Polisi, SBT wadaka wafanyabiashara saba wa sukari

Muktasari:

  • Wafanyabiashara hao wa Mbagala Rangitatu na Tandika, wanadaiwa kupandisha bei ya sukari kutoka Sh2,700 hadi Sh4,000 kwa kilo moja kwa bei ya jumla.

Dar es Salaaam. Bodi ya Sukari Nchini (SBT)kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imewakamata wafanyabiashara saba waliokuwa wanauza sukari kwa bei ya juu.

 Wafanyabiashara hao wanadaiwa kuuza bidhaa hiyo kwa bei ya juu, kinyume na maelekezo yaliyotolewa na Serikali ya kuuza Sh3,000 kwa kilo na so vinginevyo.

Ofisa Udhibiti kutoka SBT, Suzana Wenceslaus amesema bodi hiyo imefanya opereshi ya kushtukiza leo, Januari 23, 2024 katika maduka makubwa ya jumla ya bidhaa hiyo katika mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

“Tumefanya operesheni hii kwa lengo la kuangalia wafanyabiashara wasio waaminifu wanaopandisha bei ya sukari kiholela kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe bila kumwangalia mlaji wa mwisho.

“Kwa Wilaya ya Temeke pekee, tumefanikiwa kukamata wafanyabiashara wakubwa saba waliokuwa wanauza sukari kwa bei ya juu kinyume na maelekezo yaliyotolewa na Serikali katika eneo la Mbagala Rangitatu na Tandika," amesema.

Amewataja wafanyabiashara wanaotuhumiwa kuuza bishaa hiyo kwa bei ya juu kuwa ni pamoja na Hasimu Juma Chepa, Omari Sobo, Benward Mwalongo, Mabula Malale, Kajeno Barabungwa, Pendo Malale na Trezor Kiza, wote kutoka Wilaya ya Temeke.

Akifafanua zaidi jinsi walivyowakamatwa, amesema waliweka mtego kwa wafanyabiashara ikiwemo kununua bidhaa hiyo na kupewa risiti kutoka katika maduka hayo.

Amesema wafanyabiashara hao walikutwa wanauza sukari kwa bei ya juu kati ya Sh 3m800 hadi Sh4,000 kwa kilo na mfuko mmoja wenye ujazo wa kilo 50 ukiuzwa kati ya Sh190,000 hadi Sh200,000, huku mfuko wa kilo 25 ukiuzwa Sh95,000 hadi Sh102, 000 kwa bei ya jumla.

“Wafanyabiashara hao tumewakamata na tumewapeleka Kituo cha Polisi Chang'ombe kwa ajili ya kuchukuliwa maelezo na baada ya hapo tutawafikisha mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria" amesema na kuongeza;

“Ni rai yetu kwa wafanyabiashara wote kufuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali ya bei inayotakiwa kuuzwa na sio kujipangia bei kwa ajili ya kujinufaisha wao wenyewe."

Pia ameongeza kusema: “Operesheni hii ni endelevu nchi nzima, kuna wenzangu wanaendelea na zoezi hili katika maeneo ya Mazese, Kariakoo, Magomeni na maeneo mengine ambavyo tumebaini wafanyabiashara wanauza sukari kwa bei ya juu."

Amesema mbali na Dar es Salaam, operesheni hiyo, inatekelezwa katika ya Arusha, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Tabora na Mtwara.

Januari 20, 2024 Waziri Bashe wakati akitoa taarifa kuhusu mwenendo wa sekta ndogo ya sukari, alisema tatizo kubwa linalochangia kuwa na uhaba wa sukari mvua zinazoendelea kunyesha nchini, ambazo zimeathiri uvunaji wa miwa na uchakataji wa bidhaa hiyo.

Alisema bei ya sukari kabla ya tatizo, viwanda ilikuwa inauzwa Sh2,200 hadi 2,700 kwa bei ya jumla na Sh 2,700 hadi 3,000 kwa bei ya rejareja.

Hata hivyo, alisema tayari Serikali imetoa kibali kwa ajili ya ununuzi wa tani 100,000 za sukari kutoka nje ya nchi.