Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sirro atoa neno kwa washiriki wa Nane Nane

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Sirro, akitoa taarifa kwa umma kuhusu maandalizi ya kuelekea Maonesho ya Nane Nane yatakayofanyika kuanzia Agosti 1, 2026, katika Uwanja wa Nane Nane Ipuli, Manispaa ya Tabora.

Muktasari:

  • Maonesho ya Nane Nane mwaka huu ni ya 15 na yamebeba kaulimbiu isemayo, "Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050."

Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Sirro amewataka wajasiriamali, wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wote watakaoshiriki maonesho ya Nane Nane mwaka huu, kuzingatia ubora wa bidhaa pamoja na matumizi ya vifungashio vinavyokidhi viwango ili kuongeza thamani ya bidhaa na kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi.

Sirro ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Maonesho hayo, ametoa rai hiyo leo Jumamosi, Julai 25, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maonesho hayo yatakayofanyika katika Viwanja vya Nane Nane vilivyopo Kata ya Ipuli, Manispaa ya Tabora.

Amesema ubora wa vifungashio ni sehemu muhimu ya ushindani wa bidhaa sokoni kwa kuwa huongeza mvuto kwa walaji na kujenga imani kuhusu ubora wa bidhaa husika.

"Vifungashio bora ni jambo la kuzingatia sana kwa sababu navyo vinachangia kuuza bidhaa. Pia vinampa mteja imani kuwa bidhaa anayokwenda kutumia ni salama na inakidhi viwango," amesema Sirro.

Amesema maonesho hayo yatatoa fursa kwa wakulima, wavuvi na wajasiriamali kujifunza matumizi ya teknolojia za kisasa zitakazowawezesha kuongeza tija na ubora wa uzalishaji.

"Hii ni fursa muhimu ya kujifunza na kutumia teknolojia katika uzalishaji. Tunahitaji kilimo na uvuvi wenye tija ili kuongeza uzalishaji na kipato," amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, John Mboya, amesema Maonesho ya Nane Nane yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kujifunza fursa mpya za kiuchumi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

"Tunapokutana katika maonesho haya, kila mmoja akiwa ameleta bidhaa au huduma yake, tunapata nafasi ya kujifunza teknolojia na mbinu mpya ambazo baadaye huongeza tija na kipato katika shughuli zetu," amesema Mboya.

Naye Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kigoma anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, James Peter amesema lengo la maonesho hayo ni kuwawezesha wazalishaji kuongeza tija, kupata masoko na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

"Tupo kuhakikisha wazalishaji wanapata mazingira bora ya kuzalisha kwa tija na kunufaika na fursa zilizopo katika sekta mbalimbali," amesema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, John Pima, amesema maandalizi ya maonesho hayo yamekamilika kwa kiwango kikubwa, ikiwemo kuboresha miundombinu ya viwanja na maeneo ya huduma kwa wageni.

"Tumejipanga kuhakikisha washiriki na wageni wote wanapata mazingira mazuri. Maeneo ya maegesho ya magari ni ya kutosha na salama, pamoja na huduma nyingine muhimu," amesema Pima.

Baadhi ya washiriki wa maonesho hayo wamesema yameendelea kuwa chachu ya kupanua masoko ya bidhaa zao.

Mjasiriamali wa Mkoa wa Tabora, Ashura Mwazembe, amesema hatua ya Serikali kuendelea kutangaza na kuimarisha maonesho hayo imewapa wazalishaji fursa ya kupata masoko mapya.

"Hapo awali tulikuwa tunazalisha lakini changamoto ilikuwa soko. Sasa tumepata fursa ya kuunganishwa na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi. Kilichobaki ni kuhakikisha bidhaa zetu zinakidhi viwango na kupata ithibati kama ya TBS ili ziweze kushindana katika masoko ya kimataifa," amesema.

Naye kijana mjasiriamali wa Manispaa ya Tabora, Shomari Ibrahim, amesema matumizi ya teknolojia yamekuwa nyenzo muhimu ya kuongeza kipato kwa vijana na kwamba maonesho hayo yanatoa nafasi ya kuonyesha ubunifu wao.

"Kwetu sisi vijana, Maonesho ya Nane Nane ni jukwaa la kuonyesha bunifu na bidhaa zetu. Tunapaswa kutumia teknolojia kama fursa ya kujiongezea kipato badala ya kuitumia katika mambo yasiyo na tija," amesema.

Maonesho ya Nane Nane mwaka huu ni ya 15 na yamebeba kaulimbiu isemayo, "Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050."