‘Changamoto ya sukari kumalizwa mwezi ujao’


Muktasari:

Waziri Bashe amesema mvua zimeathiri uvunaji wa miwa na uchakataji wa bidhaa ambayo kwa sasa bei yake imeongezeka karibu mara mbili kwa baadhi ya maeneo.

Dar es Salaam. Wakati maumivu ya bei ya sukari yakiendelea kupamba moto, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amewahakikishia Watanzania kuwa tatizo la upatikanaji na upandaji wake wa  bei utamalizika katikati ya mwezi ujao.


Akitoa taarifa hiyo leo Jumamosi Januari 20 kuhusu mwenendo wa sekta ndogo ya sukari nchini, Bashe amesema tatizo kubwa ni mvua zinazoendelea kunyesha.


Waziri Bashe amesema zimeathiri uvunaji wa miwa na uchakataji wa bidhaa ambayo kwa sasa bei yake imeongezeka karibu mara mbili kwa baadhi ya maeneo.


Hata hivyo, Bashe amesema uzalishaji wa sukari nchini umekuwa ukiongezeka kwa kipindi cha miaka mitatu sasa.
Amesema upungufu wa sukari umefikia tani 30,000 kutoka tani 200,000 na matarajio ya mwaka huu yalikuwa ni kulimaliza pengo hilo.


“Mwaka jana zilizalishwa tani 460,000 ambazo ziliacha pengo la tani 30,000 ambazo tuliagiza, tulijua tutafikia mahali pa kujitosheleza mwaka huu tukitoka kwenye upungufu wa tani 150,000 hadi 200,000,” amesema Bashe.


Amesema mvua za elinino zimeathiri uvunaji wa miwa kutoka mashambani kwenda viwandani lakini pia kutokana na mvua hiyo, miwa inayovunwa kiwango chake cha sukari kimepungua kwa asilimia 25.


“Kutoka na mvua kuathiri uvunaji kiwanda kama Kilombero ambacho kwa kawaida huzalisha tani 700 kwa siku hivi sasa kinazalisha tani 250, TPC 450 hadi 180, Kagera kutoka tani 500 hadi 200 hadi 300, Mtibwa kutoka 450 sasa 120, Bagamoyo kutoka tani 160 na sasa wamesimamisha, Mkulazi kutoka tani 250 hadi 46,” amesema waziri huyo.


Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe


Kiongozi huyo mwenye dhamana ya bidhaa hiyo muhimu ya chakula, amesema tathimini inaonyesha mahitaji ya sukari kwa siku ni tani 1,500 lakini kwa sasa uwezo wa viwanda vyote vinazalisha tani 1,000 ndiyo maana kuna upungufu.

Hatua zilizochukuliwa na Serikali


Katika kulikabili hilo, Waziri Bashe amesema hatua ya kwanza iliyochukuliwa na Serikali ni kuagiza tani 100,000 za sukari kutoka nje ya nchi.


Amesema uamuzi huo umezingatia umuhimu wa kulinda viwanda vya ndani, na sukari hiyo itaanza kuingia nchini kesho na kesho kutwa.


“Bei ya sukari kabla ya tatizo hili kiwandani ilikuwa inauzwa kwa Sh2,200 hadi Sh2,270 na ya rejareja ilikuwa Sh2,700 hadi Sh3,000, leo bei imepanda baadhi ya maeneo hadi kufikia Sh4,000. Serikali tumewaagiza wenye viwanda na wauzaji wa jumla kusimamia usambazaji wao kama kawaida bila kumuumiza mlaji,” amesema Bashe.


Amesema Serikali imezungumza nao na kuwaandikia barua, hivyo anaamini tani hizo 100,000 zikiingia kwenye mzunguko zitasaidia kudhibiti bei hadi Februari hali ya usambazji itakuwa nzuri inayotamaniwa.


Lakini pia amewaonya wafanyabiashara kutotumia changamoto iliyopo sasa kujinufaisha kibiashara huku akiwakumbusha wenye viwanda kuchukua jukumu la kuwasimamia mawakala wao na kuhakikisha sukari inauzwa kwa bei elekezi na mwongozo wa Serikali.


“Niwaombe Watanzania wenzangu katika eneo hili la sukari tunaamini tutarudi katika hali yetu ya kawaida itakapofikia katikati ya mwezi Februari, usambazaji wa sukari utakuwa wa kutosha. Hili ni jambo la mpito, litatuathiri kwa kipindi kisichozidi siku 30,” amesema Bashe.


Aidha, ametoa wito kwa wakuu wa wilaya na mikoa nchini kuhakikisha wanafuatilia mwenendo wa usambazaji wa sukari kwenye maeneo yao na kama kuna upungufu, Serikali itoe mwongozo wa usambazaji.


Amesema Serikali inaamini mvua zitaendelea hadi mwezi wa tatu nayo itaendelea kutoa vibali vya kuingiza sukari ili kuendelea kumlinda mlaji huku akisema ulinzi kwa viwanda vya ndani utaondolewa endapo wataendelea na tabia ya kuficha sukari na kuongeza bei sokoni.


Kuhusu hali ilivyo ya uzalishaji ilivyo, Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari (SBT), Profesa Kenneth Bengesi amesema kila inapotokea nafuu ya kuanza kurudi kwenye hali nzuri ya uzalishaji mvua inaanza upya.


Amesema kulingana na hali inavyobadilika kila mara, wao pia wanabadili kiwango walichojipangia kukiingiza nchini na huenda hata mwezi ujao wakapitia upya.


“Uagiza wa sukari unachukua miezi miwili hadi kufika, tunaelekea kwenye mfungo, tusipofanya mapema unajikuta unaingia kwenye mfungo wa Ramadhani bila sukari kabisa. Usije ukashangaa hata hicho kiwango cha sasa tukakihuisha tena,” amesema huku akifafanua kwa nini kiwango kimeongezwa kutoka tani 50,000 hadi 100,000.