Prime
Somo kubwa linalopaswa kuzingatiwa baada ya ziara ya Rais Samia Russia
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisalimiana na mwenyeji wake, Rais wa Russia, Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow wakati wa ziara yake Juni 3, 2026 nchini humo.
“Uimara na udhaifu wa taasisi za dola. Anguko la dola na kuinuka kwake. Matumizi bora ya rasilimali za nchi na nguvu ya uwekezaji kwenye kilimo. Uongozi wenye maono na unaotafsiri vizazi vingi vijavyo kiuchumi, kiteknolojia, kiulinzi. Russia kutoka kuwa moyo wa dola yenye nguvu duniani (superpower), kufilisika, kisha kurudi kwenye mstari kwa ujasiri mkubwa.”
Unaweza kusema huo ni muhtasari unaosomeka baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumaliza ziara yake ya kihistoria nchini Russia.
Tayari mijadala mingi imejikita katika manufaa ya sasa yatakayotokana na ushirikiano mpya kati ya Tanzania na taifa hilo.
Bila shaka, faida za kiuchumi, kibiashara, kidiplomasia na kielimu zinazotarajiwa kutokana na ushirikiano huo ni jambo la msingi. Hata hivyo, nyuma ya manufaa hayo ya haraka, kuna somo kubwa zaidi ambalo Tanzania inapaswa kulichukua; namna ya kuijenga nchi juu ya misingi imara ya kitaasisi itakayowezesha taifa kubaki salama hata baada ya kukumbwa na dhoruba za kisiasa, kiuchumi au kijamii.
Ili kuelewa somo hilo, ni muhimu kurejea historia ya Umoja wa Jamhuri za Kijamaa za Soviet (USSR), dola iliyokuwa miongoni mwa mataifa yenye nguvu zaidi duniani kuanzia mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945 hadi kusambaratika kwake mwaka 1991.
Nguzo kuu za USSR zilikuwa jeshi lake kubwa na lenye nguvu zaidi duniani kwa wakati huo, hifadhi kubwa ya silaha za nyuklia, pamoja na mtandao mpana wa washirika wake katika mabara mbalimbali.
USSR pia ilikuwa kinara wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya anga. Mwaka 1957 ilizindua satelaiti ya kwanza duniani, Sputnik, hatua iliyofungua ukurasa mpya katika historia ya sayansi ya anga na kuanzisha kile kilichokuja kujulikana kama mbio za anga kati ya mataifa makubwa.
Miaka minne baadaye, mwaka 1961, USSR iliandika historia nyingine kwa kumpeleka Yuri Gagarin kuwa binadamu wa kwanza kufika anga za mbali.
Mbali na mafanikio hayo ya kisayansi, USSR lilikuwa taifa lenye eneo kubwa zaidi duniani, likianzia Ulaya Mashariki hadi sehemu kubwa ya Asia. Ilikuwa mbele katika mapinduzi ya viwanda na kilimo, huku uchumi wake ukiendeshwa kwa mfumo wa mipango uliodhibitiwa moja kwa moja na serikali.
Ni muhimu pia kukumbuka kuwa wakati mataifa mengi ya Magharibi yalipokuwa yakikabiliwa na mdororo mkubwa wa uchumi uliojulikana kama Great Depression kati ya mwaka 1929 na 1939, USSR iliendelea kuimarisha uzalishaji wake wa viwandani na kilimo.
Mdororo huo mkubwa wa uchumi ulianzia Marekani baada ya kuporomoka kwa thamani ya hisa katika soko la fedha na kuathiri kwa kiwango kikubwa mataifa mengi yaliyokuwa yakifuata mfumo wa kibepari.
Katika kipindi hicho, USSR iliendelea kuimarisha uchumi wake kupitia mfumo wa kikomunisti. Viwanda vilizalisha kwa kiwango kikubwa na bidhaa zake kusafirishwa ndani na nje ya mipaka yake. Kilimo kilistawi, taifa likajitosheleza kwa chakula na hata kuuza ziada katika masoko ya nje.
Sekta za huduma kama benki, bima, usafiri, afya, utalii na biashara zilikuwa zimepiga hatua kubwa. Kwa kifupi, USSR ilikuwa dola yenye uwezo mkubwa wa kufanya mambo mengi ambayo mataifa mengine yalitamani kuyafikia.
Kwa sababu hiyo, taifa hilo liliogopwa na kuheshimiwa duniani. Hakukuwa na taifa lililokuwa tayari kulikabili kijeshi kwa urahisi. Wakati huo, USSR ilikuwa moja ya dola mbili zenye nguvu zaidi duniani.
Somo linapoanzia
Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, dunia iliingia katika kipindi kipya cha ushindani wa kimataifa kati ya Marekani na USSR. Haya yalikuwa mataifa mawili yenye nguvu kubwa kuliko mengine yote.
Zilikuwa zama za mafahari wawili ndani ya sayari moja. Kila upande ulitaka kuonyesha ubora wake kijeshi, kiuchumi, kisayansi na kiitikadi.
Ushindani huo ulizaa kile kilichoitwa Vita Baridi, vilivyodumu kwa miaka 46 kuanzia mwaka 1945 hadi 1991.
Katika vita hivyo hakukuwa na mapambano ya moja kwa moja kati ya Marekani na USSR. Badala yake, kila upande ulitumia mataifa mengine kama uwanja wa kuonyesha nguvu zake.
Migogoro ya Korea katika miaka ya 1950, Vietnam katika miaka ya 1960 na 1970, pamoja na Afghanistan katika miaka ya 1980, ni baadhi ya mifano ya namna ushindani huo ulivyofanyika.
