Prime
Tanzania inavyovuna fursa mpya za uwekezaji Russia, Singapore
Muktasari:
- Baada ya ziara ya Russia, Tanzania inatarajia kupokea uwekezaji wa zaidi ya Sh5.25 trilioni, uwekezaji huu utaifanya Russia kuwa miongoni mwa wadau wakubwa wa maendeleo upande wa Tanzania.
Katika kipindi ambacho ushindani wa kuvutia mitaji ya kimataifa unazidi kuongezeka, Tanzania imejijengea nafasi kama moja ya maeneo yanayovutia wawekezaji barani Afrika kutokana na utulivu wa kisiasa, rasilimali nyingi za asili na eneo lake la kimkakati linalounganisha masoko ya Afrika Mashariki, Kusini na Kati.
Hata hivyo, swali kubwa linalobaki ni namna gani nchi inaweza kuhakikisha kuwa uwekezaji wa kigeni unaoingia unachochea mageuzi ya uchumi badala ya kuishia kuwa chanzo cha mapato ya muda mfupi.
Kutokana na shabaha zake za kiuchumi na kiuwekezaji Tanzania imeendelea kuvutia uwekezaji huo kupitia mikutano, ziara za kikazi katika mataifa mbalimbali zinazofanywa na Rais Samia na viongozi mbalimbali wa serikali.
Moja ya ziara zilizofanyika hivi karibuni ni ile ya nchini Russia Juni 3 hadi 5 mwaka huu iliyofuatiwa na ziara ya Rais wa Singapore.
Baada ya ziara ya Russia, Tanzania inatarajia kupokea uwekezaji wa zaidi ya Sh5.25 trilioni, uwekezaji huu utaifanya Russia kuwa miongoni mwa wadau wakubwa wa maendeleo upande wa Tanzania.
Lakini ni kwa namna gani Tanzania imejipanga kutumia fursa zote zinazokuja baada ya kutafutwa?
Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga anasema sasa Tanzania imeingia katika hatua mpya ya utekelezaji wa fursa za uwekezaji huo akitaja Wizara ya Viwanda na Biashara itakavyosuka mikakati ya maandalizi.
“Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan imefungua milango ya fursa kubwa za kiuchumi. Serikali itaendelea kuratibu masuala ya kibiashara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi nyingine kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki,” anasema Ulanga.
Anaongeza kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha sekta ya usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuanzisha safari za moja kwa moja Dar es Salaam- Moscow ili kuchochea uhusiano huo wa kibiashara.
“ATCL itakuwa nyenzo muhimu ya kuunganisha masoko. Tutaendelea kuwapokea wawekezaji kutoka Russia na baada ya miezi mitatu tutatoa tathmini ya matokeo ya fursa zilizopatikana,” anasema.
Kwa upande wake, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo anasema Tanzania iko katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 inayolenga kuvutia mitaji kutoka mataifa mbalimbali bila kujali upande wa kisiasa.
“Tunapoanza utekelezaji wa Dira 2050 tunahitaji wadau wa ndani na nje ya nchi. Hatutachagua marafiki wa kufanya nao kazi. Tutasaka fursa popote duniani,” anasema Profesa Mkumbo.
Alifafanua kuwa Tanzania na Russia zimeanzisha Tume ya Pamoja ya Serikali (Intergovernmental Commission) ambayo imekubaliana kushirikiana katika maeneo tisa ya kimkakati yakiwamo kilimo, elimu, nishati, madini, biashara na uwekezaji.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, alihoji kiwango cha maandalizi ya ndani ya nchi kabla ya kupokea uwekezaji huo mkubwa, akisisitiza jamii kujiandaa kupokea nia hiyo njema iliyooneshwa na Taifa la Russia kuwekeza nchini.
“Wakati Russia inaonesha nia ya kuwekeza nchini kwetu, ni lazima tujiulize sisi kama taifa tumejiandaaje kunufaika na fursa hizi,” anasema Kombo.
Hata hivyo wachambuzi wanasema uzoefu unaonyesha kuwa uwekezaji wa kimkakati nchini umekuwa ukiibua mijadala kuhusu uwazi wa mikataba, maslahi ya taifa na ushiriki wa wananchi, hali ambayo imekuwa ikiathiri ushiriki wa jamii kwenye fursa za uwekezaji huo.
