Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ZIARA YA SAMIA RUSSIA: Wachambuzi wamuunga mkono Samia ila watoa tahadhari

Muktasari:

  • Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, miaka mitano iliyopita, mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Russia yameongezeka kutoka Dola 7.5 milioni za Marekani (Sh19.5 bilioni)  mwaka 2020 hadi kufikia Dola 29.5 milioni (Sh76.7 bilioni) mwaka 2025.



Dar es Salaam. Wachambuzi wa masuala ya siasa na diplomasia wameunga mkono kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba, Tanzania haichagui kambi za kimataifa, bali hushirikiana na mataifa yote kwa masilahi ya maendeleo yake.

Hata hivyo, wameonya kuwa nchi inapaswa kuwa makini inapopanua ushirikiano wake wa kimataifa kutokana na mabadiliko yanayoendelea katika siasa za dunia na ushindani wa ushawishi kati ya mataifa makubwa duniani.

Kauli hiyo inakuja baada ya Rais Samia kufanya  mahojiano na waandishi wa habari wa Tanzania, kando mwa Jukwaa la 29 la Uchumi la Kimataifa la St Petersburg (SPIEF 2026) nchini Russia, Juni 5, 2026.

Rais Samia amesema madai ya kwamba, ziara yake ya kiserikali nchini Russia inaashiria mabadiliko ya mwelekeo wa sera ya mambo ya nje ya Tanzania, si sawa, bali nchi inaendelea kuamini sera yake ya muda mrefu ya kutofungamana na upande wowote.

“Tunafanya kazi na kila mtu. Hatuwachagui watu wa kufanya nao kazi. Kwa kuja Russia, tunaongeza tu wigo wa ushirikiano wetu wa karibu,” amesema Rais Samia.

Kauli yake hiyo imekuja kufuatia mijadala iliyoibuka ya kuichagua Russia kuwa nchi ya kwanza kuitembelea katika ziara ya kiserikali baada ya kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Tanzania, huenda kulimaanisha kuhamia upande wa mataifa ya Mashariki na kuachana na washirika wa Magharibi.

Rais Samia amekataa tafsiri hiyo, akieleza kuwa Russia si rafiki mpya wa Tanzania bali ni mmoja wa washirika wake wa muda mrefu.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Salbinus David amesema ushirikiano wa Tanzania na Russia haupaswi kutafsiriwa kama kuachana na misingi ya sera ya mambo ya nje ambayo nchi imeifuata kwa miaka mingi.

“Tanzania imekuwa ikifuata sera ya diplomasia ya kutofungamana na upande wowote na inayozingatia uhalisia wa mazingira. Nchi haijawahi kuchagua marafiki au washirika kwa kuzingatia ushindani wa mataifa makubwa. Kilicho muhimu ni kama ushirikiano huo unaleta manufaa kwa taifa na kuchangia maendeleo ya uchumi,” amesema.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Profesa Ali Makame Ussi amesema mazingira ya sasa ya dunia yanahitaji nchi kama Tanzania kuipa kipaumbele diplomasia ya uchumi kuliko kujipambanua kwa misingi ya kambi za kisiasa.

“Kinachopaswa kupewa uzito ni kupanua fursa za biashara, uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia na maendeleo ya viwanda. Nchi yoyote inayotoa fursa hizo inapaswa kuonekana kuwa mshirika anayefaa. Tanzania haipaswi kuitenga nchi yoyote kwa sababu ya masilahi ya kimkakati ya mataifa mengine,” amesema.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie amesema ni muhimu kwa Tanzania kuendelea kupanua wigo wa ushirikiano wa kimataifa, lakini iifanye hivyo kwa tahadhari.

“Dunia inazidi kuwa ngumu zaidi huku mataifa makubwa yakishindania ushawishi katika maeneo mbalimbali. Tanzania inapaswa kuendelea kushirikiana kimkakati na mataifa mengine kwa kuzingatia vipaumbele vyake vya maendeleo, badala ya kufuata misimamo ya kiitikadi,” amesema.

“Jambo muhimu ni kushirikiana na washirika kwa misingi ya manufaa ya pamoja na masilahi ya Taifa, si kwa kuangalia nani yuko upande gani katika siasa za dunia,” amesisitiza.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari, Rais Samia amesema uhusiano kati ya Tanzania na Russia una mizizi ya muda mrefu inayorejea kipindi cha harakati za ukombozi wa Afrika.

Amesema iliyokuwa Umoja wa Kisovieti iliitambua Tanganyika baada tu ya kupata uhuru mwaka 1961 na ilikuwa nchi ya kwanza kuitambua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.

“Russia si rafiki mpya. Ni rafiki wa jadi ambaye amekuwa pamoja na Tanzania kwa miaka mingi,” amesema Rais Samia.

Amesisitiza kuwa sera ya mambo ya nje ya Tanzania inaendelea kujengwa katika msingi wa kutofungamana na upande wowote na kushirikiana kwa kujenga na mataifa yote bila kujali tofauti za kisiasa au kijiografia.

Hivyo, ameutaja mchango wa nchi ya China kwa Tanzania katika maendeleo ya miundombinu, nafasi ya India kama mmoja wa washirika wakubwa wa biashara na uwekezaji, pamoja na ushirikiano unaoendelea na Japan, Ulaya na Marekani katika sekta mbalimbali.

“Ulaya ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mitaji ya uwekezaji, wakati Marekani ndiyo chanzo kikuu cha watalii wanaotembelea Tanzania na pia mshirika muhimu wa maendeleo,” amesema.

Ameongeza kuwa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwamo wa gesi asilia iliyosindikwa (LNG) na uwekezaji katika sekta ya madini, inahusisha wawekezaji kutoka Ulaya na Marekani.

“Tunapozungumzia LNG na gesi asilia, tunafanya kazi na Ulaya na Marekani. Mradi wa Kabanga Nickel pia unahusisha uwekezaji kutoka Marekani,” amesema.

Rais Samia alikuwa nchini Russia kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais Vladimir Putin.

Akiwa huko, alifanya mazungumzo ya pande mbili na Rais Putin, alipokea shahada ya heshima kutoka Chuo Kikuu cha Peoples’ Friendship University of Russia (RUDN) na kuhutubia wawekezaji katika SPIEF 2026 ambako alitangaza fursa mbalimbali za uwekezaji nchini Tanzania.

Pia, alishiriki kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Urusi na kuwahimiza wawekezaji kuunga mkono azma ya Tanzania ya kufikia uchumi wa Dola 1 trilioni za Marekani ifikapo mwaka 2050.

Licha ya kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, kiwango cha biashara bado ni kidogo.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, miaka mitano iliyopita, mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Russia yameongezeka kutoka Dola 7.5 milioni za Marekani (Sh19.5 bilioni)  mwaka 2020 hadi kufikia Dola 29.5 milioni (Sh76.7 bilioni) mwaka 2025.

Uwekezaji mkubwa zaidi wa Russia nchini Tanzania ni Mradi wa Uranium wa Mkuju River wenye thamani ya Dola 1.2 bilioni unaotekelezwa mkoani Ruvuma na Kampuni ya Mantra Tanzania Ltd, ambayo ni tanzu ya shirika la nishati ya nyuklia la Urusi, Rosatom.