari, ambapo kwa kwasasa mahitaji ya sukari ni tani 686,000 kwa mwaka, kati ya hizo matumizi ya sukari ya nyumbani ni tani 481,000 na ya viwandani ni tani 205,000,”amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwasa amewataka wataalamu hao kuzitambua changamoto zilizopo na kuwa majasiri wa kutafuta njia sahihi ya kutatua changmoto hizo ili kufikia malengo ya utoshelevu wa sukari nchini.

“Binafsi nijivunia kuwa kwenye mkoa ambao unaongoza kwa uzalishaji nchini, tunaongoza kwa uzalishaji wa miwa lakini pia kwa uzalishaji wa sukari namba moja na tunapoona sukari inazalishwa kistaarabu tuna faraja na sisi serikali tunawaahidi tutaendelea kutoa ushirikiano kwa wazalishaji na wakulima ili kuhakikisha tunaleta na kuongeza tija,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Naye, Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Sekta ya Sukari Tanzania, Deo Lyato, amesema lengo la kongamano hilo ni kubadilishana mawazo na kuangalia maeneo gani ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi kitaalamu na kulinganisha mafanikio na mbinu zinazotumika katika sehemu mbalimbali kwenye sekta ya sukari, ambapo pia mada kuu ikiwa ni utafiti na teknolojia jinsi inavyoweza kusaidia ukuaji wa haraka.