Wadau wameweka msisitizo katika maeneo makuu matatu; mshikamano wa kitaifa, uwazi wa mikataba ya uwekezaji na elimu kwa wananchi ili kupunguza sintofahamu na kuimarisha uhalali wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda anasema uwekezaji wa Russia unaweza kuibua presha za kimataifa na kuathiriwa na mgawanyiko wa ndani kama hakuna mshikamano wa kitaifa.
“Kwa sasa tunazungumzia Tanzania ambayo ina changamoto zake za ndani, lakini pia imefungua mlango kwa mwekezaji ambaye ana mvutano na baadhi ya mataifa makubwa. Hii inaweza kuleta presha za kidiplomasia,” anasema.
Anaongeza kuwa suluhisho ni kujenga mshikamano wa kitaifa na kufanya maamuzi ya pamoja kuhusu mikataba ya kimkakati.
“Namna ya msingi ni kuhakikisha tunakuwa na mshikamano wa ndani. Tujenge uelewa wa pamoja na tuondoe tofauti za kisiasa ili tusifungue mianya ya migogoro ya nje kuingilia ajenda zetu,” anasema.
Mtazamo kama huo umetolewa pia na mchambuzi wa masuala ya diplomasia, Godwin Amani, ambaye amesema wananchi wanapaswa kuhusishwa zaidi ili kuongeza uelewa na kukubali miradi hiyo. “Uwekezaji wote unahitaji umoja wa kitaifa. Jamii ikigawanyika, hata mwekezaji anakosa ushirikiano wa kijamii,” anasema.
Anafafanua kuwa suluhisho ni elimu kwa wananchi kuhusu manufaa ya uwekezaji huo ili kuimarisha uaminifu na ushirikiano.
“Serikali inapaswa kuwaunganisha wananchi na kuwaelimisha ili waone uwekezaji kama mali yao. Hapo ndipo miradi inapata uhalali wa kijamii,” amesema.
Ziara Rais wa Singapore
Wakati hilo likifanyika, siku mbili nyuma katika ziara ya Rais wa Singapore, Tanzania kupitia Rais Samia ilinadi tena maeneo matano ya kipaumbele cha ushirikiano, ikiwemo sekta ya biashara na bandari ambapo alieleza nafasi ya kimkakati ya Tanzania katika kuhudumia nchi zisizokuwa na bandari.
“Upanuzi wa bandari na uwekezaji katika huduma za meli na usafirishaji unatoa fursa kubwa ya kuongeza ufanisi wa biashara ya kikanda na kimataifa hususan kwa kushirikiana na wadau kutoka Singapore,” anasema.
Katika eneo la kilimo biashara anasema kuna fursa katika uongezaji thamani kwenye kuimarisha minyororo ya thamani katika mazao ya chai, kahawa, korosho na viungo, sambamba na kuongeza upatikanaji wa masoko ya bidhaa hizo katika soko la Asia.
“Uongezaji thamani katika madini, Tanzania bado inakabiliwa na changamoto ya kusafirisha malighafi nyingi bila kuchakatwa, hali inayopunguza thamani halisi ya rasilimali hizo katika soko la dunia. Kushirikiana na wawekezaji wa Singapore kunaweza kusaidia Tanzania kuhama kutoka uchumi wa malighafi kwenda uchumi wa bidhaa zilizoongezwa thamani, ikiwemo vito na bidhaa za viwandani.,” amesema.
Maeneo mengine ni ushirikiano katika kukuza uchumi wa bluu, nishati mbadala na miundombinu endelevu na utalii.
Akizungumza katika Jukwaa hilo, Rais wa Singapore Tharman Shanmugaratnam alisema mataifa hayo mawili yanajenga juu ya uhusiano wa muda mrefu uliotokana na biashara kupitia Bahari ya Hindi.
Ingawa yako mbali kijiografia, amesema Tanzania na Singapore zinashirikiana kupitia historia ndefu ya mawasiliano ya kibiashara ambayo inaweza kuwa msingi wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi katika mazingira ya sasa ya dunia yenye kutokuwa na uhakika zaidi.