Kulikuwa pia na vita vya teknolojia na sayansi. USSR ilitangulia kwa kuzindua Sputnik mwaka 1957 na baadaye kumpeleka Yuri Gagarin angani mwaka 1961.
Marekani ilijibu kwa kufanikisha safari ya kwanza ya binadamu kutua mwezini Julai 20, 1969 kupitia Neil Armstrong, Buzz Aldrin na Michael Collins.
Lakini nyuma ya mafanikio hayo yote, kulikuwa na mapambano ya ndani ya mifumo ya dola hizo mbili. Mwishoni, Marekani ilishinda Vita Baridi na USSR ikasambaratika.
Swali kubwa ni kwa nini taifa lenye nguvu kiasi hicho lilianguka?
Jibu halipo katika jeshi, silaha au rasilimali zake. Tatizo kubwa lilikuwa katika udhaifu wa taasisi zake.
Licha ya kuwa na nguvu kubwa kijeshi, kisayansi na kiuchumi, USSR ilishindwa kujenga taasisi imara ambazo zingeweza kustahimili mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi.
Urusi Baada ya USSR
Baada ya kusambaratika kwa USSR mwaka 1991, Russia ilirithi karibu kila kitu kilichokuwa chini ya dola hiyo.
Ilirithi kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na haki ya kura ya turufu (veto). Ilirithi pia hifadhi kubwa ya silaha za nyuklia, viwanda, miundombinu na mali nyingi za kimkakati.
Kwa kuangalia ukubwa wa urithi huo, wengi walitarajia Urusi ingeendelea kuwa superpower sambamba na Marekani.
Hata hivyo, hali haikuwa hivyo
Mapema miaka ya 1990, Russia (Urusi) ilianza kubadili mfumo wake wa uchumi kutoka ule wa kikomunisti uliodhibitiwa na serikali kwenda mfumo wa soko huria kupitia mpango ulioitwa Shock Therapy.
Lengo lilikuwa kuharakisha mageuzi ya kiuchumi na kuipa nchi nguvu mpya ya ushindani. Lakini matokeo yake yalikuwa tofauti na matarajio.
Serikali iliondoa udhibiti wa bei za bidhaa, ikabinafsisha mashirika mengi ya umma na kufungua biashara za kimataifa kwa kasi kubwa.
Hatua hizo zilisababisha mfumuko mkubwa wa bei, kuporomoka kwa pato la taifa na kuibuka kwa kundi dogo la matajiri wenye ushawishi mkubwa, maarufu kama oligarchs.
Mwaka 1992 pekee, mfumuko wa bei ulifikia zaidi ya asilimia 2,000 huku pato la taifa likishuka kwa kiwango kikubwa. Mamilioni ya wananchi walipoteza akiba zao na maisha yao kuwa magumu.
Ukosefu wa ajira uliongezeka, mishahara ilicheleweshwa kwa muda mrefu na huduma za jamii zikadhoofika.
Kwa kifupi, taifa lililorithi utajiri mkubwa wa USSR lilijikuta katika hali ya kufilisika ndani ya muda mfupi.
Sababu kuu ilikuwa mifumo dhaifu ya kitaasisi.
Taasisi dhaifu huzalisha sera dhaifu, na sera dhaifu husababisha utekelezaji dhaifu. Matokeo yake ni kuyumba kwa taifa hata kama lina rasilimali nyingi.
Somo linaendelea
Mwishoni mwa mwaka 1999, Vladimir Putin alichukua madaraka kutoka kwa Boris Yeltsin.
Katika miaka iliyofuata, nchi hiyo ilianza kuimarisha taasisi zake za kisiasa na kiuchumi. Serikali ilirejesha udhibiti katika baadhi ya sekta za kimkakati, kupunguza nguvu za oligarchs na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za taifa.
Hatua hizo ziliwezesha uchumi kuanza kukua tena. Mfumuko wa bei ulidhibitiwa, sekta za viwanda na kilimo zikaanza kuimarika na taifa kurejesha sehemu ya hadhi yake ya kimataifa.
Leo hii, Russia ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta, gesi asilia, makaa ya mawe, ngano na bidhaa nyingine nyingi duniani.
Mafanikio hayo hayajatokana na rasilimali pekee, bali yamechangiwa na uwepo wa taasisi zenye uwezo wa kusimamia rasilimali hizo kwa ufanisi.
Ndiyo maana, pamoja na mafanikio yote yaliyopatikana katika ziara ya Rais Samia nchini Russia, ikiwamo kusainiwa kwa mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi, biashara, elimu na diplomasia, pamoja na kufunguliwa kwa fursa mpya za usafiri wa anga na uwekezaji, somo kubwa zaidi linapaswa kuwa tofauti.
Tanzania inapaswa kujifunza kutoka historia ya USSR na safari ya Russia ya baadaye kwamba maendeleo ya taifa hayaamuliwi na wingi wa rasilimali au ubora wa viongozi pekee.
Nguvu ya taifa ipo katika uimara wa taasisi zake.
USSR ilipoteza hadhi yake kwa sababu taasisi zake zilikuwa dhaifu. Russia ilianza kurejea katika mstari baada ya kuimarisha taasisi hizo.
Kwa Tanzania, changamoto kubwa si kujenga viongozi bora pekee, bali kujenga taasisi bora zinazoweza kusimamia sheria, uchumi, rasilimali na utawala bila kutegemea mtu mmoja au kizazi kimoja cha viongozi.
Kwa sababu mwisho wa siku viongozi hupita, lakini taasisi hubaki.
Na taasisi imara huzaa sera bora, utekelezaji wenye tija na taifa linaloweza kustahimili dhoruba za aina yoyote.