“Tunafahamu kuwa mfumo wa biashara wa kimataifa si ule wa zamani. Sasa ni wa kutokuwa na uhakika zaidi na hali hiyo huenda ikaendelea kudumu. Katika dunia kama hii suluhisho ni kutanua ushirikiano kujenga njia mpya za fursa na kuunda minyororo ya usambazaji yenye ustahimilivu zaidi,” anasema.
Rais Shanmugaratnam alielezea Tanzania kama nchi yenye matumaini makubwa akitaja idadi kubwa ya vijana, rasilimali nyingi za asili, fursa zinazopanuka za uwekezaji na nafasi yake ya kimkakati inayounganisha masoko ya kikanda na ya kimataifa.
Alisema sekta kama kilimo-biashara, utalii, miundombinu, usafirishaji na uchumi wa kidijitali zina fursa kubwa za ushirikiano kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Singapore.
“Kuanzia kilimo biashara hadi utalii, kuna uwezekano mkubwa wa ushirikiano wa maana unaochanganya fursa za Tanzania na uzoefu wa Singapore katika mifumo bora ya ufanisi, usimamizi wa kisasa wa minyororo ya usambazaji, huduma zenye thamani ya juu na uchumi wa kidijitali,” alisema.
Katika kongamano hilo Mwenyekiti wa Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Angelina Ngalula anasema urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili sasa unapaswa kugeuzwa kuwa ushirikiano halisi wa kibiashara, ubia wa pamoja na uwekezaji.
Anasema uwezo wa Singapore katika teknolojia, huduma za kifedha, usafirishaji, uhandisi na maendeleo ya ujuzi unaendana kwa karibu na vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania.
“Serikali zinaweza kuweka mazingira wezeshi na kufungua milango, lakini sekta binafsi ndiyo inapaswa kuendesha biashara na uwekezaji. Makubaliano halisi yatafikiwa na wafanyabiashara,” amesema.
Ngalula aliitaka kampuni kutoka nchi zote mbili kutumia majadiliano ya moja kwa moja kati ya wafanyabiashara (business-to-business) ili kubaini fursa za uwekezaji na kujikita katika hatua za vitendo za ufuatiliaji.
Ushirikiano wa kihistoria wa Russia, Singapole kwa Tanzania
Ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi ni wa kihistoria na umejengwa katika msingi wa urafiki, mshikamano na ushirikiano wa maendeleo kwa zaidi ya miongo sita.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo ulianza mara baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, ambapo Umoja wa Kisovieti (Urusi ya sasa) ulikuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza kutambua uhuru wa Tanzania na kuanzisha ushirikiano wa karibu na Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere.
Katika miaka ya mwanzo ya uhuru, Russia ilitoa msaada katika nyanja mbalimbali ikiwamo elimu, afya, teknolojia, ujenzi wa miundombinu na mafunzo ya kijeshi. Mamia ya Watanzania walipata ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu vya Russia, jambo lililosaidia kuandaa wataalamu waliokuja kuhudumu katika sekta mbalimbali nchini. Ushirikiano huo pia uliimarisha uwezo wa Tanzania katika masuala ya ulinzi na usalama.
Katika kipindi cha sasa, Tanzania na Russia zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika biashara, uwekezaji, madini, nishati, utalii, kilimo na usafirishaji.
Mahusiano hayo ya muda mrefu yameendelea kudumishwa kwa kuheshimiana na kutambua maslahi ya pande zote, jambo linaloifanya Tanzania na Russia kuwa washirika wa kimkakati katika juhudi za kukuza maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi wao.
Kihistoria, ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore ulianza baada ya nchi zote kupata uhuru katika miaka ya 1960 na kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia yaliyolenga kuimarisha urafiki na ushirikiano wa maendeleo.
Ingawa kwa muda mrefu ushirikiano huo haukuwa mkubwa kama ule wa baadhi ya mataifa mengine, nchi hizo zimeendelea kudumisha uhusiano mzuri wa kisiasa na kiuchumi.
Katika miaka ya karibuni, mahusiano yameimarika zaidi kupitia biashara, uwekezaji, usafiri wa baharini, maendeleo ya bandari na uchumi wa kidijitali.
Ushirikiano huo unaendelea kukua huku Tanzania ikinufaika na uzoefu wa Singapore katika maendeleo ya uchumi na usimamizi wa miundombinu.
Kwa ujumla ziara za viongozi wa nchi hizo zimechochea makubaliano ya kuongeza ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